Na
Mary Gwera, Mahakama ya Tanzania
Katika muendelezo wa
mafunzo ya kubadilishana uzoefu juu ya uendeshaji wa mashauri ya jinai, Majaji
wanaoshiriki katika mafunzo haya wapatiwa somo
juu ya Sheria ya Utakatishaji Fedha ‘Money Laundering.’
Akitoa somo hilo mapema
jana, katika Ukumbi wa Hazina mjini Dodoma, Bw. Robert Kassim, ambaye ni
Mwanasheria- Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu ‘Financial Intelligency Unit’
(FIU) - Wizara ya Fedha na Mipango alisema elimu juu ya Sheria hii kwa Wahe.
Majaji inalenga katika kuendelea kuwajengea uelewa zaidi kutokana na kesi za
aina hiyo kuletwa Mahakamani.
“Kitengo cha
Utakatishaji Fedha kinaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ikiwa ni
pamoja na Wapelelezi, Waendesha Mashitaka, Mabenki na Sekta nyingine ili wote
kwa pamoja tuwe na uelewa wa pamoja dhidi ya vitendo hivi haramu ambavyo
huchangia katika kurudisha maendeleo ya nchi nyuma,” Alisema Bw. Kassim.
Alisisitiza kuwa suala
la Utakatishaji Fedha lina madhara mengi kwa Taifa, akitaja kuwa ni pamoja na kurudisha
nyuma ushindani wa kiuchumi, kushusha hadhi na utengamano wa Taasisi za kifedha
na mifumo yake, pia kufifisha uwekezaji wa mitaji ya kimataifa.
Kwa upande wake, Jaji
Mfawidhi, Mahakama Kuu-Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Rehema
Mkuye alisema kuwa somo hilo ni muhimu sana kulielewa zaidi, akifafanua kuwa
kati ya mashauri ambayo Divisheni yake itashughulika nayo ni pamoja na Mashauri
ya Utakatishaji fedha na uhujumu uchumi.
“ Somo juu ya Sheria
hii ni muhimu, mafunzo kama haya ni vyema yakaendelea kutolewa zaidi na zaidi
hata kwa makundi mengine kama Wapelelezi na watu tunaoshirikiana nao katika
uendeshaji wa kesi ili kujenga uelewa wa pamoja na hatimaye kurahisisha
usikilizaji wa mashauri ya namna hii,” alisisitiza Mhe. Mkuye.
Naye, Jaji Mfawidhi,
Mahakama Kuu, Kanda ya Tanga, Mhe. Iman Aboud, alisema kuwa kwa kuwa Mashauri
ya Utakatishaji Fedha ni miongoni mwa Mashauri yenye maslahi kwa jamii ni vyema
yakashughulikiwa kwa haraka kutokana na mvuto wake kwa jamii ‘public interest.’
“Miongoni mwa kesi
ambazo jamii inapenda zishughulikiwe kwa haraka ni pamoja na kesi za
Utakatishaji Fedha, hivyo uelewa zaidi juu ya Sheria hii ya Utakatishaji wa
Fedha ni muhimu sana,” alisema Jaji Aboud.
Katika hatua nyingine,
Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi alisema
kuwa ujengaji wa uelewa wa pamoja kuhusu sheria yenyewe pamoja na mikataba ya
Kimataifa na Kikanda ambayo Tanzania imeridhia na ni Mwanachama.
“Uelewa huu kwa sasa ni
muhimu zaidi kuendana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii ambayo Tanzania
inakabiliana nayo, ambapo idadi ya makosa ya kutakatisha fedha pamoja na makosa
mengine yanayohusisha ubadhilifu wa mali yameongezeka ukilinganisha na kipindi
cha nyuma, hali hii inailazimu Mahakama kuwa na uelewa wa kutosha wa namna ya
kusikiliza na kutoa maamuzi wa kesi hizo na kwa wakati,” alisisitiza, Mhe.
Jaji, Feleshi.
Mafunzo haya ya siku
tano yaliyoanza tarehe 13.12 na kutarajiwa kumalizika Jumamosi tarehe 17. 12.
2016 yanalenga katika kubadilishana uzoefu juu ya uendeshaji wa Mashauri ya
jinai, taratibu na changamoto mbalimbali zinazowakabili na hatimaye kuja na
mikakati ya pamoja ya jinsi ya kukabiliana nazo.
Aidha kwa mafunzo haya mahsusi chini ya
ufadhili wa pamoja kati ya Mahakama na Serikali ya Uingereza chini ya program
ya STACA yalitanguliwa na mafunzo kwa Mahakimu 173 yaliyofanyika kuanzia tarehe
14 Novemba – 2 Desemba, 2016.
Mwanasheria, Kitengo
cha Kudhibiti Fedha Haramu (Financial Intelligence Unit, FIU), Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Robert Kassim
akitoa somo juu ya elimu ya Utakatishaji Fedha kwa kundi la Wahe. Majaji
wanaoshiriki katika mafunzo ya kuubadilishana uzoefu juu ya uendeshaji wa
mashauri ya jinai yanayoendelea katika Ukumbi wa Hazina uliopo mkoani Dodoma.
Wahe.
Majaji wakimsikiliza mtoa mada ya Utakatishaji Fedha.
Jaji wa Mahakama Kuu,
Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akitoa mada katika mafunzo ya
Majaji, aliyeketi pembeni ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Wilfred Dyansobera, ambaye pia ni mshiriki wa Mafunzo hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni