Alhamisi, 10 Oktoba 2019

MAHAKAMA YA RUFANI YAENDELEA NA USIKILIZAJI WA MASHAURI KWA ‘VIDEO CONFERENCE’


Na Mary Gwera, Mahakama

Ikiwa ni siku ya pili ya ukilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao ‘Video Conference’ Mahakama ya Rufani (T) leo Oktoba 10, mwaka huu imesikiliza jumla  ya mashauri ya maombi tisa (9).

Kwa mujibu wa Naibu Msajili, Mahakama ya Rufani, Mhe. Amir Msumi  aliyekuwa katika Ukumbi namba moja (1) wa Mahakama Kuu akiratibu usikilizaji wa mashauri kupitia mfumo huo alisema kuwa, Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Rehema Mkuye amesikiliza jumla ya mashauri ya maombi matatu (3).

“Mashauri yaliyopanga kusikilizwa leo kati ya hapa (Dar es Salaam) na Tabora ni matano (5) mbele ya Wahe. Majaji wawili ambao ni Mhe. Jaji Mkuye na Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi,” alieleza Mhe. Msumi.

Naibu Msajili huyo alisema kuwa Mhe. Jaji Mkuye alisikiliza mashauri ya Maombi ya Jinai ‘Criminal Applications’ ambayo ni kati ya Sayi Mafizi dhidi ya Jamhuri namba. 28/11/2017, Inota Gishi dhidi ya Jamhuri namba 60/11/2017 na Jerome Ibrahim dhidi  ya Jamhuri namba. 69/11/2018.

Aidha; Mhe. Msumi alisema kuwa mashauri yote hayo yamesikilizwa na yanasubiri kutolewa maamuzi na kuongeza kuwa mashauri yaliyopangwa kusikilizwa na Mhe. Jaji Mwangesi hayakuweza kuendelea kutokana na waleta maombi ambao wapo katika magereza nje ya Tabora hawakuweza kusafirishwa kutoka magereza hayo kwenda Tabora.

Kwa upande wa Kituo cha Mafunzo Kisutu Dar es Salaam ambapo pia mashauri yalisikilizwa na upande wa Mwanza, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Bernard Mpepo amesema kuwa jumla ya Mashauri ya Maombi matano yamesikilizwa na kumalizika.

“Mashauri yote ya madai yaliyopangwa kusikilizwa leo yamesikilizwa na Wahe. Majaji na kati ya Mashauri hayo, mashauri matano (5) yamekwisha,” alieleza Mhe. Mpepo.

Hata hivyo Naibu Msajili huyo alisema kuwa shauri moja lenye namba. 191/01/2018 kati ya Victor Emmanuel &12 wengine dhidi ya Mkurugenzi wa Hospitali ya Bugando haikuweza kuendelea kutokana na mleta maombi namba. 7 kufariki hivyo kesi hiyo imeahirishwa na itaendelea mpaka atakapoteuliwa Msimamizi wa Mirathi.

Kwa upande wa Kituo hicho, mashauri yamesikilizwa na Wahe. Majaji watatu ambao ni Mhe. Jaji Jacobs Mwambegele, Mhe. Jaji Ferdinand Wambali na Mhe. Jaji Mwanaisha Kwariko.

Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (5) (2015/2016-2019/2020) inaendelea kuboresha huduma zake katika nyanja mbalimbali ikiwemo matumizi ya mfumo huo ‘Video Conference’ lengo likiwa ni kutoa haki sawa kwa wote na kwa wakati kama isemavyo dira yake.
 Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Rehema Mkuye akisikiliza kesi kwa njia ya mtandao ‘Video Conference’ katika ukumbi wa Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam mapema leo Oktoba 10, 2019.

 
Wakili wa Serikali, Mhe.Tumaini  Ochalo  akitoa maelezo yake katika kesi ya maombi ya jinai dhidi ya Jamhuri  kwa njia ya mtandao ‘Video Conference’ katika ukumbi wa Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam, akiwa mkoani Tabora leo.
Mleta maombi ya jinai dhidi ya Jamhuri Jerome Ibrahim (mwenye nguo nyeupe) akisikiliza kesi yake dhidi ya Jamhuri kwa njia ya mtandao ‘Video Conference’  akiwa mkoani Tabora leo.
Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Amir Msumi (katikati) akifuatilia kesi kwa njia ya mtandao ‘Video Conference’ katika ukumbi wa Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam. Kesi hiyo imesikilizwa wakati mleta maombi wa maombi ya jinai nyongeza  ya muda akiwa mkoani Tabora.

(Picha na Magreth Kinabo - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni