Na
Mary Gwera, Mahakama
Jaji Kiongozi, Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewataka Wajumbe wa Kamati ya
utatu ya Mahakama ya Kazi (Tripatite Users Committee) kushirikiana kwa pamoja katika kushughulikia mashauri ya migogoro ya kazi.
Akiwasilisha hotuba kwa
niaba ya Mhe. Jaji Kiongozi katika ufunguzi rasmi wa Kikao cha Kamati ya Utatu kilichofanyika
katika Ukumbi wa Benki Kuu-Dar es Salaam, mapema Oktoba 11, 2019, Kaimu Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Dkt. Benhajj Masoud alisema
kuwa takwimu zinaonyesha kuwa mzigo bado ni mkubwa na inahitaji mchango wa wadau wote katika kuyashughulikia mashauri hayo.
“Kwa mwaka 2017, idadi
ya mashauri ya kazi yaliyofunguliwa ni 3414, yaliyosikilizwa ni 3135 na
yaliyobaki ni 3664, kwa mwaka 2018 idadi ya mashauri yaliyofunguliwa yalikuwa
1944, yaliyosikilizwa ni 2012 na yaliyobaki ni 2256 na kwa mwaka huu 2019
(Januari hadi Agosti) jumla ya mashauri 1889 yamefunguliwa, yaliyosikilizwa ni
1549 na yaliyobaki ni 2549,” alieleza Mhe. Jaji Kiongozi.
Hata hivyo;
katika hotuba yake, Mhe. Jaji Kiongozi alisema kuwa Mahakama inaendelea na
mikakati mbalimbali ya kutatua mlundikano wa mashauri mojawapo ikiwa ni Mhe Jaji Mkuu wa Tanzania kupitia Tangazo lake la Aprili 30, 2018 (Labour
Division Judges and Deputy Registrars Designation Notice).
“Kupitia
tangazo hili, Mhe. Jaji Mkuu aligatua mamlaka ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi
kwa Waheshimiwa Majaji na Naibu Wasajili wote kwenye Kanda zote kasoro Kanda ya
Dar es Salaam, kusikiliza mashauri ya kazi,” alifafanua Mhe. Jaji Kiongozi.
Hata
hivyo, Mhe. Mgeni rasmi aliwashukuru Wadau kwa mchango mkubwa wanaoendelea
kuipatia Mahakama ya Tanzania hususani Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi na kuwataka
kupitia kikao hicho kuja na mikakati zaidi itakayotatua changamoto mbalimbali
kuhusiana na mashauri hayo.
Aidha;
Mhe. Jaji Kiongozi aliwakumbusha Wajumbe hao kuwa jukumu lao kwa mujibu wa
Sheria ni kuweka mikakati itakayowezesha kusukuma mbele mashauri.
Naye
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi,Vijana, Ajira
na wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa alisema Serikali
inatambua majukumu mazito na mchango mkubwa wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi,
Tume ya Usuluhishi na Uamuzi na Wadau wote wa sheria katika utatuzi wa migogoro
ya kikazi.
“Serikali
inatambua pia kuwa majukumu yenu yana uhusiano wa moja kwa moja na ndoto ya
Serikali ya awamu ya tano kuelekea uchumi wa Viwanda kwani wateja wenu yaani
wafanyakazi na waajiri ndio wazalishaji wakuu wanaochangia ukuaji wa uchumi,”
alieleza Mhe. Ikupa.
Mhe.
Waziri huyo pia ameipongeza Mahakama kwa kujipima kupitia wadau wake,
kujitathmini namna jamii inavyoitazama na kupendekeza kufanyika kwa mafunzo kuhusu Sheria za kazi kwa Wahe. Majaji na Mahakimu.
Kikao
hicho cha siku moja (1) kimeshirikisha Wajumbe wa Kamati ya Utatu kutoka
Serikalini, Chama cha Waajiri na Shirikisho la vyama vya wafanyakazi pamoja na
wadau wengine wa Mahakama hiyo wakiwemo baadhi ya Majaji Wafawidhi kutoka Kanda
mbalimbali, Majaji Wastaafu wa Mahakama Kuu divisheni ya Kazi, Wanasheria na
wengineo.
Lengo
ni kutathmini kwa pamoja juu ya utendaji kazi wa Mahakama hiyo pamoja na
kuwekeana mikakati mingineyo itakayowezesha kukabiliana na changamoto
zinazojitokeza katika kazi ya uondoshaji wa mashauri ya migogoro ya kazi.
Kaimu Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Dkt.
Benhajj Shaban Masoud akiwasilisha hotuba ya ufunguzi kwa niaba ya Jaji
Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge,
Kazi,Vijana, Ajira na wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa
akiwasilisha hotuba yake kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo, Mhe. Jenista
Mhagama.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Sophia Wambura akitoa neno la
utangulizi katika kikao hicho, amewashukuru Wadau wa kikao hicho kushiriki
kikamilifu kwa ustawi wa Mahakama hiyo.
Baadhi ya Wageni waalikwa wakiwemo Wahe. Majaji na Maafisa
wengine wa Mahakama wakiwa katika kikao hicho.
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama, kutoka Divisheni ya Kazi
wakifuatilia kikao hicho.
Washiriki wakifuatilia kinachoendelea katika kikao hicho.
Mwakilishi kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO)-Tanzania akitoa
neno.
Picha ya pamoja, (katikati) ni mgeni rasmi Kaimu Jaji Kiongozi,
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Dkt. Benhajj Masoud, wa tatu kulia ni
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge,
Kazi,Vijana, Ajira na wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa,
wa tatu kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Sophia
Wambura, wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, Mhe. Jaji
Zainabu Muruke, wa pili kushoto ni Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe.
Katarina Revocati pamoja na Wajumbe wanaounda Kamati ya Utatu.
Picha
ya pamoja (meza kuu) na baadhi ya Wahe. Majaji Wafawidhi (waliosimama)
walioshiriki katika kikao hicho.
Meza
kuu pamoja na baadhi ya Maafisa wa Mahakama walioshiriki katika kikao hicho.
Picha
ya pamoja na Wahe. Majaji wastaafu wa Mahakama Kuu-Divsheni ya Kazi
(waliosimama).
Picha
ya pamoja na Watumishi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi.
(Picha
na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni