Jumapili, 7 Julai 2019

MASHAURI ZAIDI YA 1000 YASAJILIWA KIELEKITRONIKI


Na Lydia Churi-Mahakama

Zaidi ya mashauri 1100 yamesajiliwa kupitia mfumo wa kusajili mashauri kwa njia ya kielekitroniki (E-Filling) tangu kuanza rasmi kwa mfumo huo mwezi Februari mwaka huu mpaka sasa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya, mashauri hayo yamesajiliwa na Mahakama Kuu Masjala kuu pamoja na Divisheni za Mahakama Kuu ambazo ni Ardhi, Biashara, Kazi pamoja Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Akizungumzia ufunguaji wa mashauri kwa njia ya kielekitroniki, Mhe. Nkya alisema Mahakama ya Tanzania imeanza kusajili mashauri kwa mfumo wa kielekitroniki katika Mahakama Kuu zilizoko Dar es salaam pamoja na kwenye Divisheni zote za Mahakama Kuu kwa sasa ambapo lengo ni kuwa na mfumo huo katika Mahakama zote isipokuwa Mahakama za Mwanzo.

Alisema kuanzishwa kwa mfumo huu kutamwezesha mteja kufungua shauri mahali popote alipo na kwa muda wowote na hatalazimika kufika mahakamani kufungua shauri.

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania alisema mfumo wa kusajili mashauri kwa njia ya kielekitroniki pia umeunganiashwa na mfumo wa malipo wa Serikali ili kurahisisha ulipaji wa ada ya usajili pamoja na Ada nyingine zinazotokana na huduma za Mahakama.

Alisema, Mahakama ya Tanzania pia imeanzisha huduma ya upatikanaji wa maamuzi ya mashauri ya Mahakama Kuu pamoja na Mahakama ya Rufani kupitia Tovuti ya Mahakama ya Tanzania. Mashauri yanayopatikana kwenye Tovuti ya Mahakama ni yale ya kuanzia miaka ya 1980’s.

Baadhi ya mifumo mingine iliyoanzishwa na Mahakama ya Tanzania ni pamoja na mfumo wa kuratibu mashauri (JSDS ll), mfumo huu huratibu shauri kuanzia linapofunguliwa mpaka linapomaliza. Mfumo mwingine ni ule wa kuratibu Mawakili (TAMS). Aidha, Mahakama ya Tanzania pia inao mfumo wa ramani ambao huonesha maeneo zilipo Mahakama na umbali wa kuzifikia (JMAP).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni