Na
Lydia Churi, Mahakama, Songea
Mahakama ya Tanzania
itashirikiana na Wadau wake ili kuhakikisha inawajibika ipasavyo na kufikika
kirahisi ili wananchi wapate haki kwa wakati.
Akizungumza na Mkuu wa
Mkoa wa Ruvuma jana, Jaji Kiongozi- Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand
Wambali alisema Mahakama haitaweza kufanya kazi ya kutoa haki bila kushirikisha
wadau wake.
Alisema Mahakama
kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano hivi sasa iko kwenye Mpango maalum
wa kumaliza kesi zote za zamani ambapo awamu ya kwanza ya Mpango huo iliyoanza mwezi
Aprili, itamalizika leo Mei, 26.
Alisema ili kumaliza
kesi hizo wadau wa Mahakama ni muhimu kwa kuwa wataharakisha na kurahisisha
utendaji wa shughuli za Mahakama .
Akizungumza na
Watumishi wa Mahakama, Kanda ya Songea, Mhe. Wambali amewataka kufanya kazi kwa
kuzingatia weledi na kuachana na vitendo vya rushwa na lugha mbaya kwa wananchi
wanaofika mahakamani kutafuta haki zao.
Alisema kwa kufanya
hivyo taswira ya Mahakama kwa jamii itakuwa ni chanya na Mahakama kuendelea
kuwa kimbilio la wengi.
Jaji Kiongozi ameanza
ziara katika Mahakama Kuu, Kanda ya Songea na Mtwara yenye lengo la kukagua
shughuli za Mahakama na kusisitiza utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka
mitano wa Mahakama (2015-2020).
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Ruvuma, Mhe. Binilith Mahenge amesema endapo Mahakama itatekeleza kwa vitendo
nguzo tatu za Mpango Mkakati wake ni dhahiri kuwa dhana ya Tanzania kuwa na
uchumi wa kati.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni