Na Magreth Kinabo
Hivi karibuni vyombo vya habari vimekuwa
vikiripoti kuhusu habari za vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa watoto.
Kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo,
viongozi mbalimbali wamekuwa wakitoa matamko ambayo yanaitaka jamii
kufahamu haki za mtoto ikiwa ni hatua ya kuwaepusha watoto
wasiathiriwe na tabia hatarishi.
Miongoni mwa viongozi hao ni Makamu wa Rais,
Mhe. Samia Suluhu Hassan, na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu Naibu wake. Dkt. Hamis Kingwallah na viongozi
wengine mbalimbali.
Serikali kwa kushirikiana na
viongozi wa asasi za kiraia na dini mbalimbali wameungana ili
kuhakikisha watoto hao wanakua katika maadili mema na kuweza kutimiza
ndoto zao.
Mbali na hilo, kuhakikisha kwamba watu
wanaowarubuni watoto wanachukuliwa hatua za kisheria.
Ili kukababiliana na athari hizo kwa watoto
kulingana na mazingira ya jiografia ya nchi, Mahakama ya Tanzania
kupitia Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa 2015/2016 hadi 2019/2020,
imejenga Mahakama nyingine ya watoto katika Jiji
la Mbeya hatua ambayo itarahisisha utoaji wa haki kwa wakati.
Kupitia mpango huo nchini,
hivi sasa kuna mahakama mbili za watoto ambazo moja iko katika jiji
la Dares Salaam na nyingine jiji la Mbeya.
Uanzishwaji wa Mahakama hizi mbili unatokana
na dhamira ya Mahakama ya Tanzania, kuhakikisha inaboresha
huduma za utoaji haki na kusongeza
huduma karibu na wananchi.
Mahakama ya Watoto imeanzishwa kisheria kwa
lengo la kushughulikia kesi maalum zinazohusu watoto.
Umri unatambuliwa na Mahakama hiyokuwa ni mtoto
ni mtu aliye na umri wa chini ya 18 kulingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ya mwaka 1977 inavyosema sura ya kwanza, kifungu cha 5 (1) na
Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 pamoja na kanuni zake,
marekebisho ya mwaka 2006.
Jukumu la Mahakama ni kushughulikia makosa
mbalimbali ambayo yanaweza kufanywa na watoto wakiwa katika maeneo ya shuleni,
mitaani na sehemu nyinginezo.
Mambo mengine ambayo yanayashughulikiwa na
Mahakama hii ni pamoja na taratibu za kuasili watoto na mambo ambayo yanaweza
kujitokeza kutokana na mchakato mzima wa kufanya hivyo, ikiwemo kupokea
mashauri ya madai.
Usikilizaji wa mashauri katika Mahakama hii,
hufanyika faragha ili kulinda maslahi ya mtoto.
Hivyo, jamii inapaswa
kuzifahamu haki za mtoto kama vile haki ya kuishi,
kupata huduma bora za afya, mahali pa kuishi, kupata elimu, haki ya
kutambuliwa, haki ya kurithi mali, haki ya kutonyanyaswa, ikiwemo kutofanyiwa
vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Kwa mujibu wa taarifa ya
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Sihaba Nkinga, alipokuwa
akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuzuia ukeketaji iliyofanyika
Desemba 5, mwaka 2016, Sihaba Nkinga, alisema hali bado ni mbaya.
Katibu Mkuu huyo alifafanua kwamba taarifa
zinaonyesha kuwa mtoto mmoja kati ya watatu wa kike na mtoto mmoja wa kati ya
saba wa kiume walifanyiwa ukatili wa kingono.
Kupitia maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya
Pangani, mkoani Tanga, Bi Zainabu Issa ametaka jamii ipige vita vitendo vya
ukatili dhidi ya watoto, ili kuwawezesha kufikia ndoto zao ikiwa ni hatua ya
kuwawezesha ustawi wa maisha yao na hatimaye kulijenga taifa la kesho.
“Ninasema kesi dhidi ya ukatili wa watoto sasa
zisizidi miezi sita au mwaka, kesi zisikae, muda mrefu Mahakamani. Ninasema
sasa mtu akipatikana na hatia ya kumpa ujauzito mwanafunzi au kubaka afungwe
miaka 30 jela,” alisema Mkuu huyo wa wilaya ya Pangani.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali
Appi akizungumza wakati wa maadhimisho hayo jijini Dar es Salaam, alipiga
marufuku vitendo vya baadhi ya walimu kuwafungia geti wanafunzi wanapochelewa
kufika shuleni hatua inayowapelekea kushindwa kuingia shuleni na badala yake wanaweza
kuwasababishia watoto kujiunga na makundi yenye tabia hatarishi.
Ili kuweza kuwaepusha watoto kutoathiriwa
na tabia hatarishi, Mkuu huyo Appi alipendekeza walimu watumie adhabu mbadala
kwa wanafunzi wanapofanya makosa wakiwa shuleni.
Alisema adhabu mbadala zinaweza
kutolewa na walimu, wakati wa kipindi cha mapunziko.
Naye Hakimu Mkuu wa Mahakama ya
Mwanzo Mjini Mbeya, Mhe. Onesmo Zunda
akizungumzia kuhusu uzoefu wa usikilizaji kesi za watoto
zinazohusiana na madai na kusema kuwa amekuwa kesi za ndoa na
talaka nyingi zinatoka maeneo ya vijijini kuliko mjini.
“Kuna changamoto katika kusikiliza
kesi hizi. Miongoni mwa changamoto tunazokabiliana nazo ni mgawanyo
wa mali hasa pale inapotokea mtu amefariki dunia au wazazi
kutengana mmojawapo akiwa ana fedha au mali au kaoa mke mwingine.
Mara nyingi mgawanyo wa mali huwa unaleta malalamiko
katika baadhi ya familia,” alisema Mhe. Zunda.
Alifafanua changamoto hiyo katika kesi
hizo amesema inatokea wakati Baba anapotaka kubaki na watoto halafu mama
hataki, mara nyingi mama huwa anataka kubakia na watoto, lakini
baba hataki kutokana na tabia ya mama.
“Hali hii inamfanya Hakimu kutumia sheria
pale ndoa inapotaka kuvunjika, kinachongaliwa zaidi ni
maslahi ya mtoto hata kama mtoto ana umri wa zaidi ya miaka 7,”
anasititiza Mhe. Zunda.
Akitolea mfano wa kesi mojawapo, ambapo
alisema kwamba aliwahi kutoa maamuzi mtoto abaki kwa
baba kwa sababu mama alikuwa na tabia ya ulevi kwa
mujibu wa shuhuda za watoto ili kulinda maslahi na tabia za watoto uamuzi huo.
Ingawa kulingana na sheria ya ndoa ya mwaka 1971
ni jukumu la baba kuwapa watoto matunzo japo
jukumu la kuwalea watoto ni la
wazazi wote. Hata hivyo, mwanamke anatakiwa achangie katika kuhudumia watoto.
Iwapo wazazi wametengana amri ya matunzo hutolewa na Mahakama ili baba
asiyeishi na mtoto.
Matunzo hayo huwa ni
pamoja na kutoa nguo, chakula, kugharamia masomo shuleni na matunzo
yataendelea hadi kufikia umri wa miaka 18.
“Licha ya changamoto tunazozipitia tunajitahidi
kuzitatua kwa kutumia sheria, hakuna rufaa zinazofunguliwa,”alisema Mhe.
Zunda.
Mhe. Zunda alizitaja takwimu
za kesi za ndoa na talaka walizozipokea kwa kipindi cha kuanzia Januari
hadi Machi 23, mwaka huu, kuwa ni 26 na hivyo kati ya hizo 11 bado
zinaendelea kushughulikiwa na nyingine zinaendelea kufanyiwa kazi.
Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo
Mwanjelwa, Mhe. Happiness Chuwa, alisema ili kukabiliana na tatizo la kesi
zinazo husiana na watoto ni vema jamii ijenge tabia ya kuwatambulisha watoto na
kuandika wosia ili kuondoa migongano inapotokea matatizo ya kifamilia.
Kwa mujibu wa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama
ya Watoto ya Kisutu jijini Dar es Salaam, Devotha Kissoka,
akizungumza wakati wa Wiki ya Sheria iliyofanyika mwaka huu kwenye viwanja vya
Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, alisema mtoto akikosa anaweza kupelekwa
katika makao ya watoto.
Ikiwa kuna tatizo, ambalo limeleta mabishano
kuhusu mtoto baba yake au wazazi wake ni akina nani? Mahakama hiyo inatoa
amri Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya vipimo vya utambuzi (DNA).
Takwimu zinaonesha kuwa kesi za madai katika
Mahakama hiyo kwa kipindi cha mwaka 2016 ni 154 ikilinganishwa na
kipindi cha mwaka 2015 ambapo kuliwa kesi 19. Kwa mujibu wa takwimu hizo kesi
hizo zimeongezeka kwa asilimia 78.
Hakimu huyo alifafanua kwamba sababu ya
kuongezeka kwa kesi hizo ni hali ya uchumi, mmomonyoko wa maadili na kupelekea
kuongezeka kwa watoto walio nje ya ndoa.
Aidha, Mahakama hiyo, pia inawajibu wa kusikiliza
kesi za jinai zikiwemo wizi wa kutumia silaha, kujeruhi na
kuua.
Mhe. Kissoka aliongeza kuwa ieleweke
kwa mujibu wa Sheria, mtoto aliyechini ya umri wa miaka kumi hawezi kutenda
kosa la jinai.
Desemba 5, mwaka 2016 Tanzania iliazimisha
Maadhimsho ya Kupiga Vitendo vya Ukatili dhidi ya Watoto, ikiwemo kufanyishwa
kazi ngumu, kubaka na kuolewa wakiwa na umri mdogo, au kutopewa fursa ya kupata
elimu bora kwa ajili ya maisha yao ya baadae.
Mtoto ana haki ya kupata dhamana katika
mashitaka yote isipokuwa yale, ambayo sheria imetamka hayana
dhamana.
Mhe. Kisoka alizitaja adhabu ambazo
hutolewa kwa mtoto, kuwa ni kuachiwa kwa masharti kwa kipindi fulani, kisizidi
miaka mitatu, adhabu ya kulipa faini, adhabu ya kuripoti kwa Afisa
Ustawi wa Jamii, adhabu ya kupelekwa katika shule maalum.
Pamoja na adhabu hizo mahakama ina uwezo wa
kutoa amri mbalimbali kama vile kulipa faini, kuachiwa bila masharti yoyote.
Kutokana na maoni ya watu mbalimbali mfumo
mmoja wa kisheria na nguvu za pamoja zitasaidia kupunguza au kutokomeza
vitendo vya kikatili na unyanyasaji dhidi ya watoto.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni