Mahakama ya Tanzania
inakusudia kuanzisha kituo cha Mafunzo kwa ajili ya watumishi wake pamoja na
wadau ili kuwaongezea ujuzi utakaosaidia kuboresha huduma zinazotolewa na
Mahakama.
Kituo hicho kinachojengwa
katika eneo la Mahakama ya Kisutu jijini Dar es salaam kitawaunganisha
watumishi wa Mahakama na wadau katika mafunzo kwa njia ya video (video
conferencing).
Akizungumzia Kituo
hicho, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma alisema ujenzi
wa kituo hicho ni sehemu ya Maboresho ya huduma za Mahakama ambacho pia wadau wa
Mahakama watakuwa ni sehemu ya mafunzo yatakayokuwa yakitolewa.
Alisema badala ya
Majaji, Mahakimu, watumishi na wadau wa Mahakama kwenda kupata baadhi ya mafunzo
kwenye chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto (IJA), baadhi ya mafunzo watakuwa
wakiyapata katika kituo hicho.
Naye Mratibu wa Mpango
Mkakati wa Mahakama pamoja na maboresho ya Huduma za Mahakama Mhe. Zahara
Maruma alisema ujenzi wa kituo hicho ni utekelezaji wa nguzo ya tatu ya mpango
Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania ambapo kupitia nguzo ya pili ya
Mpango huo, Majaji na Mahakimu hupatiwa mafunzo mbalimbali ili kurahisisha
upatikanaji wa haki kwa wakati.
Akizungumzia nguzo ya
tatu ya Mpango huo, Mhe. Maruma alisema nguzo hiyo inahusiana na urejeshaji wa imani
ya wananchi kwa Mahakama na ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za Mahakama
ambapo kupitia kituo hicho wadau wa Mahakama watahusishwa kwenye Mafunzo
mbalimbali ili kurahisisha suala la upatikanaji wa Haki.
Kuhusu suala la
matumizi ya Teknolojia ndani ya Mahakama, Mratibu huyo alisema hivi sasa
Mahakama inao mpango wa kujenga vituo vya aina hiyo kwenye maeneo mbalimbali
nchini kwa lengo la kuunganisha Mahakama zote nchini kwa njia ya video (video
conferencing).
Ujenzi wa kituo cha
Mafunzo cha Mahakama ulioanza hivi karibuni kwa ushirikiano kati ya Mahakama ya
Tanzania na Benki ya Dunia unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi za
kitanzania milioni 78. Aidha, Jengo la kituo hicho cha mafunzo linajengwa kwa kutumia
teknolojia ya gharama nafuu iitwayo Moladi na linatarajiwa kukamilika ndani ya wiki
nane.
Kaimu Jaji Mkuu wa
Tanzania Mhe Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwasili katika Mahakama ya Kisutu kukagua ujenzi wa kituo cha Mafunzo cha Mahakama ya Tanzania kinachojengwa jijini Dar es salaam. Kulia ni Mwakilishi wa Benki ya Dunia
Nchini, Bella Bird na kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanznaia Mhe. Ferdinand Wambali.
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Prof. Ibrahim Hamis Juma akisaini kitabu baada ya kuwasili katika Mahakama ya Kisutu kukagua ujenzi wa kituo cha Mafunzo cha Mahakama ya Tanzania kinachojengwa jijini Dar es salaam. Kulia ni Mwakilishi wa Benki ya Dunia Nchini, Bella Bird.
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Mwakilishi wa Benki ya Dunia Nchini, Bella Bird. Wa kwanza Kushoto ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Katarina Revokati akifuatiwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Hussein Katanga na wa mwisho ni Mtaalamu kutoka Benki ya Dunia, Waleed Malik
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa na Mwakilishi wa Benki ya Dunia Nchini, Bella Bird.
Mhandisi wa Mahakama ya Tanzania, Khamadu Kitunzi akielezea kuhusu Teknolojia inayotumika kujenga jengo la Kituo cha Mafunzo.
Mtaalamu kutoka Benki ya Dunia, Waleed Malik akizungumza jambo na Wahandisi wanaosimamia ujenzi wa kituo cha Mahakama
Picha ya pamoja
Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini, Bella Bird, Mtaalamu kutoka Benki ya Dunia, Waleed Malik na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. katarina Revokati wakizungumza jambo wakati walipotembelea ujenzi wa kituo cha mafunzo cha Mahakama.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Hussein Kattanmga akimwelezea jambo Mtaalamu kutoka Benki ya Dunia, Waleed Malik walipotembelea ujenzi wa kituo cha Mafunzo cha Mahakama. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni