Na Magreth Kinabo
Kaimu
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Mhe. Mohamed Gwae amesema Mahakama
inayotembea itaanza kufanya kazi katika Jiji la
Mwanza na Dar es Salaam ili
kusogeza huduma za kimahakama kwa wananchi na kutoa haki kwa wakati.Mhe. Gwae alisema hayo jana wakati akifungua mafunzo ya siku mbili Mkoani Mwanza kwa Watumishi wa Mahakama pamoja na wadau kuhusu huduma zitakazotolewa na Mahakama inayotembea.
Kaimu
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Mhe. Mohamed Gwae, wakati
akifungua mafunzo ya siku mbili Mkoani Mwanza kwa Watumishi wa Mahakama pamoja
na wadau kuhusu huduma zitakazotolewa na Mahakama inayotembea. Kulia ni Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. John Kahyoza.
Kaimu
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Mhe. Mohamed Gwae ,(waliokaa
katikati). Akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Mahakama ya
Tanzania mara baada ya kufungua mafunzo ya siku mbili kuhusu mahakama
inayotembea. Kushoto ni Msajili wa Mahakama Rufani,Mhe. John
Kahyoza na kulia ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Mhe. Mary Moyo.
|
Msajili wa Mahakama Mahakama ya Rufani Mhe. John Kahyoza akitoa mada ya uzoefu wa nchi mbalimbali kuhusu mahakama inayotembea wakati wa mafunzo hayo. |
Akielezea maana ya Mahakama Inayotembea,
alisema kwamba, ni dhana inayomaanisha mahakama katika ngazi fulani kuhamisha
huduma zake na kuzitolea katika sehemu mbalimbali ndani ya mamlaka yake.
Mahakama hizi ni gari maaluumu ambalo lina chumba maalumu kilichotengenezwa
ndani ya gari kwa ajili ya kusikilizia mashauri na kuyatolea maamuzi. Chumba
hicho ni kama ilivyo ofisi au “chamber” ya hakimu kwa sasa.
Alisema kwa sasa Mahakama zinazotembea
zimeanzishwa kwa lengo la kusogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi hasa
sehemu zisizo na mahakama au maeneo yenye watu wengi.
“Kwa Kanda ya Mwanza, maeneo ya Buswelu,
Buhongwa na Igoma yamekuwa na watu wengi sana na hivyo kuhitaji huduma ya
Mahakama ya Mwanzo,” alisema Mhe. Jaji Gwae.
Aliongeza kwa kusema kusema kwamba, kwa
kutumia Mahakama zinazotembea, Mahakama za Mwanzo Mkuyuni, Mwanza Mjini na
Ilemela zinaweza kuhamishia shughuli zake katika maeneo yenye watu wengi na
yasiyokuwa na huduma ya Mahakama karibu.
Mahakama inayotembea
itatumika pia kusikiliza na kutoa maamuzi kwa mashauri yanatokana na makosa ya
uvuvi haramu, ambayo mara nyingi yanasikilizwa na Mahakama za Wilaya.
Aidha alitaja matumizi mengine ya Mahakama
inayotembea ni kutoa elimu ya sheria, kutoa matangazo mbalimbali ya kimahakama
pamoja na huduma nyingine za Kimahakama kama vile kutoa fomu za kufungulia
mashauri mbalimbali. Wananchi watanufaika na elimu hiyo hasa kuhusiana na
masuala ya mirathi, wosia na migogoro ya ndoa.
Akizungumzia kuhusu umuhimu wa Mahakama hiyo, Mhe. Jaji
alisema kwamba, Mahakama hizi zitawapunguzia
wananchi gharama na muda wa kutafuta huduma za Mahakama.
“Ni dhamira ya Mahakama
ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wake katika kuhakikisha huduma za Mahakama
zinapatikana kwa wananchi kwa karibu, haraka na wote. Matumaini yangu ni
kwamba mafunzo haya yataleta tija katika
kutimiza lengo lililokusudiwa la utoaji haki kwa wakati na kwa gharama nafuu. ”
alisisitiza.
Aliwataka washiriki
wa mafunzo hayo, kuwa walimu wazuri wa kuwaelemisha watumishi wengine,
viongozi mbalimbali wa serikali, taasisi binafsi na wananchi kwa ujumla.
Kwa
upande wake Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania,Mhe. John Kahyoza aliwataka
washiriki hao kuzingatia maadili na kuwa wabunifu na weledi wanapotoa huduma
hiyo.
Hakimu
Mkazi Mwandamizi, Mhe. Victoria Nongwa,
kutoka Kurugenzi ya Menejimenti ya Mashauri, aliwataka washiriki kuhakikisha wanajifunza masuala
ya kompyuta hususani kwenye
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) ilikuboresha utendaji kazi na kuachana na matumizi ya karatasi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni