Na Aziza Muhali- (SJMC)
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, inaendelea kusikiliza
kesi 3,372 zilizosajiliwa Mahakamani hapo kwa sasa, zikiwamo za madai, jinai na
ardhi.
Hayo yamesemwa na Naibu Msajili Mfawidhi, Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Joachim Tiganga, wakati akitoa elimu kwa umma
kuhusu utoaji wa huduma zinazotolewa na mahakama hiyo, uliofanyika leo, Oktoba 2, mwaka huu katika ukumbi wa Mahakama Kuu, uliopo jijini Dar es Salaam.
Mhe. Tiganga
alisema lengo la kutoa elimu hiyo
kwa wananchi ni kueleza huduma zinazotolewa
na mahakama hiyo pia kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwa wateja wao.
Akifafanua kuhusu kesi hizo, alisema kesi zinazoripotiwa
kwa wingi ni kesi za madai ya kawaida ambazo ni 2,169 zikifuatiwa na kesi za
jinai 789, wakati kesi za ardhi ni 354.
“Hivyo kutokana na idadi hiyo ya kesi, jaji mmoja
anasikiliza kesi zipatazo 450 kwa mwaka badala ya kesi 220 kutokana na kuwepo
kwa idadi ndogo ya majaji” alisema.
Aliongeza kuwa Mahakama hiyo ina jumla ya majaji saba,
wakati idadi kamili inayohitajika ni 15, hivyo ina upungufu wa majaji 8.
Akizungumzia kuhusu ukataji rufaa, ambapo baadhi ya
wananchi walitaka kufahamu juu ya utaratibu wake,ambao ni Farida Mwalwaka mkazi
wa Toangoma na Ally Idd mkazi wa
Majimatitu, jijini Dar es Salaam, alisema kwamba mahakama huwawezesha wateja wake kukata rufaa kwa
kuwapatia nakala za kumbukumbu zote za kesi.
Aidha Tiganga aliwataka wananchi wenye malalamiko kuhusu
uendeshwaji wa kesi mbalimbali kufika
katika dawati la malalamiko ambalo hufanyika siku ya Jumanne na Alhamisi kila
wiki.
Kwa upande wake Hakimu Mhe. Joyce Karata, amewataka
wananchi kuwa makini wakati wa utaratibu wa ukataji wa rufaa ambapo amesema
kuwa rufaa inatakiwa kukatwa ndani ya muda, ili kuondoa usumbufu wa upatikanaji
wa nyaraka.
Naibu Msajili Mfawidhi,
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Joachim Tiganga akitoa elimu kwa umma
kuhusu huduma zinazotolewa na mahakama hiyo kwa wananchi.Kushoto ni Hakimu Mhe. Joyce Karatu.
Baadhi ya wananchi
wakisiliza elimu iliyokuwa ikitolewa na Naibu Msajili Mfawidhi huyo.
|
Mzee Ally Iddy (katikati) akiuliza jambo kuhusu taratibu za ukataji wa rufaa. |
Bi. Farida Mwalwaka (aliyevaa
ushungi) akiuliza jambo kuhusu masuala ya hukumu.
|
(Picha na Magreth
Kinabo)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni