Ijumaa, 11 Oktoba 2019

SERIKALI MKOANI MARA YAOMBWA KUHAMASISHA WANANCHI KUJITOKEZA KUTOA USHAHIDI


Na Lydia Churi- Mahakama, Musoma
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ameiomba Serikali mkoani Mara kuwahamasisha wananchi kujitokeza kutoa ushahidi Mahakamani pale wanapohitajika hatua itakayosaidia kesi kumalizika kwa wakati. 

Akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adamu Malima, Jaji Kiongozi amesema hivi sasa kesi nyingi hazimaliziki kwa wakati kutokana na wadau wa Mahakama kutokukamilisha wajibu wao kwa wakati ikiwemo polisi kutokukamilisha upepelezi wa kesi mapema pamoja na mashahidi kukosekana Mahakamani.

“Hakimu yupo, na ukiangalia jalada utakuta kesi imeahirishwa mara nyingi kutokana na mashahidi kutofika mahakamani”, alisema Jaji Kiongozi.

Alisema Mahakama kwa upande wake itatoa ushirikiano mkubwa kwa wadau wake pamoja na Serikali ili wananchi wapate haki kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mlundikano wa kesi mahakamani unakwisha.   

Aidha, Jaji Kiongozi pia amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Mara kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi ambao hawaridhishwi na huduma zinazotolewa na Mahakama kutumia mifumo ya Mahakama iliyopo ili kufikisha malalamiko yao. 

Aliitaja mifumo hiyo kuwa ni pamoja na Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama za Mikoa zinazoongozwa na Wakuu wa Mikoa, Kamati za Maadili za Wilaya zinazoongozwa na Wakuu wa Wilaya pamoja na Kamati ya Maadili ya Majaji.  

Jaji Kiongozi pia amemuomba Mkuu huyo wa Mkoa kuwahimiza wakuu wa wilaya za Mkoa wa Mara kuzisimamia kikamilifu Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama hasa kupitia Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) pamoja na Makatibu Tawala wa Wilaya (DAS).

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adamu Malima ameahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa Mahakama ya Tanzania na kuahidi kuzisimamia kikamilifu Kamati za Maadili. Aliongeza kuwa yote ya dola inalo jukumu la kuwatumikia wananchi na kuwapatia huduma zilizo bora. 

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama mkoani Mara wakati akihitimisha ziara yake, Jaji Kiongozi amewataka watumishi hao kuikana rushwa na maadili yasiyofaa na badala yake wawe na maadili mema ndani na hata nje ya Mahakama.

Amewapongeza watumishi wasiojishirikisha na vitendo vya rushwa na kuwataka   kuwa makini na kujilinda wasije wakaingia kwenye vitendo hivyo ambavyo ni kinyume na maadili ya utumishi.

Aidha, aliwataka watumishi wa Mahakama kuwakanya na kuwarejesha kwenye mstari watumishi wenzao wanaojishirikisha na vitendo vya rushwa na maadili yasiyofaa badala ya kufurahia pindi wanapopata matatizo.

“Mahakama ni Taasisi kubwa hivyo watumishi wake hawana budi kuwa na upendo kati yao na endapo mtu anakosea aambiwe na kurekebishwa na siyo kusemwa pembeni, tulindane na kupendana sisi kwa sisi”, alisema  Jaji Kiongozi. 

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania amemaliza siaza ya siku tano ya kikazi katika Mkoa wa Mara ambapo alikagua shughuli za Mahakama katika wilaya za Bunda, Serengeti, Tarime na Musoma Mjini. Jaji Kiongozi pia alikagua jengo jipya la Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Musoma lilimalizika hivi karibuni.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adamu Malima (kulia)akisalimiana na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi alipowasili Ofisi ya Mkuu huyo wa Mkoa wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Mara.



 Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adamu Malima akimuelezea jambo Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi walipokuwa wakifanya mazungumzo kwenye Ofisi ya Mkuu huyo wa Mkoa .

 
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adamu Malima mara baada ya kuzungumza naye ofisini kwake. Kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. John Kahyoza na kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Anney.
  Baadhi ya Watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Musoma wakimsikiliza Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi(hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao.
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kanda ya Musoma.
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu wa Mahakama zilizopo kwenye Kanda ya Musoma mara baada ya kuzungumza na Watumishi. Wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. John Kahyoza na wa pili kulia ni Naibu Msajili wa Kanda hiyo Mhe. Mary Moyo. Wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa Mhe. Rahimu Mushi na wa kwanza kushoto ni Afisa Utumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Bwn. Jumanne Muna.
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama Kanda ya Musoma mara baada ya kuzungumza nao. Wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. John Kahyoza na wa pili kulia ni Naibu Msajili wa Kanda hiyo Mhe. Mary Moyo. Wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa Mhe. Rahimu Mushi na wa kwanza kushoto ni Afisa Utumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Bwn. Jumanne Muna.
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na Wazee washauri wa Mahakama ya Mwanzo Kukirango pamoja na watumishi wa Mahakama alipotembelea Mahakama hiyo.
ntumishi wa Mahakama Kanda ya Musoma mara baada ya kuzungumza nao.


 
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akikagua Rejista zinazotumika katika kusajili kesi alipokuwa akikagua Mahakama ya Mwanzo Nyashimo wilayani Busega mkoa wa Simiyu. 
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akisalimiana na Watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Nyashimo pamoja na wazee washauri wa Mahakama.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akisalimiana na Kiongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Busega alipowasili kwenye ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo. Mwenye kitenge katikati ni Mkuu wa wilaya ya Busega Mhe. Tano Seif Mwera.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni