Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu Kanda ya Tanga Mhe. Imani Abood akielezea utekelezaji wa Mpango Mkakati wa
Miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania katika Kanda ya Tanga leo ofisini kwake
jijini Tanga.
Na
Lydia Churi-Mahakama, Tanga
Mahakama ya Tanzania
imeshauriwa kuwa na Mpango endelevu wa kuwajengea uwezo watumishi wake wa ngazi
zote ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tanga Mhe. Imani Abood alitoa ushauri huo leo
jjini Tanga alipokuwa akielezea utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano
wa Mahakama ya Tanzania katika Kanda yake.
Alisema pamoja na kuwa
Mahakama inaendesha mafunzo mbalimbali kwa watumishi wake lakini mafunzo hayo
hayana budi kutolewa kwa watumishi wote kuanzia ngazi ya chini mpaka ngazi ya juu
kabisa katika Mahakama.
Akizungumzia nguzo ya
pili ya Mpango Mkakati wa Mahakamainayohusu upatikanaji wa haki kwa wakati, Mhe.
Abood alisema ni muhimu suala la mafunzo likapewa kipaumbele hasa kutokana na
kukua kwa sayansi na Teknolojia.
Alisema , hivi sasa katika
Mahakama upo ushahidi wa kielekitroniki
unaotolewa hivyo ni muhimu mafunzo yakatolewa ili kuleta ufanisi katika suala zima
la utoaji wa haki.
Akizungumzia mikakati
iliyowekwa na kanda yake ili kuondosha mashauri mahakamani kwa wakati, Jaji
Abood alisema wanakusudia kuziwekea umeme Mahakama za Mwanzo kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na kuwapatia Mahakimu wote katika kanda yake vitendea kazi kama vile laptops
na printer ili ziwarahisishie kutoa hukumu kwa wakati.
Alisema hivi sasa
Mahakimu katika Mahakama za Mwanzo hulazimika kupeleka hukumu walizoandika kwa
mkono ili zikachapishwe kwenye Mahakama za wilaya ambapo kuna umeme.
Alisema licha ya changamoto
hizo, bado watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Tanga wanakuwa wakifanya kazi kwa
bidii na Mahakimu kuhakikisha hukumu zinatolewa kwa wakati ikiwa ni pamoja na na
wananchi kupatiwa nakala za hukumu ndani ya siku 21 zilizopangwa.
Mkakati mwingine uliowekwa
ili kuondosha mashauri mahakamani ni pamoja na, kufanya vikao na Mahakimu
wafawidhi wa wilaya pamoja na wadau wa Mahakama ili kurahisisha kazi kwa kuwa kila
mdau anaposhughulikia eneo lake shauri huisha mapema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni