Na
Mary Gwera na Lydia Churi-ARUSHA
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amezishauri Mahakama za
Afrika kuanzisha Mahakama maalum zitakazoshughulikia mashauri ya Jinsia ili
kuwezesha usawa na haki za kijinsia kupatikana kwa haraka.
Akifungua Mkutano wa Jinsia
na Haki ulioandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia
leo Jijini Arusha, Makamu wa Rais amesema kuwa Majaji Wakuu na Wanasheria Wakuu
ni Watendaji muhimu katika kuhakikisha
kuwa mifumo ya haki inaimarishwa kwenye nchi zao.
“Nawapongeza kwa kazi
nzuri mnayofanya, katika Bara hili la Afrika na Dunia kwa ujumla licha ya
changamoto mnazokutana nazo katika nchi zenu, Mahakama Afrika zimekuwa ni
msimamizi wa haki kwa raia wake,” alisema Makamu wa Rais.
Alisema Wanawake na
Watoto ni makundi yaliyosahaulika katika jamii ukilinganisha na wanaume.
Wanawake wamekuwa nyuma katika masuala ya kielimu, umiliki wa ardhi, uongozi
katika ngazi mbalimbali za maamuzi pamoja na umiliki wa mali za familia.
Alisema kuanzishwa kwa
Mahakama za Kijinsia kutasaidia kuondokana na vitendo vya unyanyasaji dhidi ya
Wanawake katika jamii.
Makamu wa Rais alisema,
utafiti uliofanywa na Taasisi mojawapo nchini Tanzania ijulikanayo kama ‘Tanzania
Demographic Health Survey’ (TDHS) mwaka 2010 unaonyesha kuwa asilimia 44 ya
Wanawake walioolewa wenye umri wa kati ya miaka 15-49 wanakabiliwa na ukatili
wa kijinsia kutoka kwa Wenzi wao.
Katika kukabiliana na
changamoto zinazowakabili wanawake, Makamu wa Rais amesema Tanzania imejiwekea
Mikakati ambayo mbalimbali ikiwemo maboresho katika Sekta ya Sheria
yaliyosababisha kutungwa na kurekebishwa kwa baadhi ya Sheria zinazohusiana na
masuala ya Jinsia na kuanzishwa kwa madawati ya jinsia katika vituo vya Polisi
nchini.
Sheria zilizotungwa ni Sheria
ya Ardhi na Sheria ya Ardhi ya Kijiji (Land Act and the Village Land Act) iliyowezesha
Wanawake kumiliki ardhi, pamoja na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 (Law of the
Child Act in 2009). Pamoja na kutungwa kwa Sheria hizo, Tanzania pia iliifanyia
marekebisho Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (Sexual Offences Special Provision
Act (SOSP) ya mwaka 1998.
Hata hivyo, Makamu wa
Rais alisema Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano
2015/2016-2019/2020 pamoja na Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama inao
mpango wa kupitia taratibu za Mashauri zilizopo ili kuharakisha mashauri
yanayohusu wanawake na makundi mengine wakiwemo watoto.
Kupitia Mpango Mkakati
huo, Mahakama ya Tanzania itahakikisha kuwa mashauri yanayohusu Unyanyasaji wa
Kijinsia na ukandamizaji dhidi ya Wanawake yanapewa kipaumbele katika taratibu
za Kimahakama, jitihada hizi pia zinaenda sambamba na Dira ya Mahakama ya Tanzania
ambayo ni Haki sawa kwa wote na kwa wakati.
Wakati huo huo Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema safari ya kuelekea kwenye
upatikanaji wa haki na usawa wa kijinsia hauwezi kupatikana kwa kutungwa na
kufanyiwa marekebisho kwa baadhi ya sheria.
Alisema pamoja na
kutungwa na kurekebishwa kwa sheria hizo, bado zipo changamoto za upatikanaji
wa haki na usawa wa kijinsia hivyo aliwataka Wajumbe wa Mkutano huo kuhakikisha
kuwa wanajadiliana na kuyatafutia ufumbuzi masuala haya.
Aidha; Mhe. Jaji Mkuu
aliishukuru Benki ya Dunia (WB) ambayo imeandaa Mkutano huu kwa kushirikiana na
Mahakama ya Tanzania Mkutano huu wa kihistoria ambao umefanyika kwa mara ya
kwanza katika bara la Afrika na nchini Tanzania.
Baadhi ya Wajumbe
wanaohudhuria Mkutano huo wa siku tatu ni pamoja Majaji Wakuu kutoka nchi 12 za
Afrika, Majaji wa Mahakama za Juu ‘Supreme Courts’, Majaji wengine pamoja na Wanasheria
mbalimbali.
Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasili katika
Viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa (AICC) kwa ajili ya kufungua rasmi
Mkutano wa Jinsia na Haki uliondaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana
na Benki ya Dunia. Katikati ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma na kulia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.
Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na Viongozi
wengine wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya ufunguzi wa Mkutano huo, wa tatu kulia
ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, wa pili kulia ni Jaji
Mkuu wa Kenya, Mhe. David Maraga, wa tatu kushoto ni Makamu wa Rais wa Benki wa
Dunia, Dkt. Sandie Okoro, wa pili kushoto ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe.
Prof. Palamagamba Kabudi, wa kwanza kushoto ni Mwakilishi Mkazi wa Benki ya
Dunia Nchini, Bi. Bella Bird, na wa kwanza kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha,
Mhe. Mrisho Gambo.
Mwakilishi Mkazi wa
Benki ya Dunia Nchini, Bi. Bella Bird akisoma risala yake katika hafla ya
ufunguzi rasmi wa Mkutano huo.
Baadhi ya Majaji wa
Mahakama ya Rufani pamoja na Washiriki wengine wa Mkutano huo wakifuatilia
kinachojiri.
Washiriki wakimsikiliza
Bi. Bella Bird alipokuwa akitoa risala yake.
Makamu wa Rais wa Benki
wa Dunia, Dkt. Sandie Okoro akitoa maneno ya utangulizi kabla ya ufunguzi rasmi
wa Mkutano huo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akifungua Mkutano huo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akifungua Mkutano huo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akichangia mada wakati wa Mkutano.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni