Na Waandishi, Mahakama
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga kwa kazi nzuri aliyofanya katika Mahakama ya Tanzania.
Akimuapisha Mtendaji Mkuu mpya wa
Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru leo Oktoba 20, 2019 Ikulu jijini
Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema Kattanga ana rekodi nzuri ya utendaji kazi
tangu akiwa RAS, Katibu Mkuu-TAMISEMI na
baadaye Mtendaji Mkuu wa Mahakama.
Mhe. Rais aliendelea kusema kuwa Bw. Kattanga
amefanya kazi nzuri kwani kuna maboresho mengi yaliyofanyika ndani ya Mahakama kipindi cha uongozi wake chini ya Mhe. Jaji Mkuu.
"Nampongeza sana Kattanga na
nimeamua nimtoe Mahakama ili akanisaidie kazi nchi fulani kwani naamini
ataniwakilisha ipasavyo, ninakushukuru kwa utendaji wako mzuri", alieleza
Rais Magufuli.
Akimzungumzia Mtendaji Mkuu mpya wa
Mahakama, Mhe. Rais alimtaka kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na hasa
maboresho ya huduma za kimahakama yanayofanywa kupitia mradi wa Benki ya Dunia.
Aidha alimtaka Bw. Kabunduguru
kushirikiana na Watendaji wengine wa Mahakama ya Tanzania katika kutekeleza
programu ya Benki ya Dunia ambayo inaendelea vizuri hivi Sasa.
"Kazi hii ni utume hivyo basi
nendeni mkawatumikie vyema wananchi kwa uaminifu," aliongeza Mhe. Rais.
Jana Rais alifanya mabadiliko ndani
ya Mhimili wa Mahakama baada ya kumteua Bw. Kabunduguru kuwa Mtendaji Mkuu wa
Mahakama akichukua nafasi ya Bw. Hussein Kattanga aliyeteuliwa kuwa Balozi.
Hafla ya kuapishwa kwa Mtendaji Mkuu
wa Mahakama pamoja na viongozi wengine ilihudhuriwa na Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Jaji Mkuu wa
Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi, Majaji, Viongozi wa Ulinzi na Usalama
pamoja na Watendaji wengine wa Mahakama ya Tanzania.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Bw.Mathias
Bazi Kabunduguru kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania katika hafla fupi
iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam leo Oktoba 20, 2019.
Viongozi
mbalimbali walioapishwa wakila kiapo cha Maadili ya Viongozi wa Umma mara baada
ya kuapishwa Ikulu jijini Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Bazi Kabunduguru, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI,
Bw. Gerald Godfrey Mweli pamoja na Balozi Ali Sakila Bujiku.
Viongozi
mbalimbali walioapishwa wakisaini Hati ya kiapo cha Maadili ya Viongozi wa Umma.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akizungumza mara baada ya kuwaapisha Viongozi mbalimbali Ikulu jijini Dar es
Salaam.
Viongozi
na Wageni mbalimbali waliohudhuria katika hafla hiyo fupi wakimsikiliza Mhe.
Rais alipozungumza mara baada ya kuapisha rasmi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha na Makamu wa Rais Samia Suluhu
Hassan, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John
Kijazi (wa pili kulia), Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Augustine Mahiga (wa tatu kulia), Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Bazi Kabunduguru (wa pili kushoto), Naibu
Katibu Mkuu TAMISEMI Gerald Godfrey Mweli (wa kwanza kushoto) pamoja na Balozi
Ali Sakila Bujiku wakwanza (kulia) mara baada ya uapisho Ikulu jijini Dar es
Salaam.
(Picha kwa hisani ya Ikulu)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni