Na
Lydia Churi
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa
kufungua Kongamano la kimataifa kuhusu Mahakama na Jinsia Barani Afrika
litakalofanyika kwa mara ya kwanza nchini na katika Bara la Afrika kuanzia Juni
11 hadi 13 jijini Arusha.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu
ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amesema kongamano hilo litahudhuriwa
na wajumbe zaidi ya 200 wakiwemo Majaji Wakuu, Majaji, Mahakimu na wadau
wengine kutoka nchi 51 barani Afrika.
Jaji
Kiongozi amesema pamoja na wajumbe hao, kongamano hilo pia litahudhuriwa na Makamu
wa Rais wa Benki ya Dunia Bi. Sandie Okoro ambaye tayari ameshawasili nchini.
Malengo
makuu ya Kongamano hilo ni nchi za bara la Afrika kubadilishana uelewa kuhusu
changamoto za jinsia na upatikanaji wa haki, kubadilishana uzoefu na mikakati
ya kimataifa ya kusukuma mbele ajenda ya jinsia ili kuendeleza sekta ya sheria
na kuwapa washiriki nafasi ya kujadili masuala yahusuyo jinsia na upatikanaji
wa haki.
Jaji
Kiongozi amesema kongamano hilo pia linatarajiwa kujenga ushirikiano baina ya
Mataifa katika kuleta usawa wa kijinsia na kuyafanya masuala ya jinsia kuwa
sehemu muhimu ya mfumo wa Mahakama. Aidha,
kongamano hilo pia litatoa fursa kwa Majaji Wakuu na wadau wengine muhimu
kwenye sekta ya sheria kufahamiana na kubadilishana uzoefu.
Akifafanua, Dkt. Feleshi amesema
kongamano hilo litajadili masuala muhimu ya jinsia na upatikanaji wa haki na
litajikita katika masuala muhimu ya kijinsia ndani ya Mahakama na sekta ya
utoaji haki kwa ujumla, ikiwemo umuhimu wa jinsia katika Mahakama, upatikanaji
wa haki kwa wanawake na ukatili wa kijinsia.
Amesema kongamano hilo ni alama
muhimu katika historia ya Mahakama ya Tanzania kwa kuwa linatarajiwa kutoa
mchango utakaoleta mabadiliko makubwa ya kisera kuhusu jinsia na upatikanaji wa
haki barani Afrika kwa kuwa ukatili wa kijinsia ni changamoto ya dunia
inayohitaji mikakati ya kimataifa na kikanda ili kukabiliana nayo.
Kongamano hilo la siku tatu la kihistoria
nchini limeandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia
pamoja na wadau wengine ikiwemo Taasisi ya Uongozi wa Mahakama (IJA) na chama
cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA).
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Eliezer Feleshi(katikati)
akizungumzia jambo wakati na waandishi
wa habari leo Juni 7 ,mwaka huu kuhusu Mkutano wa Kimataifa utakaojadili masuala ya Kijinsia, utakaoanza Juni 11 hadi
13, mwaka huu mkoani Arusha.Kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revokati na (kushoto)
ni Katibu wa Jaji Kiongozi, Dustan Ndunguru.
|
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revokati(kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari leo Juni 7, mwaka huu kuhusu Mkutano wa Kimataifa utakaojadili masuala Kijinsia,( katikati) ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Eliezer Feleshi na (Kushoto) ni Katibu wa Jaji Kiongozi, Mhe .Dustan Ndunguru.
Baadhi ya waandishi wa Habari wakimsiliza Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania (ambaye hayupo pichani), wakati alipofanya mkutano na waandishi hao leo Juni 7, mwaka huu.
(Picha na Mary Gwera)
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni