Jumanne, 21 Januari 2020

WATUHUMIWA 60 WA UTUPAJI TAKA NGUMU OVYO WAFIKISHWA MAHAKAMA INAYOTEMBEA


Na Magreth Kinabo – Mahakama

Mahakama Inayotembea leo imeendesha mashauri katika ngazi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine maarufu ‘ Mahakama ya Jiji’ kwa ajili ya kusikiliza mashauri mbalimbali ya watuhumiwa  wapatao 60, wa kosa la utupaji taka ngumu  ovyo   baada ya  Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam kufanya operesheni maalum.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mratibu wa Mahakama hiyo, ambaye pia ni Hakimu Mkazi, Mhe. Moses Ndelwa alisema watuhumiwa hao, wamekamatwa baada ya kupatikana na kosa la kuvunja  Sheria ya Mazingira namba mbili ya Mwaka 2004, pamoja na sheria ndogondogo  za jiji.

‘Tuko tayari tumejipanga vizuri kwa ajili ya kusikiliza mashauri haya, ambapo tumeandaa hati zao za mashtaka leo,  yanasikilizwa leo na kutolewa hukumu leoleo,’ alisema Ndelwa.

Aliongeza kuwa  mtuhumiwa akikiri kosa anatozwa faini ya kuanzia sh, 20,000/= na isiyozidi sh. 300,000/= kulingana na kosa, au kifungo kisichozidi miezi sita jela.

Mashauri hayo yameendeshwa na Hakimu Mkazi  wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Sokoine, Mhe. Anipha Mwingira, ambapo alisema kwa kundi la kwanza la watuhumiwa hao  16, kati yao 13 wamekiri kosa na wamekubali kulipa Sh. 20,000 kila mmoja, hawakukubali na mmoja hakufika mahakamani hapo.

Watuhumiwa hao, walikamatwa baada ya Manispaa ya Ilala kuendesha operesheni maalum, akizungumzia kuhusu suala hilo. Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bi. Sophia Mjema alisema zoezi hili itakuwa ni endelevu. Pia watuhumiwa hao walikamatwa kwa makosa ya kutupa ovyo taka ngumu mfano maganda ya pipi na chupa za maji ya kunywa.

Hivyo aliwataka wakazi wa eneo hilo kuacha tabia ya utupaji taka ovyo, badala yake watupe sehemu husika na kama hakuna waziweke mpaka watakapo pata mahali maalum pa kutupa ili kuepuka kufikishwa mahakamani.

‘Hii ni mara ya kwanza kwa Manispaa ya Ilala kufanya operesheni hii, na  mashauri kuendeshwa kwa kutumia mahakama hii. Pia tuna mpango wa kufanya operesheni nyingine  kwa ombaomba na anayempatia fedha ombaomba kwa kushirikiana jiji nzima, kwa kuwa tunataka kila mtu afanye kazi kama Mhe. Rais Dkt. John Magufuli anavyoelekeza,’ alisema Mjema.

Aliongeza kuwa ikiwa mtu anataka kutoa msaada aende katika vituo vya watoto yatima, kanisani au msikitini na si kutoa barabarani.

Hii ni mara ya pili kwa Mahakama Inayotembea kuendesha mashauri kupitia operesheni maalum, mara ya kwanza ilifanyika katika viwanja wa Biafra, Kinondoni, ambapo jumla ya watuhumiwa 100 walikamatwa kwa kosa la kutiririsha maji taka, katika mashauri 28.

Kwa mujibu wa Mhe. Ndelwa alisema watuhumiwa hao,  wengi walilipa faini isiyozidi Sh. 80,000/=.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bi. Sophia  Mjema (wa pili kushoto) akiwa katika gari la Mahakama Inayotembea leo kwa ajili  ya kusikiliza mashauri ya watuhumiwa wa utupaji wa taka ngumu ovyo baada ya kuvunja  Sheria ya Mazingira namba mbili ya Mwaka 2004, pamoja na sheria ndogondogo  za jiji , wakati gari  hilo likiwa ngazi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine maarufu  ‘Mahakama ya Jiji’ kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.Wa kwanza Kushoto ni Mratibu wa Mahakama Inayotembea, Mhe. Moses Ndelwa, ambaye pia ni Hakimu Mkazi na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Dar es Salaam. Mhe. Ruth Massam. 

Baadhi ya watuhumiwa  wa  kosa la utupaji taka ovyo, wakiwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam leo  kwa ajili ya kusikiliza mashauri yao kupitia gari la Mahakama Inayotembea, wakati gari  hilo likiwa ngazi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine  maarufu ‘Mahakama ya Jiji.



 Baadhi ya watuhumiwa  wa  kosa la utupaji taka ovyo, wakiingia  katika gari la Mahakama Inayotembea leo, wakati gari  hilo likiwa ngazi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine  maafrufu ‘Mahakama ya Jiji’ kwa ajili ya kusikiliza mashauri yao kwenye  viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.



 Baadhi ya watuhumiwa  wa  kosa la utupaji taka ovyo, wakiwa ndani ya   gari la Mahakama Inayotembea,   kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam leo  kwa ajili ya kusikiliza mashauri yao wakati gari  hilo likiwa ngazi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine  maarufu ‘Mahakama ya Jiji’.


Mkuu wa Wilaya ya Ilala,  Bi. Sophia Mjema (kushoto) akizungumza jambo  leo na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Mhe. Martha Mpaze ,wakati gari la Mahakama Inayotembea,  likiwa ngazi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine  maarufu ‘Mahakama ya Jiji’. 

Mkuu wa Wilaya ya Ilala,  Bi. Sophia Mjema (kulia) akizungumza jambo  leo na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Bw. Omary Kumbilamoto wakati gari la Mahakama Inayotembea,  likiwa ngazi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine  maarufu ‘Mahakama ya Jiji’ kwa ajili ya kuendesha mashauri.


Baadhi ya watuhumiwa  wa  kosa la utupaji taka ovyo, wakikwa   katika gari  kwa ajili ya kulipa faini baada ya kukutwa na kosa la utupaji taka ovyo,  wakati gari  la Mahakama Inayotembea ( halipo pichani) likiwa ngazi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine  maafrufu ‘Mahakama ya Jiji’ kwa ajili ya kusikiliza mashauri yao kwenye  viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

(Picha na Magreth Kinabo- Mahakama) 





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni