Na
Lydia Churi- Mahakama, Tanga
Mahakama Kuu Kanda ya
Tanga inakusudia kuwanunulia Mahakimu wake 67 kompyuta Mpakato (Laptops) ili
kurahisisha kazi zao na kuondosha mashauri kwa wakati katika Mahakama mbambali
za mkoa wa Tanga.
Akizungumza kwa niaba
ya Mtendaji wa Mahakama Kuu kanda ya Tanga, Afisa Utumishi wa Kanda hiyo, Bwana
Farid Mnyamike amesema kompyuta hizo zitawasaidia waheshimiwa Mahakimu katika
kuandika hukumu ili wananchi waweze kupati haki kwa wakati.
Alisema katika kanda yake,
baadhi ya Mahakama zina uhaba wa watumishi hasa Makatibu Muhtasi pamoja na
vitendea kazi jambo ambalo limekuwa likichelewesha utolewaji wa hukumu pamoja na
upatikanaji wa nakala za hukumu kwa wakati. Aliongeza kuwa kwa Mahakimu
kupatiwa kompyuta hizo kutarahisisha upatikanaji wa haki.
Aidha, Afisa Utumishi
huyo alisema hivi sasa Mahakama Kuu kanda ya Tanga inao mpango wa kuhakikisha
inazipatia umeme baadhi ya Mahakama za Mwanzo kupitia Mradi wa Umeme vijijini
(REA) ili kurahisisha upatikanaji wa nakala za hukumu kwa wakati.
Mahakama ya Tanzania
ilimwekea malengo kila Hakimu nchini ya kuhakikisha anasikiliza kesi zaidi ya 250 kwa mwaka ili kuondosha mrundikano wa mashauri yaliyoko kwenye
Mahakama mbalimbali nchini.
Bwana Mnyamike aliitaja
mipango mingine iliyowekwa na Kanda yake katika kuitekeleza nguzo ya pili ya
Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania kuwa ni kuwapeleka Mahakimu
wenye mashauri machache kwenye Mahakama zenye mashauri mengi ili kuhakikisha mashauri
yote ya muda mrefu yanaondoshwa na yaliyofunguliwa yanamalizika kwa wakati.
Kuhusu Mradi wa kupambana na Rushwa ndani ya Mahakama (STACA) Bwana Mnyamike alisema umeleta mageuzi makubwa ndani ya mahakama kwa kuwa kupitia vilivyosambazwa na Mahakama kama vile pikipiki na baiskeli zimewawezesha Mahakimu kutembelea Mahakama zenye uhaba wa Mahakimu na kumaliza kesi kwa wakati. Aidha, mradi huo pia umewezesha watumishi wengine wa Mahakama kutoa huduma kwa wakati.
Ili kuleta mabadiliko ndani ya Mahakama, Mahakama ya Tanzania iliandaa Mpango Mkakati wa Miaka mitano 2015-2020 unaotekelezwa kupitia nguzo tatu ambazo ni Utawala bora, Upatikanaji wa Haki kwa Wakati na pamoja na kurudisha na kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama.
Afisa TEHAMA wa
Mahakama Kuu Kanda ya Tanga Bi Amina Said akielezea kwa niaba ya Msajili wa Mahakama Kuu kanda hiyo kuhusu takwimu za usikilizwaji wa Mashauri katika kanda hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni