Na Magreth Kinabo na Innocent Kansha-
Mahakama
Bodi ya Udhamini wa Taarifa ya Majuzuu
ya Sheria leo imeanza kikao chake cha siku mbili cha kuchambua maamuzi ya Mahakama
Kuu na Mahakama ya Rufani Tanzania kwa ajili ya
kumaliza kuandaa Juzuu la Taarifa za
Sheria la mwaka 2018.
Aidha bodi hiyo pia itaandaa maamuzi kwa ajili ya Juzuu la Taarifa za
Sheria la mwaka 2019.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, kinachofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Sheria kwa Vitendo, iliyopo Barabara ya
Sam Nujoma, jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Jaji wa Mahakama ya
Rufani Tanzania, Mhe. Jacobs Mwambegele alisema kikao hicho ni cha mara ya
kwanza kufanyika katika kipindi cha mwaka huu.
‘Bodi imekutana ikiwa tayari imekwisha andaa Taarifa za Majuzuu ya Sheria ya Mwaka 2007 hadi Mwaka 2013 na kukabidhi Taarifa hizo katika uongozi wa juu wa Mahakama ili kuwezesha kupata Taarifa kamili katika nakala laini na ngumu,’ alisema Mhe. Mwambegele.
Aliongeza kuwa, tayari Bodi hiyo
imekamilisha kupitisha maamuzi kwa ajili ya vitabu vya Mwaka 2014 hadi Mwaka
2017.
Jaji Mwambegele alifafanua kuwa Bodi
hiyo, kwa sasa inafanya kazi zake kwa njia ya teknolojia zaidi kwa kushirikiana
na Idara ya Menenjimenti ya Mashauri ya Mahakama ya Tanzania, ambayo hupokea
maamuzi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani (Depository) katika nakala laini kila mwezi na kuishushia Bodi
ambayo huyachakata na kuyachambua maamuzi hayo ili kupata maamuzi ambayo
yanakuwa na sifa ya kutolewa Taarifa.
Alisema katika kipindi cha mwaka 2020 Bodi hiyo, imejipanga kumaliza kuchambua maamuzi
kwa ajili ya Kitabu cha Mwaka 2018, 2019 na 2020 ili kuendana na wakati ili kufikia hatua ya kutoa Taarifa kwa awamu mbili
hadi nne katika kila mwaka kuanzia mwaka wa fedha 2020/2021.
Mwenyekiti huyo alisisitiza kwamba hatua ijayo ya kutoa
taarifa za majuzuu kwa awamu inatokana na uwezo mkubwa wa Bodi wa sasa wa
kupokea maamuzi mengi kwa njia ya teknolojia.
Bodi hiyo kwa sasa inafikiwa na Maamuzi ya Mahakama Kuu na
Mahakama ya Rufani 3,000 hadi 4,500 kwa uwiano wa maamuzi 300 hadi 400 kwa mwezi
kabla ya uchambuzi.
Maamuzi yote yatakayopitiwa na Bodi
yatakabidhiwa kwa mzabuni atakaeandaa Taarifa za Majuzuu ya Sheria kwa nakala laini
na ngumu. Nakala laini zitawekwa katika mifumo ya kupandisha taarifa za Sheria
ya Mahakama ya Tanzania kwa rejea rahisi na nakala ngumu kusambazwa kwa wadau
na Taasisi.
Akizungumzia kuhusu faida ya Majuzuu
hayo ya Taarifa za Sheria, alisema husaidia wadau kufuata Maamuzi ya Mahakama za
Juu katika kutafuta haki zao na pia Mahakama za chini kufuata misingi ya
kisheria iliyowekwa na maamuzi ya Mahakama za Juu.
Faida nyingine za taarifa za majuzuu
hayo ni kusaidia Mahakama za Juu kutotofatiana katika misingi ya kisheria (Conflicting
Decisions) na kufuata misingi na taratibu za Maamuzi iliyojiwekea.
‘Taarifa hizi za majuzuu ya sheria
husaidia pia katika kuendeleza ufahamu
wa kisheria mfano,Ofisi za Mawakili, Taasisi za Elimu ya Sheria, Magereza, Mashirika
ya Misaada ya Sheria na Taasisi na Idara Mbalimbali za Sheria, alisisitiza.
Bodi hiyo ina wajumbe 12, ambao ni Majaji
kutoka Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu kwa upande wa Bara na
Zanzibar, wawakili wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa pande zote
mbili. Wajumbe wengine wawakilishi kutoka wanasheria binafsi wa pande hizo,
Bodi hiyo hufanya vikao vyake mara nne kwa mwaka.
Mwenyekiti wa Bodi ya
Udhamini ya Taarifa ya Majuzuu ya
Sheria,ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Jacobs Mwambegele
(kushoto) akisisitiza jambo kwenye kikao
hicho.Kulia ni Katibu wa Bodi hiyo, Profesa Hamudi Majamba.
Baadhi ya wajumbe
wakifuatilia kikao hicho.
Baadhi ya wajumbe Bodi ya Udhamini wa Taarifa ya Majuzuu ya Sheria wakiendelea na kikao katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Sheria kwa Vitendo, iliyopo Barabara ya Sam Nujoma, jijini Dar es Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni