Na
Lydia Churi- Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Mahakimu Wakazi walioteuliwa kuwa
Mahakimu Wafawidhi wa Mikoa kuzingatia utawala bora wanapotekeleza majukumu yao
ili haki iweze kupatikana kwa wakati.
Akizungumza katika hafla
ya kuwapa Mahakimu hao Mamlaka ya kusimamia Mahakama za Mikoa (Instrument) leo
jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu alisema ili kutekeleza nguzo ya pili ya Mpango
Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania, utawala bora na uongozi bora
ni muhimu katika kufanikisha upatikanaji wa haki kwa wakati.
Alisema endapo Mahakimu
hao watazingatia utawala bora na uongozi bora, nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati
wa Mahakama ambayo ni kujenga imani ya jamii kwa Mahakama na ushirikishwaji wa
wadau katika shughuli za Mahakaman pia itafanikiwa.
“Uongozi kwangu ni jambo
muhimu sana, bila ya kuwa na kiongozi mwenye kuzingatia utawala bora mambo
mengine yote hayawezi kuwa vizuri. Unaweza kuwa na sheria nzuri, taratibu nzuri
na bajeti ya kutosha lakini usipokuwa na uongozi bora hayo yote
hayatawezekana,” alisema.
Aidha, Jaji Mkuu
amewataka Mahakimu hao kutambua kuwa Mahakama inaongozwa kwa Sheria namba 4 ya
mwaka 2011 ambayo imetoa mgawanyo wa wazi kati ya shughuli za Mahakama na zile
za kiutawala hivyo hakutakuwa na sababu ya kuwepo kwa migongano yeyote kwa kuwa
sheria imepambanua kazi za Mahakimu ni zipi na za kiutawala ni zipi.
Aliwataka Mahakimu hao
kutokutumia mamlaka waliyopewa kama silaha ya kutokufanya kazi na kugawa kazi
kwa wengine, kujenga uhasama miongoni mwa watumishi na kuwagawa watumishi
badala yake waheshimu watumishi wote kwa kuwa kila mtumishi ana nafasi yake ndani
ya Mhimili wa Mahakama.
Naye Kaimu Jaji Kiongozi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Benhajj Masoud amewataka Mahakimu hao
kushughulikia malalamiko ya wananchi kwa kuangalia namna ya kuyapunguza ama
kuyaondoa kabisa.
Mhe. Masoud pia
amewashauri Mahakimu hao kuimarisha uhusiano kati ya Mahakama na Taasisi
nyingine pasipo kuingilia uhuru wa Mahakama na kuongoza katika matumizi ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha utendaji kazi wa
Mahakama.
Jumla ya Mahakimu wakazi wanne
wameteuliwa kuwa Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Mikoa. Mahakimu hao pamoja
na Mikoa wanayoenda kwenye mabano ni Mhe. Janet Elias Masesa (Shinyanya), Mhe. Zawadi
David Laizer (Mbeya), Mhe. Obadia Festo Bwegoge (Geita) na Mhe. Lugano Rachel
Kasebele (Mtwara).
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisaini hati kabla ya kuwakabidhi Mahakimu Wakazi Wafawidhi wateule ambao leo aliwapa mamlaka ya kusimamia Mahakama za Hakimu Mkazi.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimkabidhi 'instrument' Hakimu Mkazi Mfawidhi mpya wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga Mhe. Janet Elias Masesa.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimkabidhi 'instrument' Hakimu Mkazi Mfawidhi mpya wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi David Laizer.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimkabidhi 'instrument' Hakimu Mkazi Mfawidhi mpya wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara Mhe. Lugano Rachel Kasebele. |
Waheshimiwa Mahakimu Wakazi Wafawidhi wapya wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipokuwa akizungumza nao baada ya kuwakabidhi Instrument.Wa kwanza kushoto ni Mhe. Lugano Rachel Kasebele akifuatiwa na Mhe. Zawadi David Laizer, Mhe. Janet Elias Masesa na Mhe. Obadia Festo Bwegoge.
Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Benhajj Masoud (wa kwanza kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mashauri Mhe. Eva Nkya, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bwn. Samson Mashalla (wa kwanza kushoto) na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Bwn. Beatus wakiwa kwenye hafla hiyo iliyofanyika ofisini kwa Mhe. Jaji Mkuu leo.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu Wakazi wafawidhi wapya mara baada ya kuwakabidhi instrument.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni