Na
Lydia Churi-Mahakama, Serengeti
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amesema Mahakama
ya Tanzania haitarudi nyuma katika matumizi ya teknolojia ya habari na
mawasiliano (Tehama) hivyo amewataka watumishi wa Mahakama kujifunza ili waweze
kutoa huduma bora na kwa wakati.
Akizungumza
na watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Serengeti akiwa katika ziara yake ya
kikazi Mkoani Mara, Jaji Kiongozi amesema hivi sasa Mahakama iko kwenye
matumizi ya Tehama katika kurahisisha upatikanaji wa Haki na kutoa huduma bora
na za haraka kwa wananchi.
Amesema
Mahakama inayo mifumo mbalimbali inayorahisisha upatikanaji wa haki na baadhi
ya mifumo hiyo ni ule wa kusikiliza mashauri kwa njia ya video (Video
Conferencing), mfumo wa kuwatambua Mawakili (TAMS- Tanzania Advocates
Management System), na mfumo wa kusajili mashauri (JSDS ll (Judicial Statistics
Dashboard System).
Jaji
Kiongozi amewataka watumishi wa Mahakama kuwa wepesi katika kujifunza mifumo ya
Mahakama na pia kuhakikisha wanapata taarifa mbalimbali za shughuli za Mahakama
kupitia mifumo mingine ya Mahakama ikiwemo Tovuti, Blog, Twitter na Facebook.
“Mahakama
haitarudi nyuma kwenye suala la matumizi ya Tehama hivyo muwe wepesi kujifunza
na kuliona ni jambo la kawaida kabisa”, alisema Mhe. Dkt. Feleshi.
Awali
akizungumza na Mkuu wa wilaya ya Serengeti Bwn. Nurdin Babu alipomtembelea
ofisini kwake, Jaji Kiongozi alisema Mahakama inaendelea kuboresha huduma zake na jitihada zinafanyika
kuhakikisha inaboresha upatikanaji wa haki kwa kusogeza huduma karibu zaidi na
wananchi.
Alisema
kupitia Mpango wa ujenzi wa majengo yake unaendelea maeneo mbalimbali nchini,
Mahakama pia inao mpango wa kujenga jengo la Mahakama ya wilaya ya Serengeti
kama ilivyo kwa wilaya nyingine nchini.
Aidha,
Jaji Kiongozi ameliomba jeshi la Polisi kumaliza upelelezi kwenye kesi
mbalimbali mapema kwa kuwa kesi nyingi zinazochelewa kumalizika mahakamani ni
zile ambazo upelelezi wake huchelewa kukamilika pamoja na zile zinazosubiri
kibali cha Mwendesha Mashtaka na ambazo zinasubiri mashahidi.
Akizungumzia
kesi zinazohusu mimba za utotoni, Jaji Kiongozi ameshauri matumizi ya kipimo
cha DNA ili kesi hizo zisichukue muda mrefu kumalizika na kuahidi Mahakama kutoa uzito unaostahili
katika kesi hizo.
Naye
Mkuu wa wilaya ya Serengeti Bwn. Nurdin Babu alisema katika wilaya yake,
Serikali inapata ushirikiano mkubwa kutoka Mahakama ya Tanzania na kuiomba
Mahakama kuendeleza ushirikiano huo ili wananchi waweze kupata huduma bora.
Alisema
ofisi yake inaishukuru Mahakama kwa kukamilisha ujenzi wa jengo la Mahakama ya
Mwanzo Robonda ambalo awali lilianza kujengwa kwa nguvu za wananchi na baadaye
Mahakama ilikamilisha jengo hilo ambalo hivi sasa linatumika.
Alisema
wilaya ya Serengeti inakabiliwa na changamoto ya kuwa na kesi nyingi na hasa
zinazohusu nyara za Serikali pamoja na mimba za utotoni kwa watoto wa kike
wanaosoma shule za msingi pamoja na sekondari wilayani humo. Alisema kati ya
mwezi Januari na Septemba 2019 jumla ya wasichana 13 wenye umri wa chini ya
miaka 18 walipata mimba wakiwa mashuleni.
Aidha,
Mkuu huyo wa wilaya alielezea changamoto ya gereza la wilaya ya Serengeti ambapo
alisema ni dogo ukilinganisha na idadi ya mahabusu waliopo. Gereza hilo lina uwezo
wa kuhifadhi mahabusi 216 lakini hivi sasa kuna mahabusu 416 ambao wengi
wanatokana na kesi zinazohusu nyara za serikali.
Jaji
Kiongozi anaendelea na ziara ya kikazi katika wilaya ya Tarime na baadaye
Musoma ambapo atakagua utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Mahakama.
Watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Serengeti wakimsikiliza Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi
alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi wilaya ya Serengeti.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akikagua vitabu vinavyotumika kusajili Mashauri (Rejista) katika Mahakama ya wilaya ya Serengeti.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akikagua jengo la Mahakama ya wilaya ya Serengeti linalofanyiwa ukarabati. Kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Mhe. Ismail Ngaile.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akizungumza na watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Serengeti. Kushoto ni
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Musoma Mhe. John Kahyoza na kulia ni Naibu Msaji wa Kanda hiyo Mhe. Mary Moyo.
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi
(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu wa wilaya ya Serengeti pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Musoma. Kushoto waliokaa ni
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Musoma Mhe. John Kahyoza.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Musoma Mhe. John Kahyoza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni