Na Mary Gwera, Manyara
KAIMU Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Khamis Juma amesifu kasi ya uondoshaji wa Mashauri
katika Mahakama za ngazi za chini nchini akitaja kuwa ni Mahakama za Mwanzo na
Mahakama za Wilaya.
Alisema hayo mapema Mei
9 katika ukumbi ya mikutano wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara alipokuwa
akiongea na Watumishi wa Mahakama Mkoani humo,akiwa katika ziara yake ya kwanza kufanya
tangu kuteuliwa kwake Januari, mwaka huu.
Mhe. Jaji Mkuu
amewapongeza Mahakimu wote nchini ikiwa ni pamoja na Mahakama- Manyara
kuhusiana na kasi ya kuondosha mashauri katika Mahakama za ngazi za chini licha
ya idadi kuonekana kuwa kubwa.
Mhe. Jaji Prof. Juma
alisema kuwa wananchi wengi bado wana Imani na Mahakama yao, hivyo idadi kubwa
ya mashauri imeendelea kufunguliwa katika Mahakama zetu hususani Mahakama za
Chini ambazo ni Mahakama za Mwanzo na Mahakama za Hakimu Mkazi.
“Kwa takwimu tulizo
nazo Mahakama kwa mwaka jana, asilimia 71 ya mashauri yalifunguliwa katika
Mahakama za Mwanzo, huku Mahakama ya Wilaya ikiwa na asilimia 14 ya kesi
zilizofunguliwa kwa mwaka jana, Mahakama za Hakimu Mkazi asilimia 7, Mahakama
Kuu asilimia 5 na Mahakama ya Rufani ikiwa na wastani ya asilimia 0.5,”
alieleza Kaimu Jaji Mkuu.
Aliendelea kusema kuwa
takwimu hizo zinaonesha dhahiri kuwa wananchi bado wana imani kubwa na Mahakama
zetu na hivyo kuwataka Mahakimu na watumishi wote wa Mahakama kwa ujumla
kuongeza bidii katika kuwatumikia wananchi.
Mbali na pongezi hizo,
Mhe. Kaimu Jaji Mkuu amewataka Watumishi wa Mahakama-Manyara kufanya kazi kwa
kuzingatia Mpango Mkakati wa Mahakama ambao ndio dira ambayo itawawezesha
kufikia azma ya kuwa Mahakama bora yenye kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Wengi wenu mnafahamu
kwa sasa, Mahakama ipo katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wake wa miaka
mitano, wenye lengo la kuboresha maeneo mbalimbali Mahakamani ikiwa ni pamoja
na kuboresha huduma ya utoaji haki nchini pamoja na kurejesha imani ya wananchi
kwa chombo hiki,” aliwaambia watumishi hao akiwataka kila mmoja kushiriki
kikamilifu katika utekelezaji huo.
Aidha, Mhe. Jaji Prof.
Juma aliwataka pia watumishi wa Mahakama pia kujikita katika Matumizi ya TEHAMA ili
kurahisisha utendaji kazi huku akitilia mkazo kwa Watumishi pia kufanya kazi
kwa kuzingatia maadili ya kazi.
Awali akisoma hotuba
yake mbele ya Mhe. Kaimu Jaji Mkuu, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu
Mkazi Manyara, Mhe. Devotha Kamuzora alisema kuwa Mahakama katika mkoa huo
zimekuwa zikifanya kazi ya uondoshaji mashauri kwa jitihada ili kuhakikisha
kuwa inaondokana na mlundikano wa kesi.
“Mhe. Kaimu Jaji Mkuu,
kwa upande wetu, Mahakama kanda ya Manyara tumejiwekea mkakati wa kuhakikisha
kuwa kesi yoyote inayoletwa katika Mahakama ya Mwanzo/Wilaya isizidi miezi
mitatu mpaka kukamilishwa kwake, na hili tunalisimamia kuhakikisha tunaondokana
na mlundikano wa mashauri katika Mahakama zetu,” alisema Mhe. Kamuzora.
Ziara ya Mhe. Kaimu
Jaji Mkuu imelenga katika kuangalia utendaji kazi wa Mahakama hizo, mafanikio na
changamoto wanazokabiliana nazo na hatimaye kushughulikia changamoto hizo kwa
ustawi wa Mahakama.
Mhe. Kaimu Jaji
ametembelea Mahakama kadhaa mkoani humo ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Wilaya
Babati, Mahakama ya Mwanzo/Wilaya Hanang, pia kukagua Jengo la Mahakama ya
Hakimu Mkazi Manyara na anaendelea na ziara katika Mkoa wa Arusha.
Zifuatazo ni baadhi ya picha za ziara ya Mhe.Kaimu Jaji Mkuu, Mkoani Manyara.
Kaimu
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.Ibrahim Juma akiongea na Watumishi wa Mahakama
mkoani Manyara (hawapo pichani), miongoni mwa vitu alivyozungumzia ni pamoja na
kuzingatia maadili katika ufanyaji kazi, utoaji wa taarifa sahihi kwa manufaa ya
umma, na matumizi ya TEHAMA.
Mhe.
Prof.Ibrahimu Juma akiendelea kuzungumza na Watumishi wa Mahakama-Manyara,
aliyeketi kushoto ni Kaimu Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe.
Sekela Moshi, kulia ni Mhe. Rumisha, Msajili, Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha.
Hakimu
Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara, Mhe. Devotha Kamuzora
(aliyeketi pembeni wa kwanza) na baadhi ya Watumishi wengine wa Mahakama
mkoani humo wakimsikiliza Mhe. Kaimu Jaji Mkuu pindi alipokuwa akizungumza nao.
Watumishi
wakiendelea kumsikiliza Mhe. Kaimu Jaji Mkuu.
Miongoni
mwa Watumishi wa Mahakama waliohudhuria kikao hicho pamoja na Mhe. Kaimu Jaji
Mkuu.
Mmoja
wa Watumishi akiuliza swali.
Kaimu
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Arusha, akifafanua jambo.
Kaimu
Jaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof.Ibrahim Juma (wa tatu kushoto),
Kaimu Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Sekela Moshi (wa tatu
kulia), Katibu wa Mhe. Kaimu Jaji Mkuu, Mhe. Eliazar Luvanda (wa pili kulia) na
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Mkoa Manyara, Mhe. Devotha Kamuzora (wa
kwanza kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mahakimu wa Mahakama
wa mkoani Manyara.
Mhe.
Kaimu Jaji Mkuu akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Mahakama
walioshiriki katika kikao cha Watumishi na Mhe. Kaimu Jaji Mkuu.
Mhe.
Kaimu Jaji Mkuu akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mahakimu aliowahi
kuwafundisha chuoni, wa kwanza kulia ni Kaimu Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu,
Kanda ya Arusha.
Mhe.
Kaimu Jaji Mkuu akikagua jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi/Wilaya Manyara
lililopo katika ujenzi, kukamilika kwa ujenzi wa Mahakama hiyo kutasaidia
kuondokana na changamoto ya uchakavu wa jengo wanayokabiliana nayo katika
Mahakama ya sasa. (picha na Mary Gwera)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni