Ijumaa, 16 Agosti 2019

WASAIDIZI WAPYA WA SHERIA WA MAJAJI WAPATIWA ‘ABC’ ZA UTENDAJI KAZI

Jumla ya Wasaidizi wa Sheria 21 wa  Majaji wa Mahakama  ya Rufani (T) walioteuliwa hivi karibuni wamepatiwa utangulizi wa masuala muhimu ya kuzingatia katika ufanyaji kazi kwenye Mahakama hiyo.

Akizungumza na Maafisa hao mapema Agosti 15, 2019 katika Ukumbi ya Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam, Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati amewaasa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Mahakama imewaamini, hivyo basi ni vyema mkafanye kazi kwa uadilifu na unyenyekevu,” alieleza Msajili Mkuu.

Mbali na masuala hayo, Mhe. Revocati aliongeza kwa kuwataka Maafisa hao kutojihusisha na vitendo vya upokeaji wa rushwa wanapotekeleza majukumu yao.
“Siku hizi hakuna rushwa isiyojulikana pindi unapojihusisha katika vitendo hivi utajulikana tu, hivyo ni vyema kutojihusisha ili kuwa salama,” alisisitiza Mhe. Revocati.

Wasaidizi hao wa Sheria ambao kwa taaluma ni Mahakimu wameteuliwa kutoka Mahakama mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuwasaidia Waheshimiwa Majaji katika kufanya tafiti ambazo zitawawezesha katika utoaji wa maamuzi ya rufaa mbalimbali.


Kabla ya kuanza kazi rasmi Maafisa hao watapatiwa Mafunzo elekezi yatakayowawezesha kuwapa kwa kina misingi ya ufanyaji kazi katika Mahakama hiyo.
 Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati (katikati) akizungumza na Wasaidizi wapya wa Sheria wa Majaji wa Mahakama ya Rufani (T) (hawapo pichani), wa pili kushoto ni Naibu Msajili Mwandamizi-Mahakama ya Rufani, Mhe. Elizabeth Mkwizu, wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo-Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu, wa kwanza kulia ni Afisa Utumishi/Msaidizi wa Mtendaji-Mahakama ya Rufani, Bi. Vivienne Kishimbo na wa pili kulia ni Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Upendo Ngitiri. 
 Pichani ni Wasaidizi wa Sheria wapya wakimsikiliza Mhe. Msajili Mkuu (hayupo pichani).

Naibu Msajili Mwandamizi-Mahakama ya Rufani, Mhe. Elizabeth Mkwizu (katikati) akizungumza na Maafisa hao (hawapo pichani).
 

Mhe Mkwizu akiwaeleza jambo alipokuwa akiwapitisha katika Ofisi mbalimbali za Mahakama ya Rufani.
Wakionyeshwa Ofisi ya Mapokezi ya Mahakama ya Rufani.
 



Picha ya pamoja.

(Habari na picha na Mary Gwera, Mahakama)






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni