Na Mary Gwera,
Mahakama ya
Tanzania
Nchi
yoyote yenye kuzingatia misingi ya Utawala wa Sheria, huchangia kwa kiasi
kikubwa kuleta amani na Maendeleo ya kiuchumi katika taifa husika.
Hii
inajidhihirisha kupitia Kaulimbiu ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini,
2017 ambayo ni ‘Umuhimu wa Utoaji Haki kwa wakati kuwezesha Ukuaji wa
Uchumi.’
Kauli mbiu hii ina maana
ya kuwa kukamilishwa mapema kwa mashauri ya jinai, Rushwa na Uhujumu Uchumi
ambayo yanaendeleza amani na usalama katika jamii ni chachu ya maendeleo ya
uchumi.
Hivi
karibuni Mahakama ya Tanzania iliadhimisha Siku ya Sheria nchini, ambayo
huashiria kuanza rasmi kwa mwaka wa Mahakama ambapo shughuli za usikilizaji wa
Mashauri huanza rasmi.
Kwa
mwaka huu, sherehe za Siku ya Sheria nchini ziliadhimishwa rasmi tarehe
02.02.2017, ambapo kila Mkoa uliadhimisha, kwa upande wa Dar es Salaam, Sherehe
hizi zilifanyika katika Kiwanja cha Mahakama kilichopo Chimala karibu na
Hospitali ya ‘Ocean road’ ambapo Mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Aidha;
Sherehe za Kilele cha Siku ya Sheria nchini zilitanguliwa na Maonyesho ya Wiki
ya Sheria yaliyoanza rasmi Januari, 28 hadi Februari 01, 2017, Maonyesho ya
Wiki ya Sheria yalifanyika nchi nzima lengo kuu likiwa ni kutoa elimu ya Sheria
kwa Wananchi juu ya huduma na taratibu mbalimbali za Kisheria.
Kwa
upande wa Dar es Salaam, Maonyesho ya Wiki ya Sheria yalifanyika katika Viwanja
vya Mnazi Mmoja jijini humo, Wadau walioshiriki ni pamoja Mahakama yenyewe kama
mwenyeji, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mahakama Kuu Zanzibar, Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Mahakama (AGC), Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),
Mkemia Mkuu wa Serikali, Chuo cha Uongozi wa Mahakama IJA, Mkuu wa Kitivo cha
Sheria, Chuo Kikuu Huria, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Wengine
ni Tume ya Kurekebisha Sheria, Taasisi zinazotoa msaada wa Kisheria (Legal
Aid), TAKUKURU (PCCB), Polisi, Magereza, Msajili, Mabaraza ya Ardhi, Chama
cha Wanasheria
Katika maonesho hayo kulikuwa na uwakilishi wa ngazi
zote za Mahakama kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama ya Rufaa ambapo
taratibu/huduma mbalimbali za Kimahakama zilitolewa kwa wananchi waliopata
fursa ya kutembelea mabanda ya Maonesaho hayo yaliyofanyika katika Viwanja vya
Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Lengo la
kufanyika kwa Maonesho hayo ilikuwa ni kutoa fursa kwa wananchi kufahamu
shughuli za Mahakama pamoja na Wadau wa Sekta Sheria kwa ujumla, vilevile
kuwawezesha wananchi kupata elimu juu ya taratibu mbalimbali Mahakama katika
upatikanaji wa haki.
Aidha,
Sherehe za kilele cha Siku ya Sheria nchini zilihudhuriwa na Wageni mbalimbali
akiwepo Spika wa Bunge la Tanzania, Waziri wa Katiba na Sheria, Katibu Mkuu
Kiongozi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama
nchini, Mwendesha Mashtaka (DPP), TLS, Majaji Wastaafu, Mabalozi, Viongozi wa dini mbalimbali n.k.
Aidha
katika Sherehe hizo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizungumzia
masuala kadhaa ambayo ni pamoja na:-
Kutoa
pongezi kwa kasi nzuri ya Uondoshaji wa
Mashauri, ambapo katika taarifa iliyotolewa na Kaimu Jaji Mkuu alisema kuwa
‘Pamoja
na changamoto inayotukabili ya uwiano usio sawa wa idadi ya Majaji na Mahakimu
na Watumishi wengine kama Wasaidizi wa Kumbukumbu; wastani wa jumla ya
umalizaji wa mashauri upo wa asilimia 101
(101%), yaani kwa tafsiri ya kila mashauri mia moja (100) yanayosajiliwa uwezo
wa kuyamaliza ni asilimia 101
(101%).
Kwa mwaka wa Mahakama ulioisha Desemba,
2016, jumla ya mashauri 276,147
yalisajiliwa na mashauri yaliyosikilizwa na kukamilika yalikuwa ni 279,331.
Mashauri ambayo yapo bado Mahakamani
ilipofika Desemba, 2016 ni jumla 56,531
na kati ya hayo, yenye sifa ya kuitwa ya zamani (backlogs) ni mashauri 3,618 na ambayo ni sawa na wastani wa asilimia sita (6%) tu.
Mhe. Prof. Jaji Juma aliongeza kuwa kati
ya mashauri 249 yaliyosajiliwa
Mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi ambapo ya Ubunge yalikuwa 53 na Udiwani 196. Hadi kufikia Desemba 30, 2016 mashauri 52 yaliyohusu ubunge yaliamuliwa, hivyo kubaki na shauri moja (1) tu. Mashauri ya udiwani
yalisikilizwa na kuamuliwa yote. Mashauri ya uchaguzi wa Ubunge yalisikilizwa
mfululizo kuanzia mwezi Juni mpaka Oktoba, 2016 yakijumuisha Majaji 29 kwa yale
ya Ubunge; na Mahakimu kwa mashauri ya Udiwani.
Ari hii ya Kasi ya usikilizwaji wa
Mashauri mbalimbali, ilimfurahisha Mhe. Rais na kupelekea kutoa pongezi kwa
Mahakama kwa kazi nzuri waliofanya katika mwaka wa Mahakama uliopita.
Mbali na pongezi, Mhe. Rais alitoa
changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na ‘Mashauri ya kodi na fedha
zilizokwama kutokana na wadaawa na masjala za Mahakama kufanya mchezo maarufu
wa ‘Parking’ kuzuia mashauri yasimalizike na kuikosesha serikali mapato.’
Katika hili Mhe. Rais aliiomba Mahakama kutilia mkazo katika mashauri haya ili
kuingizia Serikali mapato.
Hata hivyo; Mahakama pamoja na jukumu
lake kuu la kutoa haki,imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha nchi inajenga
na kuweka mazingira bora ya biashara shindani ili kuvutia uwekezaji.
Baadhi ya Watumishi wa Mahakama na Wageni wengine
waalikwa wakiwa katika sherehe za Siku ya Sheria nchini, iliyofanyika Februari
02, 2017.
Kwa upande wake, Kaimu Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma, katika hotuba yake ya Siku ya Sheria nchini,
alisema kuwa Mahakama ya Tanzania imedhamiria kutimiza ahadi yake ya
kuhakikisha wadaawa wanapata nakala ya hukumu ndani ya siku 21 na mwenendo wa
shauri ndani ya siku 30 tangu hukumu iliposomwa.
“Wananchi wanastahili kupata nakala za
hukumu kwa wakati. Sheria inataka kila Jaji au Hakimu asome hukumu ndani ya
siku 90 tangu kesi ilipomalizika
kusikilizwa,” alisisitiza Kaimu Jaji Mkuu.
Miongoni mwa masuala ambayo Kaimu Jaji
Mkuu aliyatilia msisitizo/mkazo katika hotuba yake pia ni pamoja na matumizi ya
TEHAMA Mahakamani ili kurahisisha taratibu mbalimbali za Mahakama.
“Ifikapo Desemba, 2018, kulingana na
ramani (Road map) ya matumizi ya TEHAMA, kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali
Mtandao (E-govt Agency), tuweze kuanza matumizi kamili ya TEHAMA kwenye kazi za
Kimahakama na Kiutawala,” alisema Jaji Juma.
Aliongeza kuwa ujenzi na ukarabati wa
miundombinu ya kisasa ya Mahakama pia unaenda sanjari na matumizi ya hatua kwa
hatua ya TEHAMA, vilevile kuhakikisha taratibu za masuala ya fedha ndani ya
Mahakama zinaendeshwa kwa kutumia mifumo ya kisasa ya TEHAMA mpaka kwenye ngazi
ya Mikoa/Wilaya.
Alienda mbali na kuongeza kuwa Mfumo wa
TEHAMA wa ukusanyaji wa Takwimu za Mashauri (JSDS) utaboreshwa kuwa sehemu ya
mfumo wa kisasa. Matumizi makubwa ya Watanzania ya simu za kisasa (smart phone)
yanarahisisha sana azma hii ya kuleta mabadiliko makubwa ya utendaji kazi wa
kizamani na wenye tija hafifu.
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Jaji Prof. Ibrahim
Juma akisoma risala yake ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika Februari 02,
2017, waliopo nyuma ya Mhe. Kaimu Jaji Mkuu ni baadhi ya Wahe. Majaji wa
Mahakama ya Tanzania.
Jitihada mbalimbali zifanywazo na
Mahakama kwa sasa kama ujenzi na ukarabati wa miundombinu, matumizi ya TEHAMA
n.k zinalenga katika kuboresha na kusogeza huduma ya utoaji haki kwa wananchi.
Naye, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe.
George Masaju katika hotuba yake ya Siku ya Sheria nchini aliitaka Mahakama
kukamilisha mapema mashauri ya jinai, Rushwa na Uhujumu Uchumi ambayo
yanaendeleza amani na usalama katika jamii ni chachu ya maendeleo ya uchumi.
“Majaji, Wasajili, Mahakimu, Mawakili wa
Serikali, Mawakili wa Kujitegemea na wadau wengine wa Mahakama, ikiwemo vyombo
vya upelelezi wa jinai, Rushwa na Uhujumu uchumi, Mabaraza ya kodi, Ardhi,
Ushindani na mengineyo wazingatie matakwa ya Katiba ya nchi, Sheria na Kanuni
katika utoaji haki kwa wakati,” alieleza Masaju.
Siku ya Sheria nchini, hutoa nafasi kwa
Mahakama pamoja na wadau wake wakuu ambao ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali pamoja na Chama cha Mawakili Tanganyika kutoa hotuba juu ya Mafanikio
na changamoto zinazoikabili Sekta ya Sheria katika mwaka husika.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha
Mawakili Tanganyika, Bw. John Seka aliihakikishia Mahakama kupitia hotuba yake
kuwa Chama hicho kipo tayari wakati wowote kushirikiana na Mahakama ili
kuhakikisha kuwa utoaji haki unatamalaki.
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma
akikagua gwaride maalum lililoandaliwa, ukaguzi wa gwaride hili huashiria
kuanza rasmi kwa shughuli za Mahakama kwa mwaka husika.
Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini
hutumika kama njia mojawapo ya kukutana na Wadau ili kupata michango/maoni
mbalimbali ya Wadau na wananchi kwa ujumla yote yakitumika na Mahakama
kujitathmini na kuona wapi imepwaya ili kuendelea kufanya maboresho katika
suala zima la utoaji haki nchini.
Akiongea na Mwandishi wa Makala hii,
Msajili Mkuu- Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati alisema kwa mwaka
huu mpya wa Sheria, Mahakama imejipanga kuhakikisha inaendelea kushughulikia
mlundikano wa kesi/mashauri ya muda mrefu ‘case backlog’.
“Kama unavyojua kwa sasa, Mahakama
imejikita katika kufanya maboresho kadhaa wa kadhaa, miongoni mwa maboresho
hayo ni pamoja na kushughulikia mashauri ya muda mrefu, na jitihada hizi
zimezaa matunda hata kwa mwaka jana ambapo hadi tunamaliza mwaka tulikuwa
mlundikano sifuri (zero cases) katika ngazi za Mahakama za Mwanzo na za
Wilaya,hivyo jitihada hizi zinaendelea hata kwa sasa,” alieleza Mhe. Revocati.
Msajili Mkuu huyo aliendelea kusema kuwa
Mahakama imejiwekea muda maalum wa kushughulikia kesi hadi kumalizika kwake,
ambapo alieleza kuwa kwa ngazi ya Mahakama za Mwanzo kesi inabidi iwe
imekamilika kwa kipindi cha miezi sita, Mahakama za Wilaya/Hakimu Mkazi, mwaka
mmoja na kwa upande wa Mahakama Kuu/Rufani miaka miwili (2), na suala hili tunalisimamia
kwani pia Mpango Mkakati wetu wa Mahakama kupitia moja ya nguzo zake inaelekeza
kuboresha suala zima la utoaji haki nchini.
Mahakama
ya Tanzania huadhimisha Siku ya Sheria nchini ndani ya wiki ya kwanza wa mwezi
Februari kila mwaka, siku hii huashiria mwanzo wa shughuli za Mahakama kwa
mwaka husika, maudhui ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini
kwa mwaka huu ni ‘Umuhimu wa Utoaji Haki kwa wakati kuwezesha Ukuaji wa
Uchumi.’
Kwa mara ya kwanza, Mahakama ya Tanzania
iliadhimisha rasmi Siku ya Sheria nchini mwaka 1997 ambapo Viongozi wa Dini
walitoa dua ya kuombea Majaji, Mahakimu na Wanasheria ili watimize wajibu wao
mzito wa utoaji haki nchini. Hata hivyo mnamo Machi 1, 1996 kulifanyika ibada maalum
ya kuwaombea Majaji na Mahakimu ili wasikilize vyema mashauri yoyote na
hasahasa ya uchaguzi Mkuu uliofanyika 1995. Huu ulikuwa uchaguzi wa kwanza wa
vyama vingi na hivyo kulikuwa na mashauri mengi ya uchaguzi.
Aidha; mnamo mwaka 2007, Sherehe za Siku ya Sheria
nchini zilihudhuriwa na Mheshimiwa Rais kwa mara ya kwanza na Mheshimiwa Rais
alipata nafasi ya kutoa hotuba na huu ndio ulikuwa mwanzo wa mgeni rasmi kutoa
hotuba.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni