Alhamisi, 11 Julai 2019

TUMIENI BARAZA LA WAFANYAKAZI KUTATUA CHANGAMOTO ZILIZOPO


 Na Magreth Kinabo.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dares Salaam, Mhe. Beatrice Mutungi, amewataka   watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kujiunga na kutumia  mkutano wa Baraza la Wafanyakazi ili  kutatua changamoto zilizopo mahali pa kazi.

Akizungumza leo wakati wa akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,  uliofanyika jijini Dares Salaam,  na kuhusisha  watumishi wa Mahakama ya Tanzania kutoka  mkoa wa Dar es Salaam,  Morogoro  na Pwani , alisema mkutano huo hufanyika  kwa mujibu wa sheria.

“ Ni muhimu watumishi  kuelewa  nini maana ya mkutano wa Baraza la Wafanyakazi  kwa kuwa inasaidia  pande zote mbili  za mwajiriwa na mwajiri   kuboresha mazingira  ya kazi  ya taasisi husika na kuleta ufanisi na tija, “ alisema Mhe. Jaji Mutungi.

Mhe. Mutungi, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa mkutano huo, aliongeza kwamba watumishi   hao, wanapaswa kueleza mambo yanayojadiliwa katika mkutano huo, kwa watumishi wengine ili waweze kufahamu malengo yake.

Kwa upande wake, Mwakilishi  wa Mkurugenzi  wa Elimu na Ushirikishwaji  kutoka Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Deus Mchelela  aliwataka  watumishi hao, kufahamu sheria, taratibu, kanuni na miongozo mingine  mahali pa kazi  na kuzizingatia ili waweze kufanyakazi  kwa weledi.

Mchelela alisisitiza kuwepo   kwa  ushirikiano wa kutosha kati ya mwajiri na viongozi wa baraza la wafanyakazi, ikiwemo kutoa taarifa zitakazoweza  kutekeleza  majukumu ya pande hizo mbili  ili kuimarisha mahusiano mema sehemu za kazi.

“Majukumu ya Mwajiri na Mfanyakazi yakitekelezwa vema huimarisha mahusiano mema mahali pa kazi hivyo hurahisisha au kuwezesha kufikiwa kwa malengo yaliyowekwa katika taasisi na mfanyakazi binafsi,” alisema.

Aliongeza kuwa mwajiriwa anapaswa kujielimisha zaidi ili kufahamu kazi yake vema hali itakayochangia kuongezeka kwa ufanisi na tija.

Naye mmoja wa wajumbe wa baraza hilo, Ibrahim Kelenge, aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuboresha majengo mbalimbali, huku akiwataka wajumbe wanaotoka maeneo ambayo miundombinu haijaboreshwa kuvuta subira.  

Mkutano huo wa siku moja umehudhuriwa na wajumbe wapatao 71 kutoka kanda ya Dar es Salaam.



Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam Mhe Beatrice Mutungi akifafanua jambo wakati akifunga mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.




Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama kanda ya Dar es Salaam ambaye pia ni Karani Mkuu Mahakama ya Hakimu Mkazi, Bi. Nise Mwasalemba akisoma maazimio yaliyoazimiwa katika mkutano huo.
Mtendaji wa Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam Bw. Gaston Kanyairita akijadiliana jambo na Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam Mhe. Joachim Tiganga wakati Mkutano huo ukiendelea.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kilosa Mhe. Timoth Lyon akichangia mada wakati mkutano huo ukiendelea.
Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Gaston Kanyairita akifafanua jambo wakati Mkutano huo ukiendelea, kushoto kwake (aliyekaa) ni Jaji Mfawidhi Mhakama Kuu kanda ya Dar es Salaam na mwenyekiti wa Mkutano huo Mhe. Beatrice Mutungi.
Katibu wa TUGHE mkoa wa Dar es Salaam Bi. Tabu Mambo akifafanua jambo wakati mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam ukiendelea.
Sehemu ya wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wakiwa katika mkutano huo
Katibu wa TUGHE Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam akiwagawia fomu za kujiunga na chama hicho wajumbe waliohudhuria mkutano huo leo jiji Dar es Salaam.
Naibu Msajili na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mhe. Kelvin Mhina akitoa neno la shukurani mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama kanda ya Dar es Salaam uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.


Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam Mhe. Beatrice Mutungi akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafanya kazi la Mahakama ya Tanzania, mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa baraza hilo uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano uliopo ndani ya jengo la Golden Jubilee Jijini Dar es Salaam, wa pili kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu   kanda ya Dar es Salaam Bw.Gaston Kanyairita, wa kwanza kulia ni Naibu Msajili na Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mhe.Kelvin Mhina, wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam Mhe. Joachim Tiganga, wa pili kushoto ni Katibu wa Baraza hilo na Karani Mkuu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Bi. Nise Mwasalemba.

(Picha na Dennis Buyekwa).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni