Na Magreth Kinabo-Mahakama
Mahakama ya Rufani Tanzania, imesema kwamba shauri la maombi jinai la mapitio ya nyongeza
ya muda, haliwezi kuendelea kusikilizwa kwa sababu linahitaji na jopo la majaji
watatu.
Uamuzi huo ulitolewa leo Jaji wa Mahakama ya
Rufani Tanzania, Mhe. Rehema Kerefu wakati akisikiliza shauri la maombi ya jinai
ya mapitio ya muda linalomkabili Job Mlama na wenzake wawili, dhidi ya Jamhuri,ambayo
iliwasilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidambo wote wakiwa
mkoani mwanza kwa njia ‘Video conference’.
Shauri hilo liliendeshwa huku wakili huyo na
wahusika, wakiwa mkoani Mwanza, na Jaji Kerefu katika Kituo cha Habari na Mafunzo
kilichopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Katika shauri hilo, mleta maombi hayo, Mlama aliomba
mahakama hiyo isikilize maombi ya mapito ya nyongeza ya muda kwa njia ya ‘Video
Conference’.
Jaji Kerefu alitoa uamuzi huo, baada ya kuuliza
upande wa Jamhuri kuwa uko tayari kuendelea na maombi hayo ya mapitio ya muda,
ambapo ulikubali, ndipo alipotoa uamuzi huo, wa shauri kuwa linapaswa kusikilizwa na jopo la majaji watatu kama sheria inavyosema.
Katika shauri lingine la maombi ya jinai ya mapitio
ya nyongeza ya muda linalomkabili, Weisiko Ruchere dhidi ya Jamhuri, ambaye
aliwakilishwa na wakili Geofrey Kanje na kusikilizwa na Jaji Kerefu.
Wakili Kanje aliomba mahakama hiyo iongeze muda wa
maombi hayo kwa sababu ya mleta maombi kutokuwa na msaada wa kisheria.
Akijibu hoja hiyo Wakili wa Serikali Mwandamizi,Anjelina
Nchalla alisema hakuna sababu za msingi alizozitoa mleta maombi zilizosababisha
achelewe kuleta maombi hayo kwa kuwa ni mwaka moja na nusu tangu yalipotupiliwa
mbali Novemba 29, mwaka 2017.
Akisikiliza maombi hayo Jaji Kerefu alisema atatoa
uamuzi na wahusika watataarifiwa baadaye.
Shauri lingine lililosikilizwa na Mhe. Jaji Ignas
Kitusi, ambapo mleta maombi ya jinai ya mapitio ya nyongeza ya muda, Reuben
Juma dhidi ya Jamhuri iliyowakilishwa na Wakili wa Serikali Maryyasintha Lazaro
na Wakili wa serikali Mwanahawa Shangale, ambao walipinga ombi hilo.
Katika shauri hilo, Juma aliomba mahakama hiyo
isitilie maanani pingamizi la mawakili hao kwa sababu limekuja nje ya muda na pia
alikosa msaada wa kisheria wa kuwasilisha ombi lake, ndani ya wakati.
Huku Wakili huyo Mwandamizi aliomba mahakama hiyo itupilie
mbali maombi hayo kwa kuwa kukosa msaada wa kisheria sio sababu ya msingi na
maombi hayo hajazingatia matakwa ya kisheria.
Akijibu hoja ya Wakili huyo Mwandamizi, Jaji Kitusi
alisema ni takwa la kisheria la mleta maombi.
Akisikiliza hoja hizo,Jaji Kitusi alisema ataenda
kuandaa uamuzi na wahusika watataarifiwa baadaye.
Shauri lingne la madai lililosikilizwa na Jaji huyo,
la mleta maombi ya nyongeza ya muda ambaye ni Geita Gold Mine Limited,
aliyewakilishwa na Wakili Faustine Mwalongo dhidi ya Truway Muneth na wenzake
waliowasilishwa na wakili Mwita Emmanuel, ambaye aliomba mahakama isikubali
maombi hayo kwa sababu yalikuwa nje ya muda na yalipaswa kuandaliwa ndani ya
siku moja.
Wakati Mwalongo aliomba maombi hayo yakubaliwe na
mahakama hiyo kwa kuwa yako ndani ya
muda wa siku tatu, yakiwa yanaandaliwa na kuwasilishwa mahakamani, hivyo hakuna
nyaraka inayosema maombi yaandaliwe ndani ya siku moja.
Katika hatua nyingine Jaji mwingine wa mahakama hiyo,
Mhe. Dkt. Mary Levira alihairisha shauri la maombi ya nyongeza ya muda la
Mugeta Manyama dhidi ya Jamhuri kwa sababu mleta maombi haifahamiki yuko gereza
gani.
Aidha Dkt. Levira pia alisikiliza shauri la maombi
ya mapitio ya nyongeza ya muda la Kafuba Mwangulindi dhidi ya Jamhuri na
litatolewa maamuzi baadaye.
Kwa upande wa mkoa wa Bukoba Mahakama hiyo
imesikiliza mashauri sita kwa njia hiyo pia, ambapo mashauri matano ni ya
maombi ya jinai ya nyongeza ya muda na moja la maombi ya madai ya nyongeza ya
muda. Mashauri hayo yalisikilizwa na majaji watatu ambapo kila mmoja
alisikiliza mashauri mawili.
Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Sylvester Kainda, alisema majaji waliosikiliza mashauri hayo ni Mhe. Winfrida
Korosso, Mhe. Barke Sehel na Mhe. Lugano Mwandambo. Mashauri hayo baadhi yamesikilizwa na kumalizika, mengine
maamuzi yatatolewa baadaye.
Mahakama hiyo itaendelea na mashauri mengine maombi
ya jinai na madai kesho, Oktoba 16 kwa njia ya ‘Video Conference’ yaliyoko
masjala ya Mbeya na Mwanza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni