Na Amina Ahmad- Tanga
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda
ya Tanga Mhe. Amiri Mruma amesema
Mahakama ya Mwanzo Mtae itafunguliwa haraka iwezekavyo ili kuweza kutatua changamoto
ya kutokuwepo kwa huduma hiyo katika eneo hilo.
Hayo yalisemwa na Mhe. Mruma
wakati alipofanya ziara ya kikazi Novemba 25, mwaka huu kwenye mahakama hiyo ili
kukagua ujenzi wa mahakama hiyo,utendaji kazi wa Mahakama ya Wilaya Lushoto, Mahakama ya
Mwanzo Mnazi na Mlalo na shughuli za gereza
la kilimo la Mng’aro.
Katika ziara hiyo Mhe. Jaji Mruma
alitembelea na kufanya ukaguzi katika Mahakama ya Wilaya ya Lushoto ambapo
alikagua usimikaji wa miundombinu ya huduma ya intaneti kupitia mkongo wa
Taifa, usajili wa mashauri kwenye mfumo wakuratibu na kusajili mashauri kwa
njia ya kielektroniki (JSDS 2) na ulipaji wa tozo na ada za kimahakama kupitia
mfumo wa malipo wa Serikali (GePG).
Mhe. Jaji Mruma aliridhishwa na utendaji wa
Mahakama ya Wilaya ya Lushoto chini ya Mhe. Japhet Manyama Hakimu Mkazi
Mfawidhi ambapo alitoa pongezi.
Akiwa wilayani humo, Mhe. Jaji
Mruma alipata fursa ya kukagua mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Mtae
ulioanza tarehe 29 Desemba 2018.
Kwa mujibu wa tathmini ya mshauri
elekezi, (QS) Yassin Khatibu alisema mradi huo umekamilika kwa asilimia
tisini na tano (95) % ambapo tayari mfumo
wa umeme umeshasimikwa na huduma ya maji safi imekamilika na maji yanapatikana
kwa wingi.
Kwa upande wake Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtae, Fredson Masuke ambaye alimweleza Jaji Mruma kuwa kuwepo wa matukio mengi ya kihalifu
yanayoripotiwa kituoni hapo, hali inayosababisha uhitaji mkubwa wa huduma za
Mahakama.
Jaji Mruma aliahidi kufunguliwa
mapema kwa Mahakama hiyo ili kesi zianze kusikilizwa na kutolewa maamuzi kwa
misingi ya kisheria.
Hivyo itasaidia kupunguza matukio
ya baadhi ya watu kujichukulia sheria mikononi,
pale wasiporidhishwa na maamuzi ya baraza la kata na wengine kukata
tamaa kupeleka kesi zao Mahakama ya Mwanzo Mnazi, Mlalo au Dochi kwa kukosa
fedha za kusafiria zaidi ya kilometa 60.
Jaji Mruma akiendelea
na ukaguzi.
|
Muonekano wa Jengo la
Mahakama ya Mwanzo ya Mtae.
|
(Picha na Amina Ahmad- Tanga)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni