Jumanne, 26 Novemba 2019

JAJI MKUU AWATAKA WADAU WA SHERIA KUTUMIA MAKTABA MTANDAO

Na Salum Tawani-Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania,Mhe.Prof. Ibrahimu Hamis Juma ametaka wadau wa sheria kuutumia Mfumo wa Maktaba Mtandao kwa ajili ya  kufanya tafiti za kisheria kwa  urahisi.

Akizungumza baada ya uwasilishaji wa Mfumo wa Maktaba Mtandao uliowasilishwa kwa Jaji Mkuu na Hakimu Mkazi, ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maktaba cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Kifungu Mrisho, Jaji Mkuu  alisema mfumo huo utawasaidia wadau hao kuendana na mabadiliko ya teknolojia.

“Badala ya kubeba mzigo wa vitabu na nyaraka zinginezo mfumo huu utarahisisha ufanyaji wa tafiti kirahisi kuendana na teknolojia,” alisema Jaji Mkuu.

Awali Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri, Mhe. Eva Nkya alisema kuwa mfumo huo utawezesha wadau wa sheria  kusoma vitabu na Majuzuu (Law Reports) kwa njia ya mtandao na hivyo kutatua suala la ubebaji wa vitabu na baadhi ya nyaraka kwani vyote vinapatikana katika mfumo huo.

Mhe. Nkya aliongeza kwamba kutakuwa na utaratibu wa kutambaza (Scanning) vitabu ambavyo hati miliki yake imeisha na vitabu vyenye hati miliki ambavyo vimenunuliwa na Mahakama  na kuna utaratibu wa kuvilinda (Protecting by Read Only) utafanyika kupitia wataalamu wetu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano  (TEHAMA).  

Kwa  upande wake Mhe. Kifungu Mrisho alisema kuwa mfumo huo utakuwa na jumla ya vitabu  27,607. 

Mfumo huo ulikamilika tangu Agosti 30, mwaka huu na juhudi mbalimbali zinafanyika  ili kuendelea  kuuwezesha kufanya kazi, ikiwa ni mojawapo ya maboresho ya Mahakama ya Tanzania.


 
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma(kulia) akizungumza jambo leo wakati wa uwasilishaji wa mfumo wa Maktaba Mtandao uliofanyika katika ofisi ya Jaji Mkuu, jijini Dar es Salaam.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akiuliza jambo leo kwa mwezeshaji wa mfumo wa Maktaba Mtandao.Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw.Mathias Kabunduguru.

Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, na Mkurugenzi  wa  Usimamizi wa Mashauri, Mhe. Eva Nkya  akifafanua jambo  wakati wa  uwasilishaji wa mfumo wa Maktaba Mtandao kwa Jaji Mkuu. Kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi. (Katikat)i ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru na Kulia ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru (kushoto) akifafanua jambo wakati wa uwasilishaji.

Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri, Mhe. Eva Nkya (kulia),  wa pili kushoto ni  Hakimu Mkazi, ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maktaba cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Kifungu Mrisho (wa pili kulia) ni  Afisa Habari, Salum Tawani na (wa kwanza kushoto) ni Afisa  Tehama, Israel Kamendu  wakifuatilia  mfumo wa Maktaba Mtandao unavyofanya  kazi.  

(Picha na Magreth Kinabo- Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni