Kufuatia
tangazo la Serikali Na. 112 la tarehe Februari 01, 2019 la uanzishwaji wa Mahakama Kuu Kanda
za Kigoma na Musoma, Aprili 05, 2019 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma,
Mhe. Jaji John Kayoza ameripoti na kukabidhiwa rasmi kituo hicho.
Mhe. Jaji Kahyoza aliambatana na Mhe. Jaji Zefrine
Galeba pamoja na Naibu Msajili wa Kanda hiyo, Mhe, Mary Moyo ambapo pia walipata
nafasi ya kutembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na kukutana na Kaimu wake Mhe. Mkuu wa
Wilaya ya Musoma, Bw. Vicent Naano.
Katika
mazungumzo yao, Mkuu huyo wa Wilaya
alisema, kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Mara wamefurahishwa na ujio wao
kwani sasa kero za wananchi kwenda Mwanza kutafuta haki zao zimefika ukomo.
“Wananchi
wengi walikuwa wakifika katika ofisi yangu kuomba nauli za kwenda Mahakama Kuu
Mwanza umbali wa Km 223 kufuatilia mashauri yao yaliyopo katika Kanda hiyo,”
alieleza Mhe. Naano.
Aidha;
Mhe. Naano alielezea changamoto mbalimbali zilizopo katika Mkoa huo kama vile
uwepo wa mashauri mengi ya mauaji, ubakaji, ukatili wa kijinsia, uonevu kwa
wajane na yatima, ukosefu wa madalali wa Mahakama pamoja na changamoto ya
utoaji wa ushahidi.
Akikabidhi
kituo hicho, Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Mwanza, Mhe. Jaji Sam Rumanyika ambaye Kanda
yake imekuwa mlezi wa Kanda mpya ya Musoma kwa muda mrefu alionyeshwa kufurahishwa na Kanda mpya ya Musoma na
kusema kuwa Kanda hiyo ni zao la Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza.
Kwa
upande mwingine, Mhe. Jaji Rumanyika aliwaasa Watumishi wa Kanda hiyo kuendeleza
ushirikiano ule waliokuwa wakiutoa katika Kanda ya Mwanza, na pia aliwaambia
watumishi kuwa wamepata kiongozi bora na sio bora kiongozi.
Naye
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Jaji Kahyoza alimshukuru Jaji
Rumanyika kwa kuilea Musoma katika kipindi chote na kumuomba asichoke kutoa
msaada pale atakapohitajika kwani mzazi hawezi kumtupa mwana.
Aidha;
Mhe. Jaji Kahyoza alisema, hadi sasa tayari zaidi ya mashauri 100
yameshafunguliwa katika Masjala ya Mahakama Kuu Musoma iliyopo katika Ofisi za
Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma kwa muda na mashauri hayo yatasikiliziwa Musoma.
“Mashauri
haya pamoja na mashauri yote yaliyofunguliwa kuanzia 01/02/2019 yatasikiliziwa
Musoma, ila kwa yale mashauri ambayo yalifunguliwa Mwanza kabla ya tarehe hiyo
yatasikilizwa hukohuko na Jaji Galeba atabaki Mwanza akiyashughulikia akimaliza
ndipo atakuja Musoma kuungana nami pamoja na Msajili ambao wao watakuwepo
kituoni rasmi kuanzia tarehe Aprili 10, 2019,” alieleza Mhe. Jaji Kahyoza.
Katika
mazungumzo yake Mhe, Jaji Mfawidhi huyo alisema kuwa kauli mbiu ya Mahakama Kuu
Musoma itakuwa ni Mahakama ya watu, mteja kwanza (Peoples' Centric Judiciary).
“Tuwahudumie
wateja wetu kwa moyo na matatizo au changamoto zetu za ndani zisiathiri
shughuli za utoaji haki kwa wateja wetu,” alisisitiza Mhe. Jaji Kahyoza.
Naye
Mhe, Jaji Galeba alisema, ukiondoa misikitini, makanisani na mahekaluni ni
Mahakamani pekee ndiko mtu anatarajia kupata Amani, suluhu na haki ya kweli na
hivyo kwa ujio wao aliwaomba watumishi wote kuwa wamoja ili kumfanya mwananchi
aone Mahakama ni sehemu salama ya kukimbilia.
Katika
ujio wake Mhe, Jaji Mfawidhi alitembelea na kukagua miradi ya ujenzi
inayoendelea ya Mahakama Kuu Musoma na nyumba za Waheshimiwa Majaji.
Jaji Mfawidhi Kanda ya
Musoma (wa tatu kushoto), Mkuu wa Wilaya ya Musoma. Bw. Vicent Naano (wa nne kushoto) pamoja na viongozi wengine
wa Mahakama Kuu Musoma na viongozi wa Wilaya ya Musoma wakiwa katika picha ya
pamoja mbele ya jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-Mara.
Picha ya pamoja mbele
ya Jengo la Mahakama Kuu Musoma, wa tatu kushoto ni Jaji Mfawidhi Mahakama
Kuu kanda ya Mwanza, Mhe. Sam Rumanyika, wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi Kanda
ya Musoma, Mhe. John Kahyoza, wa kwanza kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu,
Kanda ya Musoma, Mhe. Zefrine Galeba, katikati ni Mkuu wa Wilaya-Musoma,
Mhe. Vicent Naan, wa tatu kulia ni Naibu Msajili Mahakama Kuu-Kanda ya Musoma,
Mhe. Mary Moyo, wengine ni baadhi ya Maafisa wa Mahakama na wilaya ya Musoma
walioshuhudia makabidhiano ya miradi ya ujenzi inayoendelea katika Kanda hiyo
ya Musoma.
Mhe.Jaji
Mfawidhi (wa kwanza kushoto) akizungumza na baadhi ya wananchi aliowakuta wakisubiri huduma za
kimahakama katika Mahakama ya Wilaya Musoma.
Viongozi wa Mahakama, Kanda ya Mwanza na Musoma wakizungumza na Watumishi wa Mahakama, Kanda ya Musoma, (wa pili kushoto) ni Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Mwanza, Mhe. Sam Rumanyika, wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Musoma, Mhe. John Kahyoza na wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Zefrine Galeba.
Sehemu
ya Watumishi walioshuhudia makabidhiano hayo wakifuatilia kwa karibu nasaha
wanazopewa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni