Alhamisi, 31 Mei 2018

HALI DUNI YA UCHUMI YASABABISHA KUONGEZEKA MASHAURI YA MADAI MAHAKAMA YA WATOTO,KISUTU



Na Magreth Kinabo
Imeelezwa  kuwa hali duni ya uchumi  imechangia kuongezeka  kwa idadi ya mashauri ya madai katika Mahakama ya Watoto, Kisutu.  
Akizungumzia kuhusu Mahakama ya Watoto iliyopo katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, Hakimu  Mkazi Mfawidhi , Mhe. Devota Kissoka  alisema  mahakama hiyo inasikiliza kesi za aina mbili  ambazo ni madai na jinai, lakini  mashauri ya madai yamekuwa yakiongezeka.
Akitolea mfano katika kipindi cha mwaka 2015 mashauri ya madai yalikuwa ni 11,  mwaka 2016   yalikuwa ni 159. Mwaka 2017  idadi ya mashauri ya madai yalikuwa ni 292 na mwaka 2018 kuanzia Januari  hadi Mei 30, mwaka huu mashauri yamefikia 109.

Hakimu  Mkazi Mfawidhi , Mhe. Devota Kissoka  wa Mahakama ya Watoto, Kisutu akifafanua jambo kuhusu Mahakama  hiyo.
Miongoni mwa mashauri  hayo ni kuomba matunzo ya mtoto, uhalali wa jina la mtoto, na ruhusa ya kumwona mtoto.
Mhe. Kissoka alishauri kuanzishwa kwa Mahakama ya Familia(Family Court) ili kuweza kurahisisha  huduma  za kimahakama  kwa wateja. Alisema mahakama hiyo ya familia iwe inashughulikia mashauri ya mirathi, ndoa, talaka na watoto kwa kuwa vinaenda pamoja.  
Afisa Ustawi wa Jamii wa Mahakama ya Watoto, Caren   Mitta alisema  hali duni ya uchumi imechangia kuongezeka kwa mashauri ya madai.Mashauri ya madai yameongezeka maofisa ustawi wa jamii na watoa msaada ya kisheria kufanya kazi katika ushirikiano wa kuelimisha jamii  juu ya Sheria ya Mtoto, kuwepo kwa migogoro ya ndoa na kuvunjika kwa ndoa, na ulevi.
Mhe.  Kissoka  anafafanua  kwamba  Mtoto ni mtu mwenye umri  wa chini ya  miaka 18  kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na kanuni zake za mwaka 2016,lakini kuna sheria inasema mtoto chini ya miaka 10 hana jukumu la kijinai.
Aliongeza kwamba kwa upande wa mashauri ya jinai mwaka 2015 yalikuwa ni 63, mwaka 2016  mashauri   120, mwaka 2017 ni mashauri 91 na mwaka 2018  kuanzia Januari hadi Mei 30,mwaka huu yamefikia mashauri 57.  Alisema kesi za jinai zimepungua kutoka na juhudi za elimu  itolewayo na  dawati la polisi na maafisa ustawi wa jamii.
Mhe . Kissoka alisema mashauri  hayo ni yanahusu kesi mbalimbali, ambazo ni kuua , kuvuta bangi ,wizi wa kawaida, wizi wa kutumia silaha, ubakaji na ulawiti.
“Changamoto inayotukabili  ni   wateja wetu kuwa na uelewa mdogo wa sheria hasa kwenye mashauri ya maombi na kutokuwa na uwezo wa kuweka wanasheria wa kuwatetea,”alisema Mhe .Kissoka.
Nyingine  wadawa kutokutekeleza  maamuzi ya mahakama hasa kwenye masuala ya fedha  na maslahi ya mtoto hayafikiwi kutokana  na baba au mama kuwa na  uchumi  mdogo.
Aliongeza kwamba  jengo la mahakama  hiyo ni chakavu  na wakati  wa mvua  linavuja, hivyo linahitaji  kufanyiwa ukarabati, Pia hakuna sehemu ya wateja  kusubiria kesi.
Naye Afisa Usatwi wa Jamii wa Mahakama hiyo, Saada Kingu alisema  kwa upande wa kesi  za jinai zinazoripotiwa kwa nyingi ni ulawiti na ubakaji, ambapo alizitaja sababu kuripotiwa .
“Mzazi au Mlezi amekuwa na kipato duni  muda mrefu wanakuwa katika shughuli zao ,hivyo watoto wanakaosa malezi bora na wajiongoza wenyewe , wazazi au walezi kutotoa elimu ya kujamiana kwa watoto  wao, na kutokuwepo kwa ukaribu baina  wazazi au walezi  na watoto, utandawazi,” alisema Kingu.
Kingu aliongeza kwamba  kuna watu hawaijui sheria ya mtoto na kukwepo kwa uelewa mdogo  wa  huduma za ustawi wa jamii,hivyo inasababisha kupata taarifa za uchunguzi kuwa ngumu.
Hata hivyo alishauri kwamba elimu  kuhusu  sheria ya mtoto itolewe na kuna haja ya kufanyiwa marekebisho kipengele cha adhabu maana ya mtoto itazamwe upya.
Wakizungumzia  kuhusu mahakama hiyo, maafisa hao walisema haiko katika mazingira  rafiki, na kushauri kuwa iwe na eneo lake na pia isichanganywe na vitu vingine.
Akizungumzia kuhusu adhabu zinazotolewa kwa mtoto Mhe .Kissoka   alisema anapatiwa adhabu mbadala mfano vile kifungo cha nje  chini ya uangalizi  wa Afisa Ustawi wa Jamii au kupelekwa Shule ya  Maadili   ya Watoto.
 
 
 




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni