Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka
watumishi wa Mahakama kutambua wajibu wao
na kutumia muda wa kazi ipasavyo kwa
kufanya kazi kwa bidii ili kuiwezesha Mahakama kutekeleza wajibu wake wa kutoa huduma bora kwa wananchi.
Jaji Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mkutano wa Baraza la
wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati
alipokuwa akifungua kikao cha siku mbili cha cha Baraza la Wafanyakazi wa
Mahakama.
Mhe. Prof. Juma pia amewakumbusha viongozi mbalimbali wa
Mahakama kuwapa watumishi taarifa muhimu zinazohusu maendeleo ya Taasisi mara
kwa mara hususan taarifa kuhusu maboresho, taratibu mpya, mafanikio na
changamoto za kila siku.
“Majadiliano, kueleweshana, kupokea mawazo na mapendekezo ya
wafanyakazi ni wajibu wetu wa kila siku bila kusubiri vikao”, alisema Jaji Mkuu
na kuwasisitiza viongozi hao kuwa na vikao vya mara kwa mara na watumishi ili
kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili.
Alisema ili watumishi waelewe malengo na muelekeo wa Mhimili ni
lazima Viongozi wajenge mazingira ambayo watumishi wote watakuwa wanapata
taarifa za mara kwa mara kuhusu mambo muhimu yanayogusa ajira, maslahi na mazingira
ya kazi.
Alisema umuhimu wa Baraza la Wafanyakazi ni kutoa fursa kwa
watumishi kujadiliana na uongozi wa Taasisi zao juu ya masuala ya msingi
yanayohusu tija na ufanisi kwa upande mmoja na maslahi yao kama watumishi kwa
upande mwingine.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, hatua kubwa za kimaendeleo zilizofikiwa
na Mahakama ya Tanzania katika kipindi cha miaka minne (4) hasa katika
uboreshaji wa Mahakama zimechangiwa na watumishi wote wa Mahakama wa ngazi na
fani zote.
“Nyuma ya kila mafanikio ya Mahakama wapo watumishi wengi wa
kawaida, waadilifu, wanaochapa kazi kwa kujituma, na ambao hufanya kazi zao
bila kujisifu, lakini matokeo ya kazi na juhudi zao ni kubwa kwa kuwa ndio wanaotoa
sura ya mafanikio ya Mahakama inayosifiwa”, alisema.
Aliwataka viongozi katika sehemu zote na ngazi zote ndani ya
Mahakama kuhakikisha watumishi wanahusishwa,
wanathaminiwa, wanahamasishwa na wanawekewa mazingira bora ili watoe huduma
zenye tija na kuwa wenye furaha siku zote.
Akizungumzia sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Namba 4 ya
mwaka 2011, Jaji Mkuu amesema sheria hii
imejenga tabia mpya ya uwazi, uwajibikaji na matumizi bora ya rasilmali. Sheria
hii pia imejenga tabia mpya ya kufanya kazi, kukubali, kuheshimu na kukaribisha
baadhi ya utaaalamu wa ndani, katika fani mbali mbali kama vile TEHAMA, Uhandisi,
Uchumi, na Mipango.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bwn. Mathias Kabunduguru
amesema Mahakama ya Tanzania haina budi kufanya mageuzi mbalimbali ili kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa
viwango vya kitaifa, kikanda, na kimataifa vinavyokubalika.
Kuhusu rushwa, Bwn. Kabunduguru amesema juhudi zimefanyika
kupambana nayo ikiwa ni pamoja na kuweka mifumo ya utendaji kazi iliyo wazi na
yenye ufanisi ikiwemo wananchi kupewa fursa ya kulalamika, kupongeza na kutoa
maoni kupitia simu za kiganjani zilizosambazwa nchi nzima na madawati ya
malalamiko yaliyopo karibu kila ngazi ya Mahakama.
Mkutano wa tatu wa Baraza kuu la sita la wafanyakazi wa Mahakama
ya Tanzania wa umeanza leo jijini Dodoma ambapo wawakilishi wa watumishi wa
Mahakama kutoka maeneo mbalimbali nchini wanahudhuria.
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wakiimba wimbo wa Mshikamano (Solidarity Forever) mara baada ya kuanza Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi leo jijini Dodoma.
Baadhi ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi ulioanza leo jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania Bwn. Kalege Enock akitoa Mada kuhusu Matumizi ya Tehama ndani ya Mahakama, leo katika Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi jijini Dodoma.
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi ulioanza leo jijini Dodoma.
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wakiimba wimbo wa Mshikamano (Solidarity Forever) mara baada ya kuanza Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi leo jijini Dodoma.
Baadhi ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi ulioanza leo jijini Dodoma.
Baadhi ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wakisikiliza Mada kwenye Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi ulioanza leo jijini Dodoma. Katikati ni Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma na kushoto ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Bibi. Rose Tengu.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (kushoto) na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmila Sarwatt wakifuatilia Mada.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bwn. Mathias Kabunduguru (kulia) na Msajili wa Mahakama ya Rufani Mhe. Kelvin Mhina wakiwa kwenye Mkutano. Katikati ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi leo jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania Bibi. Rose Tengu akizungumza.
Mtendaji wa Mahakama ya Rufani Bwn. Solanus Nyimbi akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni