Alhamisi, 26 Oktoba 2017

MAHAKAMA KUU KANDA YA DODOMA KUMALIZA MASHAURI YA ZAMANI IFIKAPO DESEMBA MWAKA HUU


Na Nurdin Ndimbe  -Mahakama Dodoma
Mahakama Kuu kanda ya Dodoma ambayo inajumuisha Mikoa ya Dodoma na Singida imedhamiria kumaliza kusikiliza mashauri yote ambayo ni mlundikano Mahakamani kufikia mwishoni mwa Desemba mwaka huu.
Akitoa takwimu za umalizaji wa  Mashauri kwa Kanda ya Dodoma, Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma Mhe. Messeka John Chaba alisema kuwa, kufikia Septemba 30, Mwaka huu katika Kanda ya Dodoma kulikuwa na mashauri 109 ya madai, jinai 407 na ardhi mashauri 300.
“Hata hivyo, mashauri yenye umri wa kati ya siku moja  mpaka miaka miwili, madai yalikuwa 100, jinai 400 na ardhi 289. Kwa ujumla mashauri yenye hadhi ya kuwa mlundikano (backlog) sio mengi kwani mpaka kufikia tarehe 23.10.2017 kulikuwa na shauri moja (1) lenye umri kuanzia miaka mitano na kuendelea (5+) na mashauri yenye umri wa 3-4 yalikuwa 25 tu,” alisema Mhe. Chaba.
Waheshimiwa Majaji Kanda ya Dodoma wamekubaliana kwa pamoja kuwa, kwa mujibu wa kalenda zao wataendelea kushughulikia mashauri hayo ya zamani bila kupanga programu maalumu ya  kumaliza mashauri hayo mpaka kufikia mwisho wa mwaka huu.
Kuhusu hali ya mashauri yenye muda mrefu Mahakamani kwa Kanda ya Dodoma, Mhe. Chaba alisema kuwa kwa sasa sio mengi kwa kuwa mpaka kufikia tarehe 23.10.2017 kuna shauri moja (1) tu la madai (ardhi) lenye umri wa miaka 5 (5+) na hakuna shauri lenye umri wa miaka kumi au zaidi (10+).   
Kwa  ujumla,   kwa upande wa  Mahakama za chini; Mahakama za Hakimu Mkazi, Wilaya na Mahakama za Mwanzo mpaka kufikia tarehe 15 Desemba Mwaka huu hakuna Mahakama itakayokuwa na mashauri ambayo ni mlundikano yaani mashauri yenye umri wa zaidi ya miezi 12 kwa Mahakama za Hakimu Mkazi na na miezi 6 kwa Mahakama za Mwanzo Wilaya ambayo wana mamlaka ya kusikiliza.
“Isipokuwa kwa mashauri ya mauaji na uhujumu uchumi ambayo Mahakama hizo hazina mamalaka ya kusikiliza moja kwa moja’’  alieleza Mhe. Chaba na kuongeza kuwa “Kwa sasa hatuna mpango wa kuwa na program maalum ya kumaliza mashauri hususani kwa mashauri ya madai (Civil and Land Cases) kwa ngazi ya Mahakama Kuu na Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya, tunachofanya ni kuendelea kusikiliza kesi zote ambazo ni mlundikano sambamba na mashauri mengine kufikia muda huo kwa mujibu wa kalenda ya kila Jaji au Hakimu” alisistiza.
Aidha, mkakati tulionao wa kusikiliza mashauri ya kesi za mauaji utaendelea kwa kutumia fedha za matumizi ya kawaida.
Mafanikio haya yametokana na ukweli kuwa kwa sasa tunashirikiana kwa karibu sana na wadau wetu na kwamba kumekuwa na mwamko wa wadau hao kufika Mahakamani kwa ajili ya kusikiliza mashauri yao ikilinganishwa na kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Aidha, vikao vya kusukuma mashauri ya jinai pamoja na madai (Case Flow Management Committee and Bench Bar Meeting) ni moja ya nguzo zinazosaidia kukumbushana kila upande kuchukua hatua zinazostahiki kumaliza mashauri kwa wakati. Na kwa kiasi kikubwa kutokana na kasi ya usikilizaji wa mashauri kwa Wahe. Majaji kwa sasa mashauri mengi yanasikilizwa na kumalizika kwa muda uliopangwa. Utaratibu wa usikilizwaji wa mashauri wa “first in, first out” umesaidia sana kufikia malengo.
 Kuhusu usikilizwaji wa Mashauri ya mirathi kwa Kanda ya Dodoma kumekuwa na mafanikio makubwa kutokana na wananchi wengi kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kufungua mashauri hayo na Mahakimu wanaosikiliza mashauri hayo kuharakisha kuyashughulikia mashauri hayo kwa mujibu wa sheria,
Mfano, katika Mahakama ya Mwanzo Makole (W) Dodoma kulikuwa na mashauri ya Mirathi 72 yaliyofunguliwa tangu Januari Mwaka huu lakini hadi kufikia tarehe 23 Oktoba, 2017 mashauri yote ya Mirathi yalikuwa yamesikilizwa na kutolewa uamuzi. Aidha, kwa upande wa  Mahakama ya Mwanzo Chamwino Mjini (W) Dodoma jumla ya mashauri ya Mirathi 78 yaliyofunguliwa tangu Januari mwaka huu lakini mpaka kufikia tarehe 23 Oktoba, 2017 mashauri 71 yalisikilizwa na kutolewa uamuzi na kubaki mashauri 7 tu. 
Kwa upande wa mashauri ya ardhi hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko  la  mashauri hayo Mahakamani kutokana na migogoro ya ardhi kuongezeka baada ya Serikali kufanya uamuzi wa kuhamishia Makao Makuu Dodoma.

Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma bado kuna changamoto mbalimbali zinazojitokeza kwenye uendeshaji wa mashauri katika Mahakama za chini ikiwemo suala la uhaba wa fedha kwa ajili ya kuwalipa wazee wa baraza, kuchelewa kukamilika kwa wakati upelelezi wa makosa ya jinai pamoja na mashahidi muhimu kutopatikana kwa wakati.

Hata hivyo, kuhusu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama na kasi ya uendeshaji wa mashauri katika Kanda ya Dodoma, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma Mhe. Mwanaisha A. Kwariko amesema kwa ujumla hali ya usikilizwaji wa mashauri katika Kanda yetu sio mbaya kama takwimu ulizopewa na Mhe. Naibu Msajili Mfawidhi zinavyoonyesha. ‘’ Nafikiri lengo liko palepale kumaliza mashauri hayo mpaka mwisho wa Mwaka huu. 

“Hata hivyo, tuna mashauri ya mauaji ambayo ni ya  tangu mwaka 2013 kwa hiyo kama kupanga program maalum ya kuondosha mashauri ya zamani itakuwa ni kwa ajili ya kesi hizo za mauaji tu” alisema Jaji Kwariko. 
Kwa ujumla, kama Kanda mpango mkakati unatekelezwa vizuri na umeleta matokeo makubwa. 

“Kwa sasa kwa kanda yetu ya Dodoma umalizwaji wa mashauri kwa kila Mhe. Jaji unaenda vizuri, tunashughulikia malalamiko kwa wakati na upatikanaji wa nakala za hukumu kwa wastani tuko kati ya siku 7 mpaka 21 baada ya kesi kumalizika kwa ngazi ya Mahakama Kuu. Kwetu sisi hayo ni mafanikio makubwa’’ alisistiza. Na kwa Mahakama za chini utaratibu wa utoaji wa nakala za hukumu ndani ya siku 21 unazingatiwa pia.


Mhe.Mwanaisha Kwariko Jaji Mfawidhi kanda ya Dodoma.

Pichani ni Mhe. Messeka John Chaba, Naibu Msajili- Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma.


Bango la Mahakama likiwa limebandikwa sehemu wanaposubiri wateja kupata huduma, Lengo la Mabango hay kwa ajili ya wananchi kutoa malalamiko yao dhidi ya vitendo vya Rushwa, Maadili pamoja na Mpango Mkakati wa Mahakama.Katika bango hili kuna namba za simu za taasisi mbalimbali zinahusu mapigano dhidi ya  maadili na rushwa kwa  watumishi wa Mahakama ya Tanzania.

Jengo jipya la Utawala na Fedha likiwa katika hatua za Mwisho kukamilika katika Mahakama Kuu kanda ya Dodoma.
( picha na Nurdin Ndimbe)
 


 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni