Na
Lydia Churi- Mahakama Singida
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt.Eliezer Mbuki Feleshi amezindua jengo la Mahakama ya Mwanzo
Iguguno na kuwataka watumishi wa Mahakama hiyo kuwa na maadili mema kwa
kupingana na vitendo vya rushwa na ukosefu wa maadili.
Akizungumza wakati wa hafla
ya uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Iguguno, Jaji Kiongozi amesema
Mahakama ya Tanzania ni Taasisi hivyo haiwezi kujishirikisha na vitendo vya
rushwa bali anayeshiriki vitendo hivyo ni mtu binafsi.
Amesema Mahakama inavyo
vyombo vya kisheria vya kushughulikia maadili ikiwemo kamati ya Maadili ya
Majaji na Kamati ya maadili ya Maafisa wa Mahakama.
Aidha, Dkt. Feleshi
ametoa wito kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa wilaya nchini kuongeza kasi katika kufuatilia malalamiko yanayotolewa
dhidi ya Watumishi wa Mahakama wakiwemo Mahakimu na kuchukua hatua stahiki pale
wanapokuwa na ushahidi wa kutosha.
“Watumishi wa Mahakama na
wananchi kwa ujumla tubadilike kwani haki hainunuliwi wala haiuzwi”, alisema
Jaji Kiongozi.
Kuhusu kuanzishwa kwa
masjala ndogo ya Mahakama ya wilaya ya Mkalama ndani ya jengo jipya la Mahakama
ya Mwanzo Iguguno, Jaji Kiongozi amesema masjala hiyo inaweza kuanzishwa endapo
wadau wanaofanya kazi na Mahakama wataridhia. Baadhi ya wadau hao ni Polisi,
Magereza, Takukuru, Mkemia Mkuu wa Serikali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na
Wakili Mkuu wa Serikali.
Akizungumzia mashauri ya
Mirathi, Dkt. Feleshi amesema Mahakama ina changamoto na mashauri hayo kwa kuwa
huchukua muda mrefu kumalizika kutokana na familia husika kuchelewesha au kutochagua
msimamizi wa mirathi mapema.
Kuhusu usikilizwaji wa
mashauri, Jaji Kiongozi amewataka Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo Iguguno
kumaliza mashauri kwa wakati kwani Mahakama ya Tanzania inapenda kuona mashauri
yaliyofunguliwa yanaisha siku hiyo hiyo na hili litawezekana endapo wanachi
watafika mahakamani na mashahidi.
Naye Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Mustapher Siyani aliwata
watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Iguguno kufanya kazi kwa kufuata maadili mema.
Jengo la Mahakama ya
Mwanzo Iguguno lilianza kujengwa na wananchi na baadaye mradi huo kuchukuliwa
na Mahakama ya Tanzania na kukamilika mwaka 2018 kwa gharama ya zaidi ya shilingi
milioni 115.
Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi
akikata utepe kuashiria uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Iguguno. Wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Dodoma Mhe. Mustapher Siyani akifuatiwa na Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar Mhe. Aziza Swedy na kulia ni Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki Mhe. Allan Kiula.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akifungua pazia kama ishara ya kuzindua jengo la Mahakama ya Mwanzo Iguguno. kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akisikiliza jambo wakati alipokuwa akikagua jengo la Mahakama ya Mwanzo Iguguno mara baada ya kulizindua leo. Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Singida Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Singida
Wananchi wa Iguguno wakiwa wamejitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi wa jengo l a Mahakama ya Mwanzo Iguguno.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni