Kaimu Jaji Mkuu wa
Tanzania Mheshimiwa Prof.Ibrahim Juma amewaagiza Majaji wote nchini kuzipa umuhimu
wa kipekee wa kuzisikiliza na kuzimaliza kwa haraka kesi zote zenye mvuto kwa
jamii na zenye maslahi kwa Umma ili kuongeza imani ya wananchi juu ya Mahakama kama
chombo cha utoaji wa haki.
Akifungua mafunzo ya
Majaji wa Mahakama ya Rufani pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania alizitaja kesi zinazotakiwa kusikilizwa na kumalizwa
kwa haraka kuwa ni zile zinazohusu dawa za kulevya, ujangili, ugaidi, Mauaji ya
watu wenye ulemavu wa ngozi pamoja na mauaji ya vikongwe kwa imani za
kishirikina.
Kaimu
Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma akifungua Mafunzo ya Pamoja
ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania leo
jijini Arusha.
|
Prof. Juma alizitaja
kesi nyingine zinazotakiwa kupewa umuhimu wa kipekee kutokana na mvuto wake kwa
jamii kuwa ni pamoja na kesi za rushwa kubwa, utakatishaji wa fedha, matumizi mabaya
ya madaraka kwa viongozi, na kesi zinazohusu changamoto za ukuaji wa demokrasia
na uendeshaji wa masuala ya siasa.
Kesi nyingine
zilizotajwa na Jaji Mkuu katika kupewa umuhimu wa kipekee ni zile zinazohusu miradi mikubwa kama Reli,
mashamba makubwa ya uwekezaji, gesi, ujenzi wa barabara, kesi za mabenki na kesi
zinazohusisha kundi kubwa la watu zinazogusa migogoro ya umiliki wa ardhi na
migogoro ya wakulima na wafugaji.
“Tukichukua hatua za
dhati kuhakikisha kesi hizi zinaisha kwa wakati tutakuwa tumetoa mchango mkubwa
katika kukuza uchumi na kuongeza imani ya wananchi kwa Mahakama”, alisema Kaimu
Jaji Mkuu.
Alisema ni Jambo muhimu
kwa Mahakama kuzipa umuhimu wa kipekee kesi hizi hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inatekeleza mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2016/17-2021) ambao kauli mbiu yake ni “kujenga
uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya
uchumi na Maendeleo ya watu”.
Aidha, Kaimu Jaji Mkuu pia
amewataka Majaji kuangalia namna ya kutoa huduma kwa haraka kwenye makundi yenye
mahitaji maalum kama vile wazee, walemavu na wajane hususan wakati huu ambapo
Mahakama inaelekeza nguvu zaidi katika kuondosha mlundikano wa mashauri
mahakamani.
Aliwakumbusha Majaji
hao kupanga kesi kwa siku kwa kuzingatia masaa kama njia ya kuwaepusha wananchi
wenye kesi mahakamani na adha ya kusubiria kwa muda mrefu kesi zao kuitwa.
Akizungumzia
usikilizwaji wa kesi Mahakamani, Prof. Juma alisema kwa mwaka 2016, Mahakama kuu
ya Tanzania pamoja na divisheni zake zote ilifanikiwa kumaliza kesi kwa idadi
sawa na zilizosajiliwa. Alisema, jumla ya kesi 276,147 zilisajiliwa na kwamba kesi
278,226 zilimalizika. Kesi 57,326 zilibaki mahakamani.
Alisema bado kuna
changamoto ya mlundikano wa kesi kwenye Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu
ambapo lengo kuu la Mafunzo hayo kwa Majaji ni kujadili namna ya kumaliza
mlundikano wa kesi kwenye Mahakama hizi.
Aliongeza kuwa Mahakama
za Mwanzo pekee ndizo zenye mafanikio makubwa ya kutokuwa na mlundikano wa kesi.
Mpaka kufikia Desemba 2016, Mahakama za Mwanzo
zilimaliza kesi zote zenye umri unaozidi miezi sita mahakamani.
Majaji wa Mahakama ya
Rufani na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wanaendelea na Mafunzo ya siku tano
mjini Arusha ambapo wanajifunza mambo mbalimbali yanayohusu utendaji wao wa
kazi likiwemo suala la kuondosha mlundikano wa kesi kwenye Mahakama zote
nchini.
Kaimu
Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma akiwa katika picha ya
pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani mara baada ya kufungua Mafunzo ya pamoja ya Majaji
wote leo jijini Arusha.
Kaimu
Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma akiwa katika picha ya
pamoja na Majaji wote wa Tanzania mara baada ya kufungua Mafunzo ya
pamoja ya Majaji wote leo jijini Arusha.
Kaimu
Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma akiwa katika picha ya
pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania mara baada ya kufungua Mafunzo ya
pamoja ya Majaji wote leo jijini Arusha.
Kaimu
Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma akiwa katika picha ya
pamoja na Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania mara baada ya kufungua
Mafunzo ya pamoja ya Majaji wote leo jijini Arusha.
Kaimu
Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma akiwa katika picha ya
pamoja na Majaji Wanawake mara baada ya kufungua Mafunzo ya pamoja ya Majaji
wote leo jijini Arusha.
Kaimu
Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma akiwa katika picha ya
pamoja na Majaji Wanaume mara baada ya kufungua Mafunzo ya pamoja ya Majaji
wote leo jijini Arusha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni