Jumatano, 31 Januari 2018

HOTUBA YA MHE. JAJI MKUU PROF. IBRAHIM HAMIS JUMA SIKU YA UFUNGUZI WA MAADHIMISHO YA WIKI YA SHERIA TAREHE 28 JANUARI, 2018

 HOTUBA YA MHE. JAJI MKUU PROF. IBRAHIM HAMIS JUMA SIKU YA UFUNGUZI WA MAADHIMISHO YA WIKI YA SHERIA TAREHE 28 JANUARI, 2018

Mhe. Mgeni Rasmi,
Wahe, Majaji wa Mahakama Rufaa,
Mhe. Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,
Ndugu Watumishi wa Mahakama ya Tanzania,
Ndugu Wadau wote wa wote wa Mahakama,
Ndugu Waandishi wa Habari,
Ndugu wananchi,
Mabibi na Mabwana,

Mhe, Mgeni Rasmi, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema na kutuvusha salama hata tukaweza kuuona mwaka mpya nawatakieni nyote HERI YA MWAKA MPYA WA 2018. Pia napenda kuchukua fursa hii kukukaribisha hapa katika viwanja vya Mnazi Mmoja katika siku hii ya leo ambapo tunafungua rasmi maadhimisho ya wiki ya sheria na kilele cha siku ya sheria nchini. 2

Mhe. Mgeni Rasmi, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo hufanya maadhimisho ya siku ya Sheria, baadhi ya nchi nikitaja chache ni;- Marekani wao siku ya sheria ilianzishwa mwaka 1957 ambapo huadhimishwa kila tarehe 1 Mei. India siku ya sheria ilianzishwa mwaka 1979 na huadhimishwa kila tarehe 26 Novemba, Nepal huadhimishwa kila tarehe 9 Mei, Uingereza ilianzishwa 1958, Singapore na nyingine nyingi.

Mhe, Mgeni Rasmi, Mahakama ya Tanzania ilianzisha rasmi kuadhimisha siku ya sheria mwaka 1996. Katika kipindi hicho chote tulikuwa tukiadhimisha siku ya sheria katika siku ile maalum tu. Kutokana na umuhimu wa siku ya sheria maboresho yameendelea kufanyika. Kuanzia mwaka 2015 siku ya sheria imekuwa ikitanguliwa na wiki ya sheria. Katika wiki hiyo Mahakama na Wadau mbalimbali kama Tume ya Utumishi wa Mahakama, ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA), Taasisi ya Uanasheria kwa vitendo 3

Tanzania (Law School of Tanzania), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Taasisi zinazotoa msaada wa Kisheria (Legal Aid), Magereza, Polisi, Takukuru na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) hutoa elimu na huduma za kisheria kwa wananchi bila malipo. Huduma zinazotolewa hazina tofauti na zile ambazo huzipata wanapotembele ofisi husika. 

Mhe, Mgeni Rasmi, maadhimisho ya wiki ya sheria na kilele cha siku ya sheria nchini katika nchi yetu huashiria mwaka mpya wa Kimahakama ambao huwa ni mwanzo wa shughuli za kimahakama katika mwaka husika. Kwa mwaka huu wa 2018 wiki ya sheria inaanza leo, kilele cha Wiki ya Sheria kitakuwa siku ya sheria tarehe 1 Februari, 2018. Baada ya kutuongoza katika matembezi utatufungulia maonesho yatakayoanza hivi punde katika viwanja hivi vya Mnazi Mmoja. Maonesho hayo yanalenga kuonyesha maboresho yanayofanywa na mahakama katika mfumo mzima wa utoaji haki, na namna ambavyo matumizi ya TEHAMA yanavyorahisisha utoaji haki katika 4

mahakama. Maonesho haya pia yataongeza ufahamu wa wananchi kuhusu taratibu za ufunguaji wa mashauri katika ngazi zote za Mahakama, upatikanaji wa msaada wa kisheria, upokeaji wa malalamiko na namna yanavyoshughulikiwa na kadhalika. Aidha, maonesho haya yataonyesha mifumo ya TEHAMA ambayo tayari imeanza au ile ambayo inatarajia kuanza katika mfumo wa utoaji haki. 

Mhe. Mgeni Rasmi, imekuwa ni utamaduni wa dunia (World Convention) kwa Taasisi mbalimbali kufanya matembezi ya hiari kama haya. Mahakama ya Tanzania pia imekuwa ikidumisha utamaduni huu kwa kufanya matembezi haya kila mwaka tunapoadhimisha wiki ya sheria na mwanzo wa mwaka kimahakama, matembezi haya ni muhimu kwetu kwani yanaimarisha afya zetu na kutuweka katika hali nzuri zaidi ya kutekeleza majukumu yetu. Kwani wote tunatambua kuwa taifa imara hujengwa na wananchi imara, wenye afya njema. 5

Matembezi haya pia yanaashiria mshikamano uliopo kati ya mahakama wa wadau wote wanaohusika kwa namna moja au nyingine katika mfumo mzima wa utoaji haki na wananchi kwa ujumla.
Mhe. Mgeni Rasmi, maudhui ya maadhimisho ya wiki ya sheria na siku ya sheria nchini kwa mwaka huu ni:-
“Matumizi ya TEHAMA katika utoaji Haki kwa wakati na kwa kuzingatia maadili”
Mhe. Mgeni Rasmi, maonesho haya yatafungwa tarehe 31 Januari, 2018 alasiri, na kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria nchini yatafanyika tarehe 1 Februari, 2018 katika viwanja vya Mahakama hapa Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi atakuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 6

Mhe. Mgeni, Rasmi, nitumie fursa hii adimu kuwakaribisha wananchi na wadau wengine wote wa mahakama kushiriki katika maadhimisho haya ya wiki ya Sheria na siku ya sheria nchini kwa kutembelea maonesho ili waweze kujipatia elimu ya masuala mbalimbali ya utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania, ni nafasi pia ya kujipatia huduma, msaada wa kisheria na kutoa maoni na mapendekezo yao yenye lengo la kuboresha utoaji haki nchini.
Kwa mara nyingine tena nitumie nafasi hii kutoa shukrani za dhati kwako wewe Mheshimiwa Mgeni rasmi kwa kukubali mwaliko huu wa kuongoza matembezi na kufungua rasmi maonesho ya wiki ya sheria. Nakushukuru sana .
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni