Na
Lydia Churi-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amependekeza makosa yote kuwa na dhamana kwa kuwa hatua hiyo itasaidia kuondoa msongamano
wa Mahabusu kwenye Magereza mbalimbali nchini.
Akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kuwakubali na kuwaapisha wanasheria waliomaliza mafunzo ya Sheria kwa vitendo kuwa Mawakili, jijini Dar es salaam leo, Jaji Mkuu ameyataja baadhi ya mapendekezo ya Mahakama yatakayosaidia kuondoa msongamano magerezani kuwa ni pamoja na upelelezi wa kesi kumalizika mapema.
Jaji Mkuu alisema Mahakama imekuwa ikilaumiwa kwa kuchelewesha kesi mahakamani lakini kinachosababisha kuchelewa kwa mashauri hayo ni upelelezi kutokukamilika kwa wakati.
“Kuchelewa kumalizika kwa shauri Mahakamani wa kulaumiwa ni wapelelezi na siyo Mahakama”, alisema Jaji Mkuu.
Alisema sheria zimeegemea
zaidi kwenye adhabu kubwa huku akitolea mfano wa mashauri ya mauaji, matumizi
ya dawa za kulevya, Uhujumu uchumi na ubakaji. Aliongeza kuwa mashauri haya
yana adhabu kubwa na upelelezi wake huchukua muda mrefu.
Alisema ili kutatua
changamoto ya msongamano wa mahabusu magerezani, Mahakama ya Tanzania pia
inapendekeza masharti ya dhamana kulegezwa na kushauri kutumiwa kwa
vitambulisho vya Taifa kwenye dhamana.
“Hivi sasa wananchi wengi
wana vitambulisho vya Taifa ambavyo vinaweza kutumika kama dhamana bila ya
kumtaka mwananchi aonyeshe mali”, alisema Prof. Juma.
Jaji Mkuu alitoa
mapendekezo hayo ya Mahakama alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na waandishi
wa habari waliotaka kufahamu Mamlaka ya kutoa Mahabusu gerezani. Kwa mujibu wa
Jaji Mkuu, Mahakama ndiyo yenye Mamlaka.
Hivi karibuni, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliagiza
kufanyika kwa uhakiki ili kubaini mahabusu na wafungwa waliobambikiwa kesi hatimaye
kuachiwa huru. Watakaonufaika na matokeo ya uhakiki huo ni mahabusu wenye kesi
ndogondogo na wafungwa watoto, wazee, na makundi mengine yenye mahitaji maalum.
Jumla ya wanasheria 720
wamekubaliwa na kuapishwa kuwa Mawakili wakiwemo Majaji nane wa Mahakama ya
Rufani, Majaji saba wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Majaji wastaafu watatu,
Manaibu Wasajili kadhaa, Mahakimu pamoja na wanasheria wengine.
Hii ni mara ya 60 kwa
Mahakama ya Tanzania kuwakubali na kuwaapisha Mawakili wapya. Kwa mara ya
kwanza Mahakama ya Tanzania iliwakubali na kuwaapisha Mawakili wapya mwaka
1986.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) pamoja na baadhi ya Wahe. Majaji wa
Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu wakiongozwa na Mhe. Jaji Kiongozi (wa tatu
kulia) wakiwa katika Sherehe ya 60 ya kuwakubali na kuwapokea Mawakili wapya 720 iliyofanyika mapema Julai 19, 2019 katika
Viwanja vya Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (Law School
of Tanzania).
Picha mbalimbali za
Mawakili wapya waliokubaliwa leo na Mhe. Jaji Mkuu. Miongoni mwa waliopata Uwakili katika sherehe hizi ni pamoja na baadhi ya Maafisa wa
Mahakama wakiwemo, Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu,
Manaibu Wasajili na Mahakimu.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Adelardus Kilangi (wa pili kushoto) pamoja na baadhi ya Viongozi wa Serikali wakiwa katika Sherehe za 60 za kuwakubali na kuwapokea Mawakili wapya 720.
Meza Kuu wakiwa katika
picha ya pamoja na sehemu ya Mawakili wapya.
Meza Kuu wakiwa katika
picha ya pamoja na Kamati ya maandalizi ya sherehe za kuwakubali na kuwapokea
Mawakili wapya.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni