Na
Lydia Churi- Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Mawakili nchini kutokuwa sehemu ya rushwa
na badala yake waisaidie Mahakama ya Tanzania katika kupambana na rushwa kwa kufanya
kazi kwa bidii na kuzingatia Maadili ya taaluma hiyo.
Akizungumza wakati wa sherehe
za 57 za kuwakubali na kuwaapisha Mawakili wapya zilizofanyika leo katika viwanja
vya Karimjee jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu amewataka Mawakili kutokutumia vifungu
vya sheria na kanuni ili kuchelewesha upatikanaji wa haki kwa kuwa suala la
upatikanaji wa haki hutegemea Mawakili.
“Katika karne hii ya 21
ni muhimu kwa Mawakili kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa huduma za karne hii huvuka
mipaka ya nchi”, alisema Jaji Mkuu.
Prof. Juma pia amewashauri
Mawakili kusoma na kuzifahamu sheria za kimataifa ili wawe na upeo mkubwa katika
kushughulikia kesi hasa zile zinazohusisha nchi zaidi ya moja. Baadhi ya kesi hizo
ni zile zinazohusu mipaka ya nchi, makosa ya kimtandao (cyber Crimes) pamoja na
zile zinazohusu Maliasili.
Aidha, Mhe. Jaji Mkuu aliyataka
baadhi ya makosa ambayo yamekuwa yakifanywa na baadhi ya Mawakili na wananchi kuwashitaki
kuwa ni kutoa siri za wateja, kughushi nyaraka, kutayarisha mikataba zaidi ya moja
kwa lengo la kudanganya, Wakili kuchukua kesi bila ya ruhusa ya mteja, kuwaibia wateja kwa kuwatoza fedha nyingi, kuwadanganya,
kuchukua kesi yenye maslahi binafsi pamoja na uzembe.
Prof. Juma pia amewashauri
Mawakili wapya kuhakikisha wanashirikiana na taaluma nyingine wanapofanya kazi zao
ilikurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa haki kwa wateja wao.
Naye Mwanasheria Mkuu wa
Serikali Mhe. George Masaju amewataka Mawakili wapya kutosubiria kuajiriwa na Serikali
na badala yake wajiajiri na kutoa huduma mikoani na siyo Dar es Salaam peke yake.
Naye Makamu wa Rais wa
Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Godwin Ngwilimi amewataka Mawakili
nchini kutekeleza wajibu wao kwa kufuata misingi ya haki na kujiepusha na vitendo
vya rushwa.
Jumla ya Mawakili wapya
296 wamekubaliwa na kuapishwa leo na kufanya idadi ya Mawakili nchini kufikia
6,536. Aidha, sherehe za kuapishwa na kukubaliwa kwa Mawakili zimefanyika kwa mara ya 57 tangu kuanzishwa
kwa utaratibu huo mwaka 1986.
Pichani ni sehemu ya
baadhi ya Mawakili wapya walioapishwa na Mhe. Jaji Mkuu mapema Desemba 15
katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, kufuatia idadi hiyo ya
Mawakili wapya inaongeza na kuwa na jumla ya Mawakili 6,536 nchini.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Juma (kushoto) akiwaapisha mawakili wapya, kulia kwake ni
Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali.
Pichani ni Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma akitoa hotuba yake katika Sherehe za
Kuwakubali Mawakili Wapya, katika hotuba yake Mhe. Jaji Mkuu amewataka Mawakili
hao wapya kutekeleza Majukumu yao kwa mujibu wa sheria na kufuata maadili ya
kazi, vilevile amewaasa kutojihusisha na rushwa kwa maana ni adui mkubwa wa
haki.
Baadhi ya Mawakili
wakitoa heshima mbele ya Mhe. Jaji Mkuu na Majaji wengine waliopo meza kuu mara
baada Mhe. Jaji Mkuu kutamka rasmi kwa mujibu sheria kuwa Mawakili rasmi.
Pichani ni Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Mhe. George Masaju akitoa hotuba yake, katika hotuba yake,
Mhe. Masaji amewataka Mawakili hao kwenda kufanya kazi ya kuwatetea wananchi katika
mikoa mbalimbali nchini na siyo lazima wote kukaa Dar es Salaam.
Baadhi ya Viongozi wa
Mahakama na Wageni waalikwa walioshiriki katika hafla hiyo, mwenye suti nyeusi
ni Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati.
Msajili-Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Ilvin Mugeta akitoa maelekezo mbalimbali katika Sherehe hizo za
Kuwaapisha na Kuwakubali Mawakili wapya iliyofanyika Desemba 15, 2017 katika
Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (kulia) akiongea jambo na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP)
walipokuwa katika hafla hiyo.
Pichani ni Baadhi ya
Majaji walioshiriki katika hafla hiyo.
Makamu wa Rais wa Chama
cha Mawakili Tanganyika (TLS), Mhe. Wakili Godwin Ngwilimi akitoa hotuba katika
hafla hiyo.
Picha ya pamoja: Meza
kuu pamoja na baadhi ya Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani (T) na
Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mawakili
wapya.
(Picha na Mary Gwera)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni