Alhamisi, 13 Aprili 2017

MAHAKAMA NA WADAU WAKE WAFANYA MAREKEBISHO YA KANUNI ZA MADALALI WA MAHAKAMA NA ‘ADR’

Na Mary Gwera
Madalali wa Mahakama nchini wametakiwa kufanya kazi kwa kufuata maadili ya kazi hiyo ili kuenda sambasamba na azma ya Mahakama ya Tanzania ya kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi.

Hayo yalizungumzwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Aisha Nyerere jijini Dar es Salaam mapema Aprili 13, alipokuwa akifungua kikao kati ya Mahakama na Wadau wake kilicholenga kukusanya maoni ili kurekebisha kanuni za Madalali wa Mahakama na za Usuluhishi wa Migogoro kwa njia Mbadala (ADR). 

Aidha; Jaji Nyerere aliongeza kuwa Madalali wengi wamekuwa wakikiuka taratibu mbalimbali, hali ambayo inapelekea taswira ya Mahakama kuchafuka.

“Madalali wengi wamekuwa na tabia zisizofaa, hivyo nawaambia Madalali mliopo hapa leo muwafikishie ujumbe na wengine ambao hawapo hapa kuwa na maadili katika utekelezaji wa majukumu yenu kwani wengi wenu mnakiuka taratibu na kanuni za utendaji kazi zilizopo,” alisisitiza, Jaji Nyerere ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho.

Kwa upande wake, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. John Kahyoza alisema kuwa Mahakama imeamua kufanya marekebisho ya kanuni hizo kutokana na kuonekana kuwa na mapungufu kadhaa.

“Lengo la kikao hiki pamoja na Wadau tuliowaalika, ambao ni Mawakili, Madalali wa Mahakama, Wanasheria, Wanataaluma wa Sheria na Walimu kutoka Vyuo Vikuu ni kupata maoni yao ili kuboresha rasimu ya kanuni za kusimamia Madalali na kuweka bayana miongozo ya utendaji kazi,” alieleza Mhe. Kahyoza.

Aliongeza kuwa hatua hii inafanyika kwa lengo la kuhakikisha kuwa Mashauri ya Madai yanasikilizwa kwa haraka na kuhakikisha kuwa mshindi anapata haki yake kwa muda muafaka.

Aliendelea kusema kuwa kanuni hizo zinaboreshwa kwa kuangalia upya sifa za Madalali, kuziba mianya kwa madalali kudanganya thamani ya mali wanazouza, kudhibiti Madalali bandia na kadhalika.

Katika kikao hicho, wadau hao walitoa maoni yao ambayo yamechukuliwa na yatapelekwa katika Kamati ya Kanuni ya Mahakama kwa ajili ya kuyaingiza katika rasimu hiyo ya kanuni na hatimaye itapelekwa kwa Mhe. Jaji Mkuu kwa ajili ya kutia sahihi na kuanza rasmi kwa utekelezaji wake.
 Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Aisha Nyerere akifungua rasmi kikao cha Mahakama na Wadau cha Marekebisho ya Kanuni za Madalali wa Mahakama na ADR, Mhe. Jaji Nyerere ndiye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho.
Msajili, Mahakama ya Rufani, Mhe. John Kahyoza akiongea na Wadau (hawapo pichani) katika kikao cha Marekebisho ya Kanuni za Madalali na ADR kilichofanyika Aprili 13, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere.
Wakili wa Kujitegemea, Bw. Francis Stolla akichangia mada katika Mkutano huo.
Wadau wakiwa kikaoni.
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, Mhe. Aisha Nyerere akifafanua jambo alipokuwa kwenye kikao hicho.
Meza Kuu wakiwa katika picha ya pamoja na wadau walioshiriki katika majadiliano hayo ya kutoa maoni/mapendekezo ya marekebisho ya kanuni za Madalali na Usuluhishi wa Migogoro kwa njia Mbadala 'ADR.'

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni