Na
Mary Gwera, Mahakama
Mahakama ya Tanzania
imedhamiria kufanya malipo yote ya huduma zake na ukusanyaji wa mapato kielektroniki
ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya Teknolojia na vilevile kuboresha huduma
kwa manufaa ya wananchi.
Hayo yalisemwa na
Mkurugenzi Msaidizi, Mipango na Bajeti-Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso Januari
16, alipokuwa akifungua mafunzo ya Siku tano ya Mfumo wa Kielektroniki wa
Kukusanya Mapato ya Serikali ‘Government Electronic Gateway (GEPG) yanayofanyika
katika Ukumbi mpya ya Mikutano uliopo katika eneo la Mahakama ya Hakimu
Mkazi-Kisutu jijini Dar es Salaam.
“Mahakama kama ilivyo
kwa Taasisi nyingine za Serikali imejiunga katika Mfumo huu ili kufanya
ukusanyaji wa Mapato na malipo yote ya Huduma za Mahakama kufanywa kwa njia ya
Kieletroniki, kwa hiyo ili kuwezesha matumizi ya mfumo huu yameandaliwa mafunzo
haya maalum kwa Watumiaji katika ngazi mbalimbali za Mahakama kuwapa ujuzi wa
kuwawezesha kufanya kazi hii,” alifafanua Bw. Uisso.
Alitaja kuwa kwa
kuanzia mafunzo hayo ya awamu ya kwanza yameshirikisha jumla ya Watumishi 35 wa
Mahakama kwa Mkoa wa Dar es Salaam, akitaja watumishi hao kuwa ni pamoja na
Wahasibu, Maafisa TEHAMA, Makarani kutoka Makao Makuu na ngazi zote za Mahakama
kwa mkoa huu.
“Tunatarajia kuendelea
kutoa elimu hiyo katika mikoa mingine kwa awamu, ili kuiwezesha Mahakama nchi
nzima kutumia mfumo huu,” aliongeza Bw. Uisso.
Kwa mujibu wa
Mkurugenzi huyo Msaidizi anasema kuwa Mfumo wa sasa unaotumika na Mahakama una
changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na baadhi ya Mahakama kutowasilisha ‘bank
slip’ kwa wakati, fedha kuingizwa kwenye akaunti ambazo sio za Mahakama n.k
Bw. Uisso anaongeza
kuwa Mfumo huu umekuja wakati muafaka kwa Mahakama ambapo kwa sasa ipo katika
maboresho ikiwa ni pamoja na kuwa na mpango wa kuanzisha ‘e-Judiciary’ ili
kuboresha mfumo wa usimamizi wa mashauri na ukusanyaji wa takwimu.
Kwa upande wake Afisa
TEHAMA kutoka Wizara ya Fedha na Mipango-Kitengo cha Usimamizi wa Mifumo ya
Fedha, Bi. Penina Henjewele aliwatoa hofu Washiriki wa Mafunzo hayo kuwa mfumo
huo ni rafiki kutumia hivyo wasiwe na wasiwasi katika utekelezaji.
“Mfumo huu ni rafiki
sana kutumia, vilevile unaokoa muda, hivyo basi msiwe na wasiwasi mtaelewa na
kufanya vizuri cha msingi ni kufuata taratibu na maelekezo yanayokuwa
yakitolewa,” alisema Bi. Henjewele.
Mafunzo hayo ya siku
tano (5) yanaendeshwa na Wawezeshaji kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na Mfumo
huu wa ‘GEPG’ uliandaliwa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango pamoja
na Wadau wengine.
Tayari Mfumo huo
umeshaanza kutumiwa na baadhi ya Taasisi za Serikali kama Wizara ya Ardhi,
Wakala wa Misitu, Jeshi la Polisi-Kitengo cha Usalama Barabarani ‘Traffic’ na
baadhi ya Halmashauri za Serikali za Mitaa.
Mkurugenzi Msaidizi,
Mipango na Bajeti-Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso akiongea jambo na
Washiriki katika Mafunzo hayo.
Baadhi ya Sehemu ya
Wahasibu na Makarani wa Mahakama wakiwa katika Mafunzo hayo.
Washiriki wakifuatilia
mada.
Afisa
TEHAMA kutoka Wizara ya Fedha na Mipango-Kitengo cha Usimamizi wa Mifumo ya
Fedha, Bi. Penina Henjewele akitoa Mada ya Mfumo wa Kielektroniki wa Kukusanya Mapato
ya Serikali ‘Government Electronic Gateway (GEPG) kwa Washiriki wa Mafunzo hayo
(hawapo pichani)
Mada inayotolewa
Baadhi ya sehemu ya Washiriki
wa Mafunzo hayo.
Washiriki wakiwa katika
picha ya pamoja.
(Picha na Mary Gwera)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni