MAHAKAMA Kuu, Kanda ya
Mwanza imejipanga kuondoa Mashauri yote yenye umri zaidi ya miaka miwili
yaliopo katika Kanda hiyo ili kuendana na azma ya Mahakama ya Tanzania ya
kutokuwa na mlundikano wa kesi katika Mahakama za ngazi zote nchini.
Hayo yalisemwa na Jaji
Mfawidhi, Kanda ya Mwanza, Mhe. Robert Vincent Makaramba katika Mahojiano
maalum aliyofanya na Mwandishi wa habari hii hivi karibuni ofisini kwake,
Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza.
Pichani ni Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, Mhe. Robert Vincent Makaramba.
“Mbali na agizo la
Mahakama la kutaka kila Mahakama ishughulikie mashauri ya muda mrefu
Mahakamani, Mahakama, Kanda ya Mwanza tayari tulishajipanga katika kuondosha
Mashauri haya, na kila Jaji amejipangia namna ya kusikiliza na kutolea maamuzi
mashauri hayo,” alisisitiza Jaji Makaramba.
Aliongeza kuwa ili
suala hili liweze kufanikiwa ni vyema kuwa kitu kimoja na Wadau wa Mahakama
kuwezesha zoezi hili kufanikiwa na vilevile kuwa na rasilimali wezeshi kama
fedha.
Afisa Habari, Mahakama, Bi. Mary Gwera akiwa katika Mahojiano maalum na Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, Mhe. Robert Makaramba ofisini kwake, Mahakama Kuu-Mwanza.
Aidha; ili kuweza
kufanyika kwa zoezi hili la kuondoa mlundikano wa Mashauri Mahakamani, Majaji
wote saba (7) wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza pamoja na Viongozi wengine wa
Mahakama hiyo ikiwa ni pamoja na Naibu Msajili na Mtendaji wa Mahakama walikutana
na Wadau wa Mashauri ya Jinai na Madai ili kujadili namna bora ya kuondosha
mashauri yenye umri wa miaka miwili Mahakamani.
Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza wakiwa katika kikao pamoja na Wadau wa Mahakama wa Kanda hiyo (hawapo pichani) kilichofanyika hivi karibuni, wa kwanza kulia ni Naibu Msajili, Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, Mhe. Eugenia Rujwahuka.
Kwa upande wake, Naibu
Msajili, Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, Mhe. Eugenia Rujwahuka alisema kuwa zoezi la kuondosha mashauri haya linatakiwa
liwe limekamilika kufikia mwezi wa tano mwaka huu.
“Kikao hicho
kilichojumuisha Wadau mbalimbali kama Mawakili, Waendesha Mashitaka, Magereza
n.k, kililenga katika kujipanga ili kufanikisha usikilizaji wa Mashauri ya
Mauaji katika vikao maalum vitakavyoanza Aprili, 24, mwaka huu hadi hadi Mei, 24
mwaka huu,” alisema Naibu Msajili.
Baadhi ya Watumishi wa Mahakama na Wadau wakiwa katika kikao hicho.
Mhe. Rujwahuka aliongeza
kuwa jumla ya Mashauri 107 yamepangwa kusikilizwa katika vikao hivyo ambavyo
vitafanyika Tarime, Sengerema, Magu, Geita, Mwanza na Musoma.
Hata hivyo; katika
kikao hicho kati ya Mahakama na Wadau wake walikubaliana kushirikiana ili
kufanikisha zoezi zima la uondoshaji wa mrundikano wa mashauri.
Mmoja kati ya Wadau walioshiriki katika kikao hicho akichangia jambo.
Katika muendelezo wa
uboreshaji wa huduma ya Utoaji haki nchini Mahakama ya Tanzania imedhamiria
kuondoa mlundikano wa kesi katika Mahakama zake.
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Mwanza akiongea jambo katika kikao hicho, pamoja nae wanaoonekana katika picha ni baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza ambayo ina jumla ya Majaji saba (7).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni