Jumatatu, 20 Januari 2020

MAHAKAMA YAWANOA MAJAJI UANDISHI WA HUKUMU



Na Ibrahim Mdachi - IJA Lushoto
Majaji wa Mahakama ya Rufani pamoja na wa Mahakama kuu ya Tanzania leo wameanza mafunzo ya siku tano yanayolenga kuwajengea uwezo wa namna bora ya uandishi na uandaaji wa hukumu, uamuzi mdogo na amri mbalimbali za Mahakama.

Mafunzo hayo yanatolewa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na  yanawajumuisha  jumla ya Majaji 25 ambapo kati yao, (10) ni kutoka Mahakama ya Rufani na 15 wa Mahakama Kuu.  

Sambamba na Mafunzo hayo, Mahakama pia inawapatia mafunzo maalumu  madereva wa viongozi ambao ni madereva wa waheshimiwa Majaji hao ishirini na tano (25) kwa lengo la kuwaongezea ujuzi na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Akizungumzia mafunzo Majaji, Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Mratibu wa Mafunzo hayo Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe., Dkt Paul Kihwelo alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo endelevu ya muda mfupi kwa watumishi wa Mahakama ili kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa wakati kufuatia malengo ambayo Mahakama imejiwekea katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2015/16 - 2019/20).

Kuhusu mafunzo kwa madereva, Jaji Kihwelo alisema yamelenga kuwakumbusha misingi muhimu ya kuzingatia kama madereva wa viongozi ikiwemo kudumu katika nidhamu nzuri, kuzingatia itifaki, matunzo ya magari pamoja na kujali afya zao kabla na wakati wa safari ikiwemo huduma ya kwanza.

Vilevile mafunzo hayo yamelenga kuzitambua changamoto mbalimbali ambazo madereva hao wanakumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao na kukusanya mapendekezo kama suluhisho mbadala na kuyafanyia kazi.

Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania Bibi. Patricia Ngungulu aliwasisitiza washiriki hao umuhimu wa kuzingatia mafunzo ili kuondoa mapungufu yaliyopo na kuboresha utendaji kazi wa kila siku.

Kwa upande wao, Waheshimiwa Majaji wakielezea matarajio yao kwa nyakati tofauti walisema kuwa mafunzo hayo yatakuwa ni kichocheo kikubwa cha kuboresha mbinu mbalimbali za uandishi wa hukumu, uamuzi mdogo na amri mbalimbali na pia yatawaongezea weledi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku katika kuhakikisha utoaji wa haki kwa wakati unatendeka.

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt Paul Kihwelo akitoa neno la ukaribisho kwa washiriki wa mafunzo ya siku tano ya Majaji wa Mahakama ya Rufani pamoja na Mahakama Kuu ya Tanzania (hawako pichani) leo Lushoto .
Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Barke Mbaraka Aboud Sehel (kulia) akichangia jambo katika mafunzo hayo sambamba na mwezeshaji Prof. James Raymond (kushoto).
  Prof. James Raymond akiwasilisha mada kwa washiriki.
Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu wakiwa katika katika picha ya pamoja na mwezeshaji Prof. James Raymond (mbele katikati).

 Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania Bibi. Patricia Ngungulu akifungua mafunzo maalumu kwa madereva wa viongozi, (kulia) Mkuu wa Idara ya Sheria kutoka Kitengo cha Usalama barabarani Makao Makuu na mwezeshaji (SP) Deus Sokoni, (kushoto) ni Afisa wa Usafiri wa Mahakama Bw. Dionis Kishiwa.

Washiriki wakifuatilia kwa makini maelezo ya Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania Bibi. Patricia Ngungulu alipokuwa akifungua mafunzo maalumu kwa madereva wa viongozi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni