Na.
Rajabu Singana, Mahakama Kuu Mbeya
Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amesema kwamba
Tanzania ina mgawanyo wa madaraka
na unaofuatwa vizuri tofauti na nchi nyingine.
Akizungumza leo Novemba
28, mwaka huu wakati alipotembelea Ofisi
za Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Waziri Mahiga alisema ametembea nchi mbalimbali na kujifunza
kwamba katika nchi yetu mgawanyo wa madaraka (separation of power) unafuatwa.
'Mgawanyo wa madaraka kwa mihimili ya dola, ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama upo na unafuatwa
vizuri ukilinganisha na nchi nyingine ambapo hata kuonekana haionekani kabisa
na kama ilikuwepo basi ilikufa,' alisema Waziri Mahiga.
Akizungumzia kuhusu kazi kubwa inayofanywa na
Wahe. Majaji ya kusikiliza mashauri ambapo kuna wakati wanalazimika kufanya
kazi hadi kwa zaidi ya saa 18 kwa siku ili kuweza kuwahudumia wananchi na
kufikia malengo ya kitaasisi, alisema anatambua mchango huo na kuwapongeza.
Pamoja na pongezi hizo,
Waziri Mahiga amewataka majaji hao, kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia
maadili na utendaji uliotukua kiasi kwamba ikitokea mtu ameulizwa haki ni nini?
katika kutoa majibu amchukue Jaji na kusema hii ndio maana ya haki.
Hivyo katika hilo amewashauri Wahe. Majaji
kuwa na maadili ya ziada na kuufanya Mhimili wa Mahakama kutekeleza majukumu
kwa viwango vya juu.
Vile vile Waziri Mahiga
amesema kupitia kuongezeka kwa watu na kukua kwa Sayansi na Teknolojia, nchi
yetu imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali zinazosababisha watu kubuni
njia nyingi za uhalifu.
Alisema
changamoto hizo zinasababisha kuwa na uhaba wa majaji kitendo
kinachowalazimu kuwa na makadirio ya kusikiliza mashauri mengi zaidi tofauti na mipango ya kitaasisi,
na kila mmoja kulazimika kufanya kazi kwa muda mrefu.
Naye Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Dkt. John Utamwa, alisema mikakati ambayo imekuwa ikitumiwa na Mahakama
Kuu Kanda ya Mbeya katika kuhakikisha mashauri yanaamuliwa kwa wakati na ubora
unaotakiwa ni uwepo wa miongozo mbalimbali juu ya utoaji huduma kwa
mfano kabla ya kufika siku 21 nakala za hukumu zinatakiwa kuwa tayari lakini
Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Nakala za Hukumu hutolewa ndani ya siku ambayo
hukumu hutolewa.
Aidha Waziri wa Sheria na
Katiba yupo katika ziara ya kikazi mkoani Mbeya, na ameambatana na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini
(DPP) Biswalo Mganga, ambapo walikagua magereza yote ya mkoa wa Mbeya na kutambua changamoto
mbalimbali zinazowakabili wafungwa na Mahabusu.
Katika ziara hiyo, Mganga amewafutia mashtaka jumla ya watuhumiwa 47.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akitembelea jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya leo. Kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe.Dkt. John Utamwa. |
Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya,
Mhe.Dkt. John Utamwa.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni