Na
Mary Gwera, Mahakama-Iringa
Katika mwendelezo wa ziara yake ya Mahakama Kanda ya
Iringa, Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki
Feleshi amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Ally
Hapi.
Katika mazungumzo yake
na Mkuu huyo wa Mkoa yaliyofanyika Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Aprili
05, 2019, Mhe. Jaji Kiongozi alipata wasaa wa kutoa elimu kuhusu mpango Mkakati
wa Mahakama ambapo aliizungumzia nguzo namba tatu (3) ya Kurejesha imani ya jamii na
ushirikishwaji wa wadau.
“Mahakama ya Tanzania
inaendelea kuboresha huduma zake, ambapo kupitia Mpango Mkakati wetu, nguzo
namba tatu (3) inatuelekeza kushirikiana na Wadau katika ufanyaji kazi,”
alieleza Mhe. Jaji Kiongozi.
Mbali na nguzo hiyo, Mhe.
Jaji Kiongozi alimueleza Mhe. Hapi kuwa Mahakama inaendelea na maboresho ya
huduma zake ikiwa ni pamoja na kumaliza mashauri kwa wakati huku akitoa ombi
kwa Mkuu huyo wa Mkoa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya
Mkoa huo kuelekeza Jeshi la Polisi kuharakisha kumaliza upelelezi.
“Mahakama inaendelea
kushughulikia suala la mlundikano ambapo imejiwekea malengo yake kwa kujiwekea
kiwango cha idadi na muda wa mashauri kumalizika kwa kila ngazi ya Mahakama, hivyo
hili haliwezi kufanikiwa bila ushirikiano na Wadau,” alieleza.
Hata hivyo; Mhe. Jaji
Kiongozi alieleza changamoto ya ukosefu wa Gereza la kuhifadhi mahabusu na
wafungwa katika Wilaya ya Kilolo na kumuomba Mkuu huyo wa Mkoa kunusuru hali
hiyo.
Aidha; Jaji Kiongozi,
Mhe. Dkt. Feleshi aliongeza kuwa suala la maboresho linaenda sambamba na
ushughulikiaji wa maadili ya Mahakimu na Watumishi wa Mahakama kwa ujumla kwa
kuchukua hatua stahiki kwa wale wanaojihusisha na vitendo vya Rushwa na mienendo
ya ukiukwaji wa maadili kwa ujumla.
“Mahakama ya Tanzania
haina simile na Maafisa wake wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na vitendo
vya ukiukwaji wa maadili, mbali na Kamati za Maadili za Mahakimu, Mhe. Jaji
Mkuu ameelekeza Majaji Wafawidhi kushughulikia masuala ya rushwa na kutoa
taarifa pale inapotokea viashiria vya rushwa ili hatua stahiki ziweze
kuchukuliwa,” alisisitiza Mhe. Jaji Dkt. Feleshi.
Akizungumzia suala la
maadili ya Mahakimu, Mhe. Jaji Kiongozi alieleza kuwa kwa ngazi ya mkoa,
Mahakama hutegemea kupata taarifa kutoka katika Kamati za Maadili za Mahakama
za mikoa ili kufanya maamuzi stahiki ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi,
kusimamishwa kazi au kuonywa.
“Mara zote tunasisitiza
Kamati hizi ambazo Mwenyekiti wake ni Mkuu wa Mkoa kukaa na kuwasilisha taarifa
katika Mahakama za Mahakimu wake wanaotuhumiwa na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na rushwa katika Mkoa husika ili
kuchukua hatua zinazostahili kwa mujibu wa sheria,” alieleza Mhe. Jaji. Dkt.
Feleshi.
Kwa upande wake Mkuu wa
Mkoa wa Iringa, Mhe. Ally Hapi alimueleza Mhe. Jaji Kiongozi kuwa ofisi yake
inafanya kazi kwa kushirikiana na Viongozi wa Mahakama katika mkoa huo na
alimhakikishia kuwa wataendelea kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu
mbalimbali.
“Kuhusu suala la Kamati
ya Maadili ya Mahakama ya Mkoa, tumepanga kukaa mwezi Mei na tayari
nimeshawasiliana na Mahakama Iringa kuhusu kikao hicho na taarifa itatolewa,”
alisema Mhe. Hapi.
Jaji Kiongozi, Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (kulia) akizungumza jambo
na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Ally Hapi (Kushoto), wanaosikiliza (mbele
kushoto) ni Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Jaji Panterine
Kente, kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Jaji Immaculata
Kajetan Banzi.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa,
Mhe. Ally Hapi (kushoto) akisoma nakala ya kitabu cha Mpango Mkakati wa miaka
mitano wa Mahakama ya Tanzania (2015/2016-2019/2020) alichopewa na Mhe. Jaji
Kiongozi.
Mazungumzo yakiendelea,
pamoja na Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu Iringa, Mhe. Jaji Kiongozi
aliambatana na baadhi ya Maafisa wa Mahakama.
Mhe. Hapi (kushoto)
akizungumza jambo na Mhe. Jaji Kiongozi kabla ya kuagana rasmi.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama-Iringa)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni