Serikali
yatimiza azma yake ya kuanzisha Mahakama ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi
Na
Lydia Churi- Mahakama ya Tanzania
Moja
ya ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
katika kampeni za uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ni kuanzishwa Mahakama
itakayokuwa ikishughulika na kesi za ufisadi ikiwa ni mkakati wake wa kupambana na ufisadi pamoja
na matumizi mabaya ya fedha za Umma. Ikiwa ni miaka miwili (2) sasa tangu kuingia
kwake madarakani, tumeshuhudia Mahakama hiyo inayoshughulika na Makosa ya
Rushwa na Uhujumu Uchumi ikianzishwa Julai 7, 2016, ikiwa ni Divisheni ya
Mahakama Kuu ya Tanzania.
Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria ya Marekekebisho
mbalimbali ambayo pamoja na mambo mengine inampa Jaji Mkuu Mamlaka ya kuanzisha
Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ya Mahakama kuu ya Tanzania.
Akiwasilisha Muswada wa Sheria hiyo Bungeni mjini Dodoma, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali Mhe. George Masaju alisema, “ Divisheni Maalum ya Mahakama kuu itakuwa
na Majaji na Watumishi wengine ambao wanahusika moja kwa moja na uendeshaji wa kesi
za Rushwa na Uhujumu Uchumi, Hatua hii itawezesha kesi hizi kusikilizwa kwa
urahisi na kwa haraka”, alisema Mhe. Masaju.
Kuanzishwa
kwa Divisheni hii kunaifanya Mahakama kuu ya Tanzania kuwa na jumla ya Divisheni nne sasa. Divisheni
nyingine za Mahakama kuu ya Tanzania ni ile ya Biashara iliyoanzishwa mwaka
1999 ilifuatiwa na ya Ardhi mwaka 2001, na mwaka 2007 ilianzishwa Divisheni ya
Kazi.
Sheria zilizoanzisha Divisheni ya Makosa
ya Rushwa na Uhujumu Uchumi
Divisheni
ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ilianzishwa kufuatia mabadiliko ya Sheria
ya Uhujumu uchumi, sura namba 200 ya sheria za Tanzania yaliyofanyika kupitia
sheria namba 3 ya mwaka 2016. Kifungu namba tatu (3) cha Sheria ya Uhujumu
Uchumi, kama ilivyofanyiwa marekebisho kupitia sheria namba 3 ya mwaka 2016
kinaanzisha Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi katika ngazi ya
Mahakama Kuu.
Sehemu
ya Jengo la Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ya Mahakama Kuu ya Tanzania lililopo Sinza jijini Dar es salaam.
Usajili wa Kesi katika Divisheni ya
Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi
Utaratibu
wa kusajili kesi katika Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ya
Mahakama Kuu ya Tanzania unafanyika kwa hatua mbili. Usajili wa mashauri katika
hatua ya kwanza ufanyika katika Mahakama zote za Hakimu Mkazi/Wilaya hapa
nchini. Hatua hii inalenga kutoa nafasi kwa upande wa Jamhuri kukamilisha
upelelezi na taratibu zote za awali za
kesi za rushwa na uhujumu uchumi. Katika hatua ya kwanza, iwapo shtaka
linalomkabiri mshtakiwa linahusisha
kiasi cha fedha kinachozidi shilingi za
Kitanzania milioni kumi, mshtakiwa
atapaswa kuwasilisha maombi yake ya dhamana kwenye Masjala za Divisheni ambazo zinapatikana kwenye kila
jengo la kanda ya Mahakama kuu, ispokuwa Dar es salaam ambapo Divisheni ina
jengo lake maalumu. Maombi ya dhamana katika hatua ya kwanza yanafanyika
Mahakama kuu kwa kuwa Mahakama za Hakimu Mkazi/Wilaya hazina mamlaka ya
kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ispokuwa kwa kibali maalumu kutoka kwa
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini.
Hatua
ya pili ya usajili wa kesi unafanyika katika masjala zote za Divisheni ya
Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ya Mahakama kuu baada ya Mkrugenzi wa
Mashtaka nchini kuwasilisha taarifa ya Mashtaka. Hatua hii ufuatia kukamilika
kwa upelelezi na taratibu zingine za awali katika hatua ya kwanza. Baada ya
kuwasilishwa kwa taarifa ya mashtaka usajili wa kesi ufanyika na taratibu za
kusikiliza kesi husika huanza mara moja.
Kwa
mujibu wa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya
Rushwa na Uhujumu Uchumi Mhe. Charles Magesa, kati ya mwaka 2016 na 2017, mpaka
kufikia Novemba 30, 2017 jumla ya mashauri 117 yaliyosajiliwa kwa ajili ya
maombi ya dhamana yamesikilizwa na kutolewa uamuzi katika masjala mbalimbali za
Divisheni nchini. Alisema kati ya hayo yaliyotolewa uamuzi ni mashauri 39 ya kanda ya Dar es salaam, Dodoma
15, Iringa 8, Mbeya 10, Mtwara 14, Songea 19, Shinyanga 3 na Tabora 1.
Mhe.
Magesa alisema jumla ya mashauri 14 ya maombi ya dhamana yako katika hatua
mbalimbali za usikilizwaji ambapo masjala ya Dar es salaam ina mashauri11,
Songea 2 na Dodoma 1 ambayo yanaendelea kusikilizwa kwenye Mahakama hiyo.
Akizungumzia
mashauri yaliyokamilika upelelezi wake, Naibu Msajili huyo alisema Mkurugenzi
wa Mashtaka nchini tayari amekamilisha na kuwasilisha taarifa za mashtaka za kesi
tatu (3) katika masjala ya Divisheni ya Dar es salaam. Taratibu za kusikiliza
hoja za awali za kesi hizo zitafanyika na kukamilika kabla ya Desemba 15, 2017
na usikilizaji wa mashauri hayo utafanyika mwanzoni mwa mwezi Februari, 2018.
Mamlaka ya Mahakama katika
kusikiliza kesi za Rushwa na Uhujumu Uchumi
Mahakama
hii imepewa Mamlaka ya kusikiliza
mashauri ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, aidha Divisheni hii ina mamlaka
ya kusikiliza mashauri ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ambayo thamani yake
au kiwango cha fedha ni kuanzia shilingi za kitanzania bilioni moja na
kuendelea. Aidha, Divisheni ina mamlaka pia ya kusikiliza makosa yote
yaliyo orodheshwa katika jedwali la sheria ya uhujumu uchumi yanayoangukia katika vifungu vya sheria mbalimbali zilizopo kwenye jedwali
sheria ya uhujumu Uchumi bila kujali thamani au kiwango cha fedha. Baadhi ya
sheria hizo ni pamoja na Sheria ya kuzuia utakatishaji fedha, sheria ya
udhibiti wa madawa ya kulevya, Sheria ya kuzuia ugaidi na sheria ya uhifadhi wa
wanyamapori.
Sheria
nyingine ni ile ya Uvuvi wa bahari kuu, sheria ya madini, sheria ya silaha na
milipuko, sheria ya udhibiti wa silaha, sheria ya misitu na sheria ya petrol.
Sheria nyingine ni ya Mafuta na gesi, sheria ya makosa ya mtandao na sheria ya
miamala ya kielektroniki.
Divisheni
hii ya Mahakama kuu ambayo ni maalum kwa Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi pia
inaendeshwa kwa mujibu wa kanuni zilizotolewa la Serikali Namba 267 la tarehe
9/9/2016. Kanuni hizo pamoja na mambo mengine zinaelekeza mambo mbalimbali kama
vile taratibu za ufunguaji mashauri, uendeshaji wa mashauri.
Kwa
mijibu wa kanuni hizo,ukomo wa muda wa kusikiliza mashauri katika Divisheni ni
kipindi kisichozidi miezi tisa (9) tangu kuwasilishwa kwa taarifa ya mashtaka.
Aidha, ukomo wa muda wa kusikiliza mashauri unaweza kuongezwa kwa kipindi
kisichozidi miezi sita endapo kutakuwa na sababu maalum zitakazopelekea shauri
kushindwa kumalizika ndani ya kipindi cha miezi tisa (9).
Mipaka ya kuisajili kesi za Rushwa
na Uhujumu Uchumi nchini
Divisheni
hii inayo masjala kumi na nne ambapo mashauri yanaweza kusajiliwa katika
masjala yoyote nchini. Masjala hizi ziko katika kanda 14 za Mahakama Kuu ya
Tanzania zilizoko kwenye miji ya Tanga, Mwanza, Dodoma, Arusha, Moshi,
Sumbawanga, Songea, na Mtwara, Dar es salaam, Tabora, Mbeya, Bukoba, Iringa na
Shinyanga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni