Ijumaa, 8 Juni 2018

MAKAMU WA RAIS WA BENKI YA DUNIA ATEMBELEA MAHAKAMA YA WILAYA KIGAMBONI: AISIFU MAHAKAMA KWA KUTUMIA TEKNOLOJIA YA MOLADI KTK UJENZI


Na Mwandishi wetu
 MAKAMU  wa Rais wa  Benki ya Dunia Bi.Sandie Okoro ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa utekelezaji wa mradi ya ujenzi wa Mahakama kwa kutumia teknolojia ya Moladi na kutaka iwe mfano wa kuigwa katika nchi nyingine za Afrika.

Pia,  ameipongeza Mahakama hiyo kwa uwiano wa jinsia kwa uwepo wa watumishi wengi wanawake.

Sandie alitoa pongezi leo, Juni 08 jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea jengo la Mahakama ya Wilaya na  ya Mwanzo Kigamboni ambalo limejengwa kwa kutumia teknolojia ya Moladi na kupata fursa ya kujionea mahakama inayotembea 'Mobile Court'.

 "Nashukuru kwa mada zilizowasilishwa. Ujenzi wa muda mfupi na majengo mazuri ambayo ni ya mfano wa kuigwa kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla," alisema Sandie.

Alisema taarifa za ujenzi wa majengo hayo inapendeza kuzifikia nchi nyingi kwa kuwa majengo yake ni mazuri na yamejengwa kwa viwango vizuri kuendana na thamani ya fedha.

Makamu huyo wa Rais wa Benki ya Dunia, Sandie ambaye yuko nchini kuhudhuria mkutano wa kimataifa juu ya upatikanaji wa haki na jinsia kwa bara la Afrika na kutembelea Mahakama ya Tanzania kujionea Mradi wa Maboresho wa huduma za Mahakama unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, alipongeza Mahakama ya Tanzania kwa uwiano wa jinsia.

Alitoa pongezi hizo baada ya kushuhudia watumishi wengi wa mahakama hiyo wakiwa wanawake na wanawake kushuriki katika ujenzi wa majengo ya mahakama kwa kutumia teknolojia ya Moladi.

Kuhusu Mahakama inayotembea, Sandie alisema ni ubunifu mzuri ambao katika utendaji haki utaweza kuwafikia wananchi kwa urahisi hivyo kusaidia kutatua migogoro mbalimbali katika jamii kwa haraka na kwa wakati.

Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Joachim Tiganga, alisema ujenzi wa Mahakama hiyo unarahisisha upatikanaji wa haki kwa wakazi wa Kigamboni ambao walikuwa wakisafirisha kilomita 50 kwenda Temeke kufuata huduma ya Mahakama ya Wilaya.
Alisema eneo lililojengwa mahakama hiyo,  awali lilikuwa na Mahakama ya Mwanzo na jengo hilo jipya lina miundombinu muhimu ikiwemo ya walemavu na lina mfumo wa teknolojia.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Dk. Daniel Mbisso, alieleza teknolojia ya Moladi ilivyotumika kujenga majengo mbalimbali ya Mahakama na kusema ujenzi wake ni rahisi na wa gharama nafuu na huchukua muda mfupi.
Alisema teknolojia hiyo inatumika kujenga majengo ya Mahakama kutokana na changamoto ya majengo ya mahakama.

Alitaja mahakama zilizojengwa kwa kutumia teknolojia hiyo kuwa ni Kibaha, Bagamoyo, nyumba za watumishi Bagamoyo, Kituo cha Mafunzo kilichoko Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Kigamboni, Mkuranga na Kawe.



Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Bi Sandie Okoro akipolewa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Eliezer Feleshi mara kuwasili  katika Mahakama ya Wilaya Kigamboni na Mahakama ya Mwanzo leo Juni 8,mwaka huu.

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Bi .Sandie Okoro(kushoto) akisikiliza  maelezo ya mchoro wa jengo la Mahakama ya Wilaya Kigamboni na Mahakama ya Mwanzo, kutoka kwa Mhandisi Khamadu Kitunzi.


Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Bi .Sandie Okoro(wa pili kushoto) akisikiliza mada kuhusu ujenzi wa  majengo ya Mahakama kwa kutumia teknolojia ya Moladi wakati alipotembelea Mahakama ya Wilaya Kigamboni na Mahakama ya Mwanzo.


Naibu  Msajili  Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Joachim  Tiganga  akitoa mada kuhusu ujenzi   Mahakama ya Wilaya Kigamboni na Mahakama ya Mwanzo kwa kutumia teknolojia ya Moladi.


Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Bi. Sandie Okoro akisalimiana na baadhi ya watumishi wa   Mahakama ya Wilaya Kigamboni na Mahakama ya Mwanzo, iliyoko jijini Dar es Salaam.


Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Bi. Sandie Okoro (wanne kutoka kulia) akiwa katika  picha ya pamoja  na baadhi ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kigamboni na Mahakama ya Mwanzo, iliyoko jiji Dar es Salaam.


Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Bi. Sandie Okoro  akiwa  kwenye gari la mahakama inayotembea alipotembelea Mahakama ya Wilaya Kigamboni na Mahakama ya Mwanzo, iliyoko jijini Dar es Salaam.



Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Bi .Sandie Okoro (kushoto) akitembelea  Mahakama ya Wilaya Kigamboni na Mahakama ya Mwanzo, iliyoko jijini Dar es Salaam. Katikati ni   Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Eliezer Feleshi na Kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revokati.
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni