Na
Mary Gwera, Mahakama Kuu-Iringa
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewataka Mahakimu
Wafawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa kuongoza kwa mfano ikiwa ni pamoja na
kuondosha mashauri kwa wakati.
Mhe. Jaji Kiongozi
alitoa maelekezo hayo Aprili 06, 2019, alipokuwa akizungumza na Mahakimu Wafawidhi kutoka
Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, Mahakama ya Wilaya Iringa, Mahakama ya Wilaya
Mufindi, Mahakama ya Wilaya Makete, Mahakama ya Wilaya Kilolo, Mahakama ya
Hakimu Mkazi Njombe na Mahakama ya Wilaya Njombe.
Mhe. Jaji Dkt. Feleshi
aliwaelekeza Mahakimu hao Wafawidhi kusimamia na kuhakikisha kuwa mashauri yanaamuliwa
kwa wakati sanjari na kuhakikisha kuwa nakala za hukumu zinachapwa na
kukabidhiwa kwa wadaawa na wadau bila kuchelewa.
“Nyote mnaelewa kuwa
Mahakama imejiwekea malengo katika usikilizaji wa mashauri, hivyo ni wajibu
wenu kusimamia malengo ambayo yameelekezwa kupitia nyaraka mbalimbali za
Mahakama, kwahiyo ni muhimu kujituma ili kufikia malengo husika,” alieleza Mhe.
Jaji Kiongozi.
Mhe. Jaji Kiongozi
aliuagiza pia Uongozi wa Mahakama Kanda ya Iringa kutoishia tu kupokea taarifa
za mashauri bali kupata suluhisho kwa Mahakama ambazo hazifanyi vizuri katika
uondoshaji wa mashauri.
“Ninyi ni Viongozi,
mkiona vitu havitekelezeki au kama kitu kinashindikana jiulize tatizo ni nini,
na kama tatizo ni sheria jengeni hoja sheria husika zirekebishwe,” alisisitiza
Mhe. Jaji Dkt. Feleshi.
Aliongeza kuwa kama
Hakimu ameshindwa kufikia malengo yaliyowekwa anapaswa kutoa taarifa na kueleza
sababu zilizochangia kutofikia malengo husika ili utatuzi upatikane kuanzia
ngazi ya kituo husika mpaka ngazi ya Kanda au ikishindikana ifikishwe ngazi ya
Makao Makuu kwa ufumbuzi.
Kwa upande wake, Jaji
Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Iringa, Mhe. Jaji Panterine Kente
alimuhakikishia Mhe. Jaji Kiongozi kuwa wamepokea maelekezo yote aliyoyatoa na
kuahidi kushughulikia vikwazo vyote ili kusonga mbele.
Mhe. Jaji Kiongozi yupo
ziarani kikazi katika Mahakama Kanda ya Iringa na anatarajia kufanya ziara pia
katika Mahakama Kanda ya Mbeya lengo likiwa ni kujua hali ya
maendeleo ya utekelezaji wa huduma mbalimbali za Mahakama na
vilevile kuwakumbusha Watumishi wa Mhimili huu kuendelea kutekeleza jukumu la
msingi la utoaji haki nchini kwa ubora wa hali ya juu na kwa manufaa ya wananchi
ambao ndio walengwa wakuu.
Jaji Kiongozi, Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (katikati) akizungumza na
Wahe. Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama Kanda ya Iringa (hawapo pichani), kushoto
ni Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, Mhe. Jaji Panterine Kente na
kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, Mhe. Jaji Immaculata Kajetan
Banzi.
Pichani ni Wahe.
Mahakimu Wafawidhi wa Kanda ya Iringa wakiwa katika kikao na Mhe. Jaji Kiongozi.
Baadhi ya Maafisa wa
Mahakama walioshiriki katika kikao hicho wakifuatilia kwa makini maelekezo yanayotolewa na Mhe. Jaji Kiongozi (hayupo pichani).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni