Na
Lydia Churi- Mahakama, Arusha
Mahakama Kuu Kanda ya
Arusha imefanikiwa kusikiliza na kumaliza kwa zaidi ya asilimia tisini mashauri
yaliyofunguliwa katika kipindi cha mwezi Januari hadi Agosti mwaka huu.
Kwa mujibu wa takwimu
zilizotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu kanda ya Arusha Mhe. Angelo
Rumisha, jumla ya mashauri 737 kati ya 805 yaliyosajiliwa kuanzia mwezi Januari
hadi Agosti 2017, yamemalizika.
Alisema haya ni
mafanikio ya kuridhisha kwa Mahakama Kuu kanda ya Arusha ambapo kila Mhe. Jaji
amesikiliza na kumaliza wastani wa mashauri 245. Hivi sasa, Mahakama Kuu kanda
ya Arusha ina jumla ya majaji watatu.
Katika kuhakikisha
inaondokana na mlundikano wa mashauri kwenye Mahakama mbalimbali nchini,
Mahakama ya Tanzania ilipanga idadi ya mashauri yatakayosikilizwa na Majaji na
Mahakimu. Kwa mujibu wa mpango huo, kila Jaji anatakiwa kumaliza mashauri
yasiyopungua 220 kwa mwaka na hakimu Mashauri 250.
Akifafanua takwimu za
mashauri, Naibu Msajili alisema hadi kufikia Agosti 31, mwaka huu, Mahakama
hiyo imebakiwa na mashauri 809 ambapo kati
ya mashauri hayo, 788 yana umri wa kati ya miaka 1-2, mashauri 17 yana umri
kati ya miaka 3-5, mashauri 2 yana umri kati ya miaka 5-10 na mashauri mengine 2
yana umri wa zaidi ya miaka 10.
Alisema mashauri yote
yenye miaka 10 na zaidi ni yale yaliyorudishwa kutoka Mahakama ya Rufani baada
ya kikao cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kilichofanyika April
mwaka huu.
Akizungumzia Mahakama
za Hakimu Mkazi na za Wilaya kwa Mikoa ya Arusha na Manyara, Mhe. Rumisha
alisema jumla ya mashauri 223 yana umri zaidi ya miezi 12, kati ya mashauri hayo,
ni mashauri mawili tu ndiyo ambayo Mahakama zina mamlaka nayo ikiwa ni sawa na
asilimia 1.3 ya mashauri yote yenye umri zaidi ya miezi 12 hivyo mashauri mengi
ya mlundikano ni yale ambayo Mahakama hazina mamlaka nayo.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu kanda ya Arusha Mhe. Sekela Moshi
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu kanda ya Arusha Mhe. Angelo Rumisha
Wakati
huo huo, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Arusha
Mhe. Sekela Moshi amesema hivi sasa kanda yake imeanza kutekeleza Mikakati
iliyojipangia ya kuondoa mashauri yote yenye muda mrefu Mahakamani.
Akiitaja mikakati hiyo,
Kaimu Jaji Mfawidhi alisema tangu Oktoba 2 mwaka huu, kanda ya Arusha imekuwa
ikifanya vikao vya kumaliza mashauri ya zamani ya madai ambapo mpango huo unatarajiwa
kukamilika Oktoba 13, 2017.
Alisema baada ya
kukamilika kwa mkakati huo, kanda yake itaanza mkakati mwingine uliopangwa na Mahakama
ya Tanzania wa kumaliza mashauri ya zamani chini ya mradi wa Benki ya Dunia
unaotarajiwa kuanza Oktoba 16 na 17 mwaka huu.
Alisema kanda ya Arusha
ina mashauri ya zamani machache hivyo wanatarajia ifikapo Novemba 14, 2017 mashauri yote ya muda mrefu yatakuwa
yamemalizika.
Wananchi wakiwa Mahakama Kuu kanda ya Arusha kwa ajili ya kupatiwa huduma za kimahakama. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni