Na
Mary Gwera
WADAU wa Haki Jinai
nchini wameazimia kwa pamoja kukuza ushirikiano baina yao katika kushughulikia
uhalifu wa makosa yanayovuka mipaka kuanzia eneo la Ukusanyaji wa taarifa, Upelelezi,
Uendeshaji wa Mashtaka pamoja na Mashauri ya namna hiyo.
Hayo yalibainishwa
mwishoni mwa wiki iliyopita Februari 02, 2018 na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama
(IJA), Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo katika mahojiano maalum mara baada ya kuhitimishwa
kwa Kongamano la Wadau wa Haki Jinai lililofanyika katika Kituo kipya cha kisasa cha Mafunzo na
Habari za Kimahakama kilichopo eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
“Katika Kongamalo hilo
ambalo lilihusisha Wadau mbalimbali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Mkemia Mkuu wa Serikali, Jeshi la Magereza, Wizara ya Katiba na
Sheria na wengineo tumeazimia pia mamlaka zinazofanya upelelezi ziwe na Maabara
za kufanyia Upelelezi wa Kisayansi ‘Forensic Science’ ili kuharakisha
uendeshaji wa kesi na hatimaye haki iweze kupatikana kwa wakati,” alisema Mkuu
wa Chuo huo ambaye pia alikuwa Mwezeshaji katika Mafunzo hayo.
Mhe. Kihwelo anasema
kuwa kwa sasa wenye Maabara hizo ni Polisi pamoja na TAKUKURU, lakini wengine
wote wanategemea Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, na kuongeza kuwa Tume ya
Kupambana na Madawa ya Kulevya ipo kwenye mchakato wa kuanzisha Maabara yao ya
uchunguzi.
Aidha; Wadau wa
Kongamano hilo waliazimia kwa pamoja kuwa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali
iendelee kutoa majibu kwa wakati ili kuharakakisha haki kupatikana kwa wakati.
Mafunzo hayo ya Siku
tano yalifanyika kwa mara ya kwanza katika Kituo Kipya cha Mafunzo na Habari za
Kimahakama yalijikita katika Mada ya ‘Sheria za Uhalifu wa Makosa yanayovuka
Mipaka’ ambapo katika Mada hii Sheria zilizoangaliwa ni pamoja na
Sheria ya Makosa ya Kimtandao ‘Cybercrime’, Makosa yanayohusu miamala ya fedha
kwa njia ya Kimtandao pamoja na Sheria ya Madawa ya Kulevya na makosa
yanayoundwa na Sheria hiyo.
Kongamano hili lililofunguliwa
rasmi na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma Januari 29, 2018 lililenga
kuwakutanisha Wadau wa Haki Jinai ili kujadili changamoto zilizopo katika
sheria hizokatika maeneo ya upelelezi, uendeshaji mashtaka pamoja na
ubadilishanaji wa Wahalifu na kuwakutanisha kwa lengo la kujenga Mtandao wa
Wadau na kukuza ushirikiano.
Aidha; Mhe. Jaji Dkt.
Kihwelo anaongeza kuwa Mafunzo hayo yaliyomalizika ni miongoni mwa mafunzo
mengi zaidi yatakayofuatia huku yakishirikisha Wadau tofauti tofauti.
Jaji Kiongozi, Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali akifunga
Kongamano
la Wadau wa Haki Jinai lililofanyika katika Kituo cha Mafunzo na Habari
kilichopo eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, katika
maneno yake ya kufunga, Mhe. Jaji Wambali amewataka Wadau kuendeleza
ushirikiano ili kuiwezesha Mahakama kutoa haki kwa wakati.
Mkuu wa Chuo cha
Uongozi wa Mahakama-Lushoto (IJA) (aliyesimama mwenye tai akitoa maelezo mafupi
kwa Mgeni rasmi juu ya Mafunzohayo kabla ya kufunga rasmi Kongamano hilo.
Jaji Kiongozi, Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali akikabidhi cheti cha Ushiriki kwa mmoja
wa Washiriki wa Kongamano hilo, Mhe. Jaji Firmin Nyanda Matogolo.
Mgeni
rasmi, Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali akiwa
katika picha ya pamoja na baadhi ya Wahe. Majaji wa Mahakama Kuu na baadhi ya
Watumishi wa Mahakama walioshiriki katika Kongamano.
Jaji Kiongozi, Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali (katikati) akiwa katika picha ya pamoja
na baadhi ya Washiriki wa Kongamano.
(Picha na Ibrahim Mdachi, IJA)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni