Na
Lydia Churi-Mahakama
Taasisi ya Usuluhishi
Tanzania (The Tanzania Institute of Arbitrators) imeiomba Mahakama ya Tanzania kusaidia
katika mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Usuluhishi ya mwaka 1931 (The Tanzania
Arbitration Act, 1931) kwa kuwa sheria hiyo hivi sasa imepitwa na wakati.
Sheria ya Usuluhishi ya
mwaka 1931 ilifanyiwa marekebisho (Amendment) mara moja tangu Tanzania ipate
Uhuru wake ambapo marekebisho hayo yalifanyika mwaka 1971.
Mwenyekiti wa Taasisi
hiyo Gabriel Malata alitoa ombi hilo leo wakati ujumbe kutoka Taasisi hiyo
ulipomtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ofisini
kwake kwa lengo la kujenga mahusiano ya kiutendaji kati yake na Mahakama ya
Tanzania na pia kutambulisha uongozi mpya wa Taasisi hiyo.
Akizungumzia mchakato wa
mabadiliko ya Sheria ya Usuluhishi, Bwana Malata aliiomba Mahakama
kuishirikisha Taasisi hiyo kwa karibu katika mchakato wa mabadiliko ya Sheria
ya Usuluhishi na hususan katika hatua ya utengenezaji wa kanuni.
Alisema Taasisi ya
Usuluhishi Tanzania iko tayari kutoa maoni na mapendekezo pindi hatua hiyo
itakapofikiwa. Aliongeza kuwa hivi sasa Taasisi hiyo imejikita katika kutoa
Elimu husika katika Shule ya Sheria (Law School of Tanzania) ambapo wanafanya
vipindi ili waweze kupata Wasuluhishi bora hapo baadaye.
Mwenyekiti huyo alisema
Taasisi yake inao mfumo unaowatambua Wasuluhishi hai na hivyo ameiomba Mahakama
kuishirikisha ili wapatikane wasuluhishi hai. Sheria ya Tanzania inaruhusu
kuteua Wasuluhishi.
Kwa Upande wake, Jaji
Mkuu wa Tanzania amesema Mahakama iko tayari kurekebisha Kanuni za Usuluhishi
pale inapobidi kufanya hivyo ili Tasnia ya usuluhishi ifanye kazi vizuri na
kuwasaidia wananchi kwa haraka.
Alisema suala la
usuluhishi ni muhimu kwa Mahakama ya Tanzania kwa kuwa litasaidia kupunguza idadi
ya kesi mahakamani.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, utafiti
unaonyesha kuwa suala la usuluhishi wa migogoro nje ya Mahakama linaweza
kufanyika katika ngazi zote za Mahakama kuanzia Mahakama za Mwanzo mpaka
Mahakama ya juu.
Aidha, Jaji Mkuu ameishauri
Taasisi ya Usuluhishi Tanzania kuhakikisha inatoa zaidi elimu juu ya masuala ya
usuluhishi kwa kuwa wananchi wengi bado hawana uelewa wa masuala hayo.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akizungumza na wajumbe wa Taasisi ya Usuluhishi Tanzania ( Tanzania Institute of
Arbitrators) waliofika ofisini kwake leo jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Usuluhishi Tanzania, Gabriel Malata akizungumza
jambo na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.
Prof. Ibrahim Hamis Juma(hayupo pichani) mara baada ya kutembelea ofisini
kwake leo.
|
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akizungumza na wajumbe wa Taasisi ya Usuluhishi Tanzania( Tanzania Institute of
Arbitrators) walipofika ofisini kwake.
Mjumbe kutoka Taasisi ya Usuluhishi Tanzania, Frank Mwalongo akizungumza jambo wakati wa mazungumzo hayo.
|
Mjumbe wa kutoka Taasisi ya Usuluhishi Tanzania, Larissa Leach (wa pili kulia)akizungumza
jambo wakati wa mazungumzo hayo.
|
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisisitiza jambo.
|
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, akipokea nyaraka kutoka kwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Usuluhishi Tanzania, Gabriel Malata (kulia).
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni