Na
Lydia Churi-Mahakama Dodoma
Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ameiomba ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutenga bajeti kwa ajili ya kamati za Maadili za
Maafisa wa Mahakama za Mikoa na wilaya ili ziweze kutekeleza majukumu yake kama
sheria inavyozitaka ikiwa ni pamoja na kukutana na kuwasilisha taarifa zake kwa
Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Kamati za Maadili za
Maafisa wa Mahakama zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya kutotekeleza
majukumu yake kwa mujibu wa sheria kutokana na upungufu wa bajeti. Kamati hizi ziliundwa baada ya kutungwa kwa
sheria ya Usimamizi wa Mahakama namba 4 ya mwaka 2011.
Akizindua Mwongozo wa
Uendeshaji wa kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama leo jijini Dodoma,
Waziri Mahiga amesema Serikali kupitia wizara ya Katiba na Sheria itahakikisha
Tume ya Utumishi wa Mahakama inapatiwa rasilimali fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli zake ikiwemo
Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama
kwa ufanisi unaotakiwa.
Amewataka wajumbe wa
kamati hizo kuutumia mwongozo huo wa uendeshaji kuondoa changamoto mbalimbali
zilizokuwepo kwani matarajio ya Tume na Serikali ni kuona utekelezaji wa majukumu
unaozingatia matakwa ya sheria, kanuni na taratibu.
Alisema kwa kuona umuhimu
wa kuimarisha dhana ya utawala bora kupitia sheria ya uendeshaji wa Mahakama,
Serikali imeruhusu uwepo wa kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama ambazo ni pamoja
na; Kamati ya Maadili ya Majaji, Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama na Kamati
ya Maadili ya Mahakama ya Mkoa na wilaya.
Kwa mujibu wa Waziri
Mahiga, kamati hizi zina nafasi kubwa katika kusimamia, kuendeleza na kudumisha
maadili ya Utumishi wa Mahakama. Aliongeza kuwa suala la kuwapatia wajumbe wa
kamati Mwongozo huo ni suala la msingi kwani sasa watatekeleza majukumu yao kwa
kufuata msingi wa sheria, kanuni na taratibu.
Akizungumzia Maadili kwa
watumishi wa Mahakama, Waziri Mahiga amewataka watumishi wachache wanaoendelea na vitendo vya ukiukaji wa
maadili kuacha mara moja ili kulinda heshima ya Mhimili wa Mahakama na pia kwa
usalama wa ajira zao.
Aidha amesema wananchi
wengi bado hawafahamu uwepo wa kamati za maadili na majukumu yake ambapo
wamekuwa wakipeleka malalamiko yao dhidi ya Maafisa wa Mahakama kwenye Mamlaka
zisizo sahihi na hivyo kupoteza muda mwingi.
Ameitaka Tume ya Utumishi
wa Mahakama kutoa Elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya uendeshaji wa Kamati za
Maadili na huduma zinazotolewa na kamati hizo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza kwa niaba ya wakuu wote wa mikoa nchini
amesema kupitia Mwongozo uliozinduliwa, Serikali imeruhusu uwepo wa wa sura ya
utendaji wa pamoja baina ya mihimili yote mitatu ya dola.
Alisema palipo na Maadili
pana amani, haki, uaminifu katika utendaji kazi, umoja na ushirikiano. Aliongeza
kuwa kuwepo kwa maadili pia ni ni kichocheo cha Maendeleo ya Taifa.
Aidha Dkt. Nchimbi
alisema suala la uwepo wa Maadili miongoni mwa watumishi wa Mahakama ya
Tanzania husaidia kuifanya Mahakama kuwa rafiki na karibu zaidi na wananchi.
Kamati za Maadili za Maafisa
wa Mahakama ngazi za mikoa na wilaya huongozwa na Wakuu wa Mikoa na Wilaya
ambao hupokea na kuchunguza malalamiko dhidi Mahakimu wa Mahakama za Hakimu Mkazi,
Mahakama za wilaya na Mahakama za Mwanzo.
Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akizindua Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama leo jijini Dodoma. Kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na kulia ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Mhe. Josephat Kandege. Aliyeshika vitabu vya Mwongozo ni Katibu Msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Bibi. Enziel Mtei.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akiwa ameshika kitabu cha Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama baada ya kuzindua leo jijini Dodoma. Wa pili kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na wa pili kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akifuatiwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Mhe. Josephat Kandege. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi na wa kwanza kulia ni Mkuu wa wilaya ya Dodoma Bwn. Patrobasi Katambi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akiwa kwenye hafla ya Uzinduzi wa Mwongozo wa Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama. Kulia ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmila Sarwatt na kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Dodoma Bwn. Patrobasi Katambi.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akizungumza wakati wa hafla ya Uzinduzi.
Viongozi mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama.
Viongozi mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama.
Viongozi mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama.
Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja na Meza Kuu wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama.
Viongozi mbalimbali wa Mahakama wakiwa katika picha ya pamoja kwenye hafla ya uzinduzi wa Mwongozo wa Uendeshaji wa
Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni