Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim hamis Juma amewataka Naibu Wasajili, Watendaji, Mahakimu pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Mahakama kutenda haki kwa watumishi walio chini yao kwani kimbilio la Mtumishi anapopata matatizo ni kwa kiongozi wake katika sehemu yake ya kazi.
Akifungua Mkutano wa
Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania leo mjini Dodoma, Jaji Mkuu
amesema endapo viongozi hao watajifungia na kutojihusisha na matatizo ya
watumishi walio chini yao ni wazi kuwa morali ya utendaji kazi itashuka, tija
itakosekana na hivyo wananchi watapewa huduma zisizoridhisha hasa katika
kipindi hiki ambapo Mahakama ya Tanzania inaendelea na maboresho ya kisayansi
ya huduma zake.
“Kiongozi sehemu ya
kazi ni yule anayehamasisha na kuelimisha kwa kuonyesha njia mpya, anasikiliza,
anajifunza na anakubali kuwa mfanyakazi anaweza kumfungus macho,” alisema Jaji
Mkuu.
Aidha, Jaji Mkuu pia
amewataka Viongozi hao kuacha tabia ya ubwana bali watekeleze wajibu wao kwa
kuwaongoza watumishi walio chini yao kwa ustaarabu na uadilifu.
Alisema Mahakama ya
Tanzania imeamua kufanya kazi kisayansi na kwa malengo na misingi inayokubalika
kwa vitendo na kwa mujibu wa Sheria na itatekeleza hilo kwa kuhakikisha kuwa
inakuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka
mitano (2016/17-2020/21) kupitia Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya
Tanzania (2015/16-2019/20) ambao unatekelezwa kwenye maeneo matatu muhimu.Aliyataja maeneo hayo kuwa ni Utawala Bora, Uwajibikaji na Usimamizi wa Rasilima, Upatikanaji wa Haki kwa wakati pamoja na Uimarishaji wa imani ya wananchi kwa Mahakama na ushirikishwaji wa wadau kwenye shughuli za Mahakama.
Jaji Mkuu alisema ili kutekeleza Mpango huo wa Maendeleo wa Taifa, Watumishi wa Mahakama hawana budi kujiona kuwa wao ni sehemu ya mabadiliko na kwamba mabadiliko yaliyopo sasa ndani ya Mahakama yanatokana na wao kutoa huduma bora kwa wananchi.
Alisema imeshirikisha Watumishi wake katika hatua mbalimbali za kujenga Mpango Mkakati na kutekeleza kwa vitendo. Kupitia baraza la katika utoaji wa huduma za mahakama kuepuka migogoro isiyo ya lazima sehemu za kazi.
Mabaraza ya Wafanyakazi sehemu za kazi yanaundwa kwa mujibu wa Sheria na Miongozo ambayo ni Agizo la Rais namba 1 la mwaka 1970, Sheria ya Utumishi wa Umma namba 8 ya mwaka 2002 pamoja na kanuni zake za mwaka 2003 na Sheria ya Majadiliano ya pamoja katika Utumishi wa Umma Namba 19 ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake za mwaka 2005.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni