Na
Lydia Churi-Arusha
Waziri wa Katika Katiba
na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema Mahakama katika bara la Afrika
zina jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa haki za wanawake zinalindwa.
Akifunga Mkutano wa Kimataifa
wa siku tatu wa Jinsia na Haki leo jijini Arusha, Prof. Kabudi amesema pamoja
na Mahakama hizo kulinda haki za Wanawake, pia zina mchango katika kuhakikisha
kuwa Sheria zinazotungwa katika zinalenga katika kuufikia usawa wa kijinsia.
Aidha, Waziri wa Katiba
na Sheria amesema kupitia mkutano huo, imefahamika kuwa endapo Majaji pamoja na
Mahakama kwa ujumla zitatoa kipaumbele kwenye kesi zinazohusu masuala ya kijinsia ni wazi
kuwa usawa wa kijinsia utafikiwa katika nchi za bara la Afrika.
Prof. Kabudi
alizishauri Mahakama hizo kutoa kipaumbele kwenye kesi zinazohusu masuala ya
kijinsia ikiwemo unyanyasaji na ukandamizaji dhidi ya wanawake na kufuatwa kwa
taratibu za kimahakama ili kulinda hadhi na utu wa Mwanamke.
Alisema majadiliano ya
kina ya mkutano huo yamebainisha kuwa wanawake na wasichana hasa katika nchi za
Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara bado wanakabiliwa na unyanyasaji wa
kijinsia ikiwemo kupigwa na kuteswa na wenzi wao pamoja na kubakwa. Aliongeza
kuwa kinachosikitisha zaidi ni kuwa hata wale wanaume wanaohusika na vitendo hivi
hawaadhibiwi au wachache wanaoadhibiwa hupewa adhabu ndogo isiyolingana na kosa
walilolitenda.
Alisema Mahakama za
Afrika zinapaswa kuwa ni sehemu ya mageuzi yatakayofikia kwenye usawa wa
kijinsia kwa wanawake na wasichana kwa kutoa mawazo yatakayochangia katika kuinua
hadhi na utu wa mwanamke.
Prof. Kabudi alisema
Serikali pamoja na Mihimili mingine imefanya jitihada za makusudi katika
kupambana na vitendo vya ukatili, unyanyasaji na ukandamizaji dhidi ya wanawake
hivyo juhudi hizo zinapaswa kupongezwa.
Aliishukuru na kuipongeza
Benki ya Dunia pamoja na Mahakama ya Tanzania kwa kuandaa Mkutano huo muhimu na
wa kihistoria katika bara la Afrika
ambao umeonyesha kuwa maendeleo ya kweli hayatapatikana bila ya kuwepo kwa usawa wa kijinsia.
Alisema Serikali ya
Tanzania itayafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa kwenye mkutano huo na
kujipanga namna ya kutekeleza kwa manufaa ya Tanzania pamoja na nchi nyingine za
Afrika kwa ujumla.
Wakati huo huo, Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewashukuru wajumbe wa Mkutano
huo kwa kufika na kutoa mchango wao mkubwa wa mawazo utakaowezesha kufikiwa kwa
maendeleo ya kiuchumi yatakayotokana na kufikiwa kwa usawa wa kijinsia.
Jaji Mkuu pia aliishukuru
Benki ya Dunia kupita Makamu wa Rais wa Benki hiyo, Sandie Okoro kwa kuandaa
Mkutano wa Jinsia na Mahakama kwa nchi za Afrika.
Mkutano wa kimataifa wa
siku tatu wa jinsia na Mahakama ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa sekta ya
Sheria kutoka nchi mbalimbali wakiwemo Majaji Wakuu 12, Majaji wa Mahakama za
Juu (Supreme Court), Majaji wa Mahakama
ya Rufani, Majaji wengine pamoja na wanasheria mbalimbali kutoka nchi 51 za
bara la Afrika.
Waziri wa Katiba na
Sheria pamoja , Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania pamoja na Washiriki wengine wa Mkutano huo wakiimba
wimbo wa Taifa kabla ya Mhe. Waziri kufunga rasmi Mkutano huo.
Waziri wa Katiba na
Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akitoa hotuba yake ya kufunga Mkutano wa
Jinsia na Mahakama Afrika, Mkutano huo wa siku tatu (3) ulianza rasmi Juni 11.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa maneno ya utangulizi kabla ya kumkaribisha
rasmi Mhe. Waziri kufunga rasmi mkutano huo, Mhe. Jaji Mkuu ameishukuru Benki
ya Dunia ambayo imeshirikiana kwa karibu na Mahakama kufanikisha Mkutano huo,
vilevile amewashukuru Wajumbe wote kwa ujumla wao kushiriki katika Mkutano.
Sehemu
ya Washiriki wakiwa katika Mkutano huo.
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiteta jambo na Makamu wa Rais
wa Benki ya Dunia, Dkt. Sandie Okoro.
Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi pamoja na baadhi ya Majaji wengine
waliohudhuria katika Mkutano huo.
Jaji wa Mahakama Kuu,
Kanda ya Mwanza, Mhe. Joaquine Demello akikabidhi zawadi ya Kitenge cha Chama
cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof.
Palamagamba Kabudi.
Jaji wa Mahakama Kuu,
Kanda ya Mwanza, Mhe. Joaquine Demello akikabidhi zawadi ya Kitenge cha Chama
cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) kwa Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Dkt.
Sandie Okoro.
Jaji wa Mahakama Kuu,
Kanda ya Mwanza, Mhe. Joaquine Demello akikabidhi zawadi ya Kitenge cha Chama
cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Anna Mghwira.
(Picha na Mary Gwera,
Arusha)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni